Fanya hivi ngozi yako isipauke wakati wa baridi
Muktasari:
- Usipaniki wala kukimbilia kubadilisha bidhaa zako zote za urembo. Mara nyingi, mabadiliko hayo yanaweza kuhusishwa na ukavu wa ngozi unaochochewa na hali ya hewa ya baridi, upepo, maji ya moto na namna unavyoitunza ngozi katika kipindi hicho.
WAKATI wa baridi kuna watu hubadilika ghafla, si tabia wala mavazi, bali ngozi. Mwingine huanza kuonekana mweusi zaidi, mwingine ngozi inapauka, huku mwingine akibaki anajiuliza kwa nini mwili wake hauna tena ule mwonekano aliouzoea.
Uso unaweza kuanza kukosa mng’ao, mikono ikawa na ukakasi, miguu kuonekana kama imepakwa unga na midomo kuanza kuchanika. Hapo ndipo maswali huanza, “Kwani nimebadilika rangi?” au “Mbona ngozi yangu imekuwa hivi?”
Usipaniki wala kukimbilia kubadilisha bidhaa zako zote za urembo. Mara nyingi, mabadiliko hayo yanaweza kuhusishwa na ukavu wa ngozi unaochochewa na hali ya hewa ya baridi, upepo, maji ya moto na namna unavyoitunza ngozi katika kipindi hicho.
Na kama unadhani suluhisho ni kujipaka kila krimu unayoiona, subiri kwanza! Kuna mambo machache muhimu ya kufanya ili kuisaidia ngozi yako ibaki na unyevunyevu, ulaini na mwonekano mzuri hata baridi inapokaza.
TUMIA MAFUTA MALAINI
Usisubiri ngozi ianze kukakamaa ndipo ukumbuke kilainishi. Wakati wa baridi, ngozi inaweza kupoteza unyevunyevu kwa haraka, hivyo ni muhimu kutumia mafuta malaini na siyo mgando. Hii husaidia kuhifadhi unyevunyevu kwenye ngozi na kupunguza ukavu.
USIOGE MAJI MOTO SANA
Najua baridi ikikamata, maji ya kawaida yanaweza kuonekana kama adhabu. Lakini usigeuze bafu kuwa sehemu ya kuchemsha ngozi yako.
Maji yenye joto kali yanaweza kuondoa mafuta ya asili yanayolinda ngozi na kuifanya ikauke zaidi. Tumia maji ya uvuguvugu, usitumie ya moto sana.
KUNYWA MAJI HATA KAMA HUNA KIU
Usisubiri kiu ikupige ndipo unywe maji. Wakati wa baridi watu wengi hupunguza unywaji wa maji kwa sababu hawatokwi na jasho sana kama wakati wa joto.
Mwili bado unahitaji maji, hivyo endelea kunywa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili wako. Hii ni sehemu ya utunzaji wa mwili kwa ujumla.
ACHA KUSUGUA NGOZI KUPITA KIASI
Kama ngozi imeanza kukauka, usifikiri suluhisho ni kuisugua kwa nguvu kila siku. Kusugua kupita kiasi kunaweza kuongeza muwasho na kuharibu mafuta ya asili ya ngozi.
Safisha ngozi kwa upole na epuka bidhaa zenye kemikali kali ambazo zinaifanya ngozi iwe kavu zaidi.
LINDA MIDOMO YAKO
Midomo nayo haijasaini mkataba wa kuvumilia baridi bila ulinzi. Wakati wa baridi inaweza kukauka na kuchanika kwa urahisi. Tumia kilainishi cha midomo mara kwa mara na epuka tabia ya kulamba midomo kila baada ya muda mfupi kwa sababu hali hiyo inaweza kuongeza ukavu.
USIACHE KINGA YA JUA
Baridi haimaanishi jua limeondoka duniani. Mionzi ya jua bado inaweza kuathiri ngozi hata siku zenye mawingu. Kwa hiyo, kama unatumia kinga ya jua katika utaratibu wako wa kawaida wa kutunza ngozi, endelea kuitumia kulingana na mahitaji yako.
CHAGUA SABUNI
Sabuni kali inaweza kuifanya ngozi ipoteze mafuta yake ya asili. Wakati wa baridi, hali hiyo inaweza kuongeza ukavu. Chagua bidhaa ya kusafisha ngozi ambayo ni laini na inayofaa aina ya ngozi yako. Si kila bidhaa inayomfaa mtu mwingine itakufaa wewe.
USIBADILISHE MAFUTA KILA SIKU
Ngozi ikianza kubadilika wakati wa baridi, usikimbilie kutumia kila bidhaa unayoiona kwenye mitandao. Kubadilisha bidhaa mara kwa mara kunaweza kuichanganya ngozi na wakati mwingine kuongeza tatizo.
Kama ukavu au mabadiliko ya ngozi ni makubwa, yanaendelea, yanaambatana na kuwasha, maumivu, vidonda au magamba mengi, ni vizuri kupata ushauri wa mtaalamu wa afya.
USHAURI
Baridi si sababu ya kuikabidhi ngozi yako kwa ukavu. Maji ya uvuguvugu, kilainishi kinachofaa, kunywa maji ya kutosha, sabuni laini, lishe bora na kujikinga na mazingira makavu vinaweza kusaidia ngozi kubaki katika hali nzuri.