Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAONI YA MHARIRI: Uhuni huu wa wanasoka kwa wanahabari haukubaliki asilan

UHUNI na vitendo vya wachezaji kujichukulia sheria mikononi dhidi ya wanahabari vimeendelea tena baada ya majuzi, mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa kumshambulia kwa kipigo mpiga picha wa magazeti ya  New Habari Ltd.

Inaelezwa kuwa, Mzambia huyo aliamua kumshambulia mpiga picha huyo John Dande kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati timu yake ikifanya mazoezi kwa kukerwa na kitendo cha kupigwa picha akifanya mazoezi.

Beki wa pembeni wa Yanga, Juma Abdul aliyekuwa karibu na tukio hilo ndiye aliyelazimika kuingilia kati na kumwokoa mpigapicha huyo asiendelee kudhuriwa zaidi na mashambulizi ya Chirwa anayedaiwa alikuwa na hasira kali.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa soka, tunalaani na kukemea vikali tukio hilo ambalo sio la kiuanamichezo lililofanywa na mchezaji huyo raia wa kigeni.

Ingawa bado haijafahamika chanzo halisi kilichosababisha Chirwa kumshambulia Dande, lakini kwa vyovyote ilivyo, alichokifanya Mzambia huyo sio sahihi kwa kuzingatia yeye ni mchezaji wa kimataifa anayejua umuhimu wa wanahabari na hata sheria za nchi.

Kwa mchezaji wa kulipwa kama yeye tena mwenye jina kubwa katika soka la Afrika, kwani amecheza katika klabu tofauti nje ya taifa lake la Zambia ikiwamo FC Platinum ya Zimbabwe. Hivyo hakuna aliyetarajia kufanya kitendo kama hicho.

Ikumbukwe kuwa hii sio mara ya kwanza kwa wachezaji kugeuka mabondia na kuwashambulia wanahabari, kwani mwaka jana kiungo wa Simba Mwinyi Kazimoto alimshambulia na kumjeruhi kwa kipigo mwandishi wa gazeti hili, Mwanahiba Richard, japo baadaye Mahakama ya mjini Shinyanga lilipotokea tukio hilo ilimuacha huru kwa kutomkuta na hatia yoyote.

Lakini, watu wakiwa wameshasahau tukio hilo la Shinyanga, Chirwa amekirejea tena kitendo hicho mbele ya viongozi, makocha na wachezaji wenzake jambo linaloonyesha wazi ni namna gani mchezaji huyo asivyojiheshimu.

Ameshindwa kuheshimu taaluma yake kadhalika taaluma ya wanahabari ambao, wamekuwa msaada mkubwa kwake tangu alipotua nchini akitokea Zimbabwe.

Ingawa tayari suala hili lipo kwenye vyombo vya dola kwa sasa, lakini sisi kama wadau wa michezo hususani soka tuna kila sababu ya kulaani matukio ya aina hii dhidi ya wanahabari kwani, ni kuwaingilia katika majukumu yao ya kazi.

Wanahabari wana mchango mkubwa katika mafanikio ya wachezaji na hata watu wengine kwa namna wanavyoripoti matukio yao. Hakuna asiyefahamu vyombo vya habari vilivyomsaidia Chirwa wakati alipotua Yanga na kushindwa kuonyesha ubora wake.

Ni vyombo vya habari vilivyomkingia kifua kwa kusaidia kuelimisha waliokuwa na haraka ya kutaka kuona Mzambia huyo anaonyesha ubora kwa kusisitiza apewe muda akae vema kabla ya kurudi kwenye kasi yake na kupata sifa kubwa.

Hata hivyo, ni kama vile Chirwa amesahau mchango mkubwa wa wanahabari wakiwamo wapiga picha ndiyo iliyomfikisha hapo alipo, kiasi cha kufikia hatua ya kumdunda mtu. Hii kwa hakika haikubaliki na hatuwezi kunyamazia kabisa.

Tunajiuliza tu, hivi kama Juma Abdul hakuwa karibu na kuamulia, hasira za Chirwa zingemuacha vipi mpiga picha aliyemshambulia?

Imefika wakati wachezaji na wadau wa michezo kuthamini, kuheshimu na kujali kazi kubwa ya wanahabari kwani, wamekuwa mhimili wa maendeleo ya soka nchini hususani kuwapiga tafu wachezaji wa soka ndani na nje.

Tunaamini wazi kuwa wachezaji na wanahabari ni watu wanaotegemeana, hivyo wanapaswa kushirikiana na isifikie hatua ikaamuliwa vyombo vya habari kuacha kuripoti habari za Yanga kutokana na mwenendo kama huo.

Kimsingi inapotokea kukwaruzana kwa bahati mbaya katika kazi kwa watu hawa wawili, hakuna mwenye ruksa ya kujichukulia sheria mkononi. Kila mtu anapokerwa na jambo akiamua kujichukua sheria mikononi dhidi ya mwingine, hatuwezi kufika mbali na ni kuvunja sheria na kujengeana uhasama usio na  sababu.

Tunasisitiza kuwa vitendo hivyo vya kihuni dhidi ya wanahabari visinyamaziwe na visijirudie kwa maendeleo ya soka la Tanzania.