Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za mba kichwani, mwilini

UREMBO Pict

Muktasari:

  • Mbaya zaidi, akivaa nguo nyeusi mabegani unaona kama unga mweupe umetapakaa inasemwa “Huyu ana uchafu kichwani!”

KUNA watu wakiona mtu anajikuna kichwani, tayari wanamwangalia kwa jicho la pembeni kana kwamba hajawahi kukutana na maji ya kuoga.

Mbaya zaidi, akivaa nguo nyeusi mabegani unaona kama unga mweupe umetapakaa inasemwa “Huyu ana uchafu kichwani!”

Kumbe si kila mba inatokana na uchafu. Wakati mwingine ni ngozi yenye mafuta mengi, ukavu, bidhaa za nywele au changamoto nyingine za ngozi zinazoweza kumfanya mtu ajikute anavaa 'unga' begani bila hata kuagiza.

Tatizo hili halihusishi ngozi ya kichwa pekee. Magamba yanayofanana na mba yanaweza pia kujitokeza katika sehemu mbalimbali za mwili, hasa maeneo yenye mafuta mengi kama usoni, pembeni mwa pua, nyuma ya masikio, kifuani na mgongoni.


MAFUTA YA NGOZI

Moja ya mambo yanayoweza kuchangia mba ni uzalishaji mkubwa wa mafuta kwenye ngozi. Mafuta hayo yakizidi yanaweza kuathiri mazingira ya ngozi na kuchochea kuchubuka.

Daktari wa ngozi, Dorcas Natse anasema watu wenye ngozi yenye mafuta wanapaswa kuwa makini zaidi na hali hiyo.

“Uzalishaji mkubwa wa mafuta kwenye ngozi unaweza kuchangia kuonekana kwa mba, hasa kwenye ngozi ya kichwa na maeneo mengine yenye mafuta. Hii haimaanishi mtu mwenye mba ni mchafu, bali kuna mabadiliko yanayotokea kwenye ngozi,” anasema.


URE 02

FANGASI WA KAWAIDA

Ngozi ya binadamu huwa na viumbe wadogo wanaoishi juu yake bila kusababisha tatizo katika hali ya kawaida. Hata hivyo, mazingira yakibadilika, baadhi yao wanaweza kuhusishwa na kuongezeka kwa mba.

Fangasi wanaoishi kwenye ngozi wanaweza kutumia mafuta ya ngozi na kusababisha muwasho pamoja na kuchubuka kwa ngozi kwa baadhi ya watu.

Mabadiliko hayo yanaweza kufanya vipande vya ngozi vionekane zaidi kichwani au kwenye maeneo mengine ya mwili.


URE 04

NGOZI KAVU

Wakati mwingine mba unaweza kuhusishwa na ngozi kuwa kavu. Mtu anapokuwa na ukavu mkubwa wa ngozi, seli zilizokufa zinaweza kujikusanya na kuonekana kama vipande vidogo vyeupe.

Hali hii inaweza kuongezwa na kutumia maji ya moto sana, sabuni kali au bidhaa zinazokausha ngozi.


URE 03

BIDHAA ZA NYWELE

Mafuta, dawa za nywele, rangi, sabuni na bidhaa nyingine zinaweza kumkera mtu mwenye ngozi nyeti. Muwasho huo unaweza kusababisha ngozi kuchubuka na mtu kudhani ana mba.

Daktari wa ngozi Nathanael Jonas, anasema ni muhimu mtu kutambua bidhaa zinazomletea tatizo.

“Bidhaa za nywele zinaweza kusababisha muwasho au mzio kwa baadhi ya watu. Mtu akiona mba au magamba yameanza baada ya kutumia bidhaa fulani, anapaswa kuacha kuitumia na kuangalia kama hali inabadilika,” anasema.


MSONGO WA MAWAZO

Msongo wa mawazo pia unaweza kufanya matatizo ya ngozi kuwa makali zaidi kwa baadhi ya watu. Mtu mwenye mba anaweza kuona kuwasha na kuchubuka kunaongezeka wakati anapokuwa kwenye kipindi cha mawazo mengi au uchovu.

Hii inatokana na kutokujijali, kuna watu wakipitia kipindi kigumu wanajisahau kujijali hasa kwenye kutunza miili yao kuanzia ngozi ya mwili mpaka kichwani.


URE 01

MAGONJWA YA NGOZI

Si kila ngozi inayochubuka ni mba ya kawaida. Baadhi ya magonjwa ya ngozi yanaweza kusababisha magamba kichwani au mwilini na kuhitaji matibabu maalumu.

Miongoni mwa hali hizo ni ugonjwa unaosababisha ngozi kuwa na magamba mazito, pamoja na maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya kichwa ambayo yanaweza kuambatana na kukatika au kupotea kwa nywele.

Kwa hiyo, mtu anayesumbuliwa na mba ya muda mrefu, kuwasha sana, vidonda, maumivu au kupoteza nywele anashauriwa kumuona mtaalamu wa afya badala ya kuendelea kubadilisha bidhaa za nywele bila kujua chanzo.

Kwa kifupi, mba inaweza kuchochewa na mafuta mengi ya ngozi, ukavu, fangasi, bidhaa za nywele, msongo wa mawazo na baadhi ya magonjwa ya ngozi. Kutambua chanzo ndiyo hatua muhimu ya kupata suluhisho sahihi.