Mambo ya kufanya kuzuia miguu kupasuka
Muktasari:
- Kwa baadhi ya watu, hali hiyo huonekana kama tatizo dogo la urembo, lakini ikiachwa bila uangalizi inaweza kusababisha maumivu, kutokwa na damu na hata maambukizi. Wataalamu wa afya wanashauri watu kuzingatia usafi, kulainisha ngozi na kuvaa viatu vinavyofaa ili kupunguza uwezekano wa miguu kupasuka.
Magaga ya miguu ni tatizo linalowasumbua watu wengi, hasa katika sehemu za visigino na ngozi hukauka, kuwa ngumu na hatimaye kupasuka.
Kwa baadhi ya watu, hali hiyo huonekana kama tatizo dogo la urembo, lakini ikiachwa bila uangalizi inaweza kusababisha maumivu, kutokwa na damu na hata maambukizi. Wataalamu wa afya wanashauri watu kuzingatia usafi, kulainisha ngozi na kuvaa viatu vinavyofaa ili kupunguza uwezekano wa miguu kupasuka.
- LAINISHA NGOZI YA MIGUU
Miongoni mwa sababu zinazochangia magaga ni ngozi kukauka. Hali hiyo inaweza kufanya visigino kuwa vigumu na kuanza kupasuka, hasa mtu anapotembea au kusimama kwa muda mrefu.
Daktari Dorcas Natse anashauri kuwa hatua ya msingi ya kuzuia tatizo hilo ni kuhakikisha ngozi ya miguu inapata unyevunyevu wa kutosha.
“Ni muhimu mtu kujenga mazoea ya kupaka mafuta mazito au malaini yatakayo lainisha ngozi kila siku, hasa baada ya kuoga. Baada ya kukausha miguu vizuri, anaweza kupaka kilainishi kwenye visigino ili kuzuia ngozi isikauke na kupasuka,” anashauri daktari huyo.
2. OSHA MIGUU NA KAUSHA VIZURI
Kuosha miguu ni sehemu muhimu ya utunzaji wa mwili. Inashauriwa kutumia maji ya uvuguvugu na sabuni isiyokausha ngozi kupita kiasi.
Baada ya kuosha, miguu inapaswa kukaushwa kwa upole, hasa katikati ya vidole. Matumizi ya maji ya moto sana au kuloweka miguu kwa muda mrefu yanaweza kuongeza ukavu wa ngozi, hivyo ni vizuri kuepuka mazoea hayo.
3. VAA VIATU VISIVYOBANA
Viatu vina nafasi kubwa katika kulinda miguu dhidi ya msuguano na shinikizo linaloweza kuchangia kupasuka kwa visigino. Viatu vinavyobana sana au vilivyo wazi sehemu ya nyuma vinaweza kuongeza tatizo kwa baadhi ya watu.
Daktari Dorcas Natse anasema watu kuchagua viatu vinavyolingana na ukubwa wa miguu yao na vinavyoshikilia vizuri visigino.
“Viatu vinavyofaa husaidia kulinda visigino dhidi ya msuguano na shinikizo. Ni vizuri pia kuepuka kutembea bila viatu kwenye sehemu zenye ukali au vumbi, kwa sababu zinaweza kujeruhi ngozi au kuongeza ukavu zaidi na kupasuka,” anasema.
4 .ONDOA NGOZI NGUMU
Ngozi inapokakamaa, mtu anaweza kutumia jiwe maalumu la kusugulia miguu kwa upole baada ya kuilowesha kwa muda mfupi kwenye maji ya uvuguvugu. Hata hivyo, hatua hiyo inapaswa kufanyika kwa uangalifu ili kuepuka kujeruhi ngozi.
Wataalamu wa afya wanashauri kuepuka kutumia wembe, visu au vifaa vyenye ncha kali kukata magaga, kwa sababu vinaweza kusababisha majeraha na maambukizi.
5. KUNYWA MAJI YA KUTOSHA
Kunywa maji ya kutosha na kula vyakula vyenye virutubisho husaidia kudumisha afya ya mwili, ikiwemo ngozi. Ni muhimu kula mlo kamili unaojumuisha matunda, mboga za majani, protini na vyakula vingine vyenye virutubisho muhimu.
Hata hivyo, maji pekee hayawezi kuondoa magaga yaliyokwishatokea. Utunzaji wa ngozi na kutumia kilainishi kinachofaa ni hatua muhimu zaidi katika kupunguza ukavu wa visigino.
6. WAHI KITUO CHA AFYA
Mtu ambaye tayari ana magaga yaliyopasuka anapaswa kuchukua tahadhari, hasa ikiwa ngozi ina maumivu makali, inavuja damu, inatoa usaha au imekuwa nyekundu na kuvimba. Watu wenye kisukari wanapaswa kuwa waangalifu zaidi na kutafuta ushauri wa mtaalamu wa afya mapema, kwa sababu majeraha ya miguu yanaweza kuwa magumu kupona.