Mambo matano Ngao ya Jamii Wanawake 2026
Muktasari:
- Kichapo hicho kinaifanya Yanga kucheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Mashujaa Queens iliyotandikwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens ambayo itaumana na Simba Oktoba 03 kutetea taji la tatu mfululizo.
MAMBO bado magumu kwa Wananchi! ndiyo Yanga Princess imepoteza tena taji ililokuwa inalisaka kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake mwaka 2018 ikikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya watani zao Simba Queens.
Kichapo hicho kinaifanya Yanga kucheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Mashujaa Queens iliyotandikwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens ambayo itaumana na Simba Oktoba 03 kutetea taji la tatu mfululizo.
Tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2023, ni timu mbili tu zilizobeba taji hilo, Simba iliyokuwa bingwa wa kwanza wa kihistoria na JKT Queens iliyonyakua mara mbili mfululizo mwaka 2024 na 2025.
Huu hapa ni uchambuzi wa kina wa kiufundi, mbinu za mchezo na maeneo yaliyoamua mchezo huo wa kukata na shoka.
MBINU
Simba Queens iliingia uwanjani ikiwa na mbinu ya kutawala eneo la kiungo wa kati na kushambulia kwa kasi kutokea pembezoni mwa uwanja. Elizabeth Joseph ndiye alikuwa silaha ya siri ya kocha Mussa Hassan Mgosi.
Corazone Aquino alionyesha ukomavu mkubwa katika kupanga na kuratibu mashambulizi kutoka nyuma, akishirikiana vyema na Mary Siyame kutengeneza presha ya mapema kwenye safu ya ulinzi ya Yanga Princess. Corazone alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti kali na la ufundi lililomshinda kipa wa Yanga.
Kwa upande wa Yanga Princess, walianza mechi wakiwa na nidhamu ya kujilinda kwa nguvu na kujaribu kushambulia kwa kushtukiza. Mbinu hii ilionekana kufanya kazi katika dakika 20 za mwanzo kabla ya safu yao ya kiungo kupoteza mwelekeo kwa sababu ya presha ya Simba.
KADI NYEKUNDU ILIVURUGA
Moja ya matukio yaliyoamua hatima ya mechi hiyo ni kadi nyekundu aliyoonyeshwa kiungo wa Yanga Princess, Ritticia Nabbosa, katika dakika ya 36 baada ya kumchezea madhambi makubwa kiungo wa Simba, Mary Siyame.
Kabla ya kadi hiyo, Yanga walikuwa bado wapo kwenye mchezo ingawa walikuwa nyuma kwa bao 1-0. Kadi hiyo nyekundu ilivuruga kabisa mipango ya mwalimu wa Yanga Princess Edna Lema.
Kuondoka kwa Nabbosa kuliacha nafasi kubwa katikati ya uwanja, na kuwapa Simba Queens uhuru wa kutawala umiliki wa mpira kwa zaidi ya 65%. Hivyo Yanga ililazimika kumtoa Fatuma Shagembe ambaye ni kiungo mkabaji na kumwingiza mshambuliaji Sandrine Mutuyimana.
Hivyo kupunguza kiungo mkabaji wakati ambao Nabbosa anayecheza kiungo namba nane tayari ametoka na kocha kumuingiza mshambuliaji kuliifanya safu ya ulinzi ya timu hiyo kukosa nguvu na kuruhusu Simba walisogelee lango lao mara wa mara.
MATUMIZI YA NAFASI
Baada ya Yanga kubaki pungufu, Simba Queens walitumia mwanya huo kupanua uwanja kwa kutumia mabeki wa pembeni Zainah Nandede na Fatuma Issa kupanda na kuongeza idadi ya wachezaji kwenye eneo la hatari la Yanga.
Pengo la idadi ya wachezaji lilifanya mabeki wa Yanga Princess, Akudo Ogbonna na Vera Afful kupoteza umakini na kusababisha safu ya ushambuliaji ya Simba kupenya kwa urahisi na kufunga mabao mengine mawili yaliyokamilisha ushindi wa 3-0.
Mbinu ya Simba ya kushinikiza kutoka juu iliwalazimisha mabeki wa Yanga kufanya makosa mengi ya pasi kwenye eneo lao la ulinzi, jambo lililowapa Wekundu wa Msimbazi nafasi ya kutengeneza nafasi nyingi za wazi.
USAJILI MPYA
Mechi hiyo imeonyesha wazi safu mpya ya Yanga Princess bado inahitaji muda zaidi wa kuelewana. Wachezaji wapya walioingizwa kikosini walionekana kupoteza ushirikiano pale timu ilipokutana na presha kubwa.
Katika mechi hiyo ni wachezaji wanne tu ndio walikuwepo msimu uliopita hivyo idadi iliyobaki wote hawaifahamu ligi wala ushindani wa mechi zenye presha kama dabi. Hilo lilikuwa kosa la kwanza Yanga msimu uliopita iliachana na wachezaji takribani 10 ambao walikuwa wanaanza kikosini, Aregash Kalsa kiungo mshambuliaji kutoka Ethiopia, Igwe Uzoamaka, Angel Chineneri mabeki waliokuwa na uwezo mkubwa wa kukaba na kuelewana vizuri hasa kwenye mipira ya juu.
Wengine ni kipa Rita Akarekor na ambao waliondolewa lakini ukiwatazama hawa waliosajiliwa hakuna utofauti mkubwa na wale waliondoka japo ni mapema na wanahitaji muda ili kuonyesha uwezo wao.
Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) inatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 23, na benchi la fundi la Yanga lina kibarua kizito cha kurekebisha nidhamu ya mechi, utulivu wa safu ya ulinzi, na maamuzi ya wachezaji wakiwa na mpira au bila mpira kabla ya ligi kuanza.
JKT NAYO INA KAZI
Licha ya JKT kushinda bao moja na kutinga fainali lakini nayo ina kazi ya kufanya hasa kwenye umaliziaji na utengenezaji wa nafasi.
Asilimia kubwa ya wachezaji walioanza kwenye mechi ya nusu fainali dhidi ya Mashujaa hawana uzoefu mkubwa wa ligi kwani wengi ni mabinti wadogo waliotoka kwenye timu mbalimbali na wengine wamekuwa wakipata nafasi ya kuanza mara chache.
Wachezaji wenye uzoefu kama Donisia Minja, Stumai Abdallah, Winifrida Gerald, Jamila Rajabu, Naijat Abbas hawapo kikosini na sababu za kutokuwepo ni pamoja na adhabu, majeraha na kuwa kwenye kozi ya ajira hilo ni kwa mujibu wa Kocha Kessy Abdallah.
Simba Queens wanaendelea kuthibitisha ubabe wao kwenye soka la wanawake nchini, wakionyesha ukomavu, nidhamu ya kiufundi na uwezo mkubwa wa kutumia makosa ya mpinzani. Ushindi huu siyo tu umewapeleka Fainali ya Ngao ya Jamii kumenyana na JKT Queens, bali pia ni ujumbe mzito kwa timu zote za WPL msimu mpya wa 2026/27.
Kwa Yanga Princess, matokeo haya yanapaswa kuwa taa ya tahadhari. Bado wana kazi kubwa ya kufanya kwenye safu yao ya kiungo na ulinzi ili kuziba pengo lililopo kati yao na Simba Queens ikiwa wanataka kushindania mataji msimu huu.
WASIKIE HAWA
Kocha wa JKT Queens, Kessy Abdallah, amesema baada ya kufuzu fainali ya Ngao ya Jamii Wanawake, sasa wanaingia kwenye hatua nyingine ya kutetea ubingwa huo walioutwaa msimu uliopita na mechi dhidi ya Mashujaa Queens umewaonyesha msimu huu watakutana na upinzani mkubwa kutokana na kasi na ushindani ulioonekana.
Kocha Mkuu wa Mashujaa Queens, Rajab Ally, amesema kikosi chake kilicheza vizuri licha ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens, baada ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini kushindwa kuzitumia.
"Tulicheza vizuri licha ya kupoteza, baada ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tukashindwa kuzitumia. Wapinzani wetu walitumia nafasi waliyoipata kuondoka na ushindi, huku sisi tukikosa umakini katika hatua ya mwisho ya mashambulizi.
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi', amesema mazoezi maalum aliyompa mshambuliaji wa timu hiyo, Senaf Demise kwa siku nne mfululizo yamesaidia kufunga bao dhidi ya Yanga Princess.
"Utekelezaji huo umenifurahisha na naamini utampa Senaf kujiamini zaidi, huku tukiendelea kujiandaa kwa msimu wa 2026-2027 kwa lengo la kufanya vizuri zaidi baada ya kupoteza taji la Ligi Kuu msimu uliopita."
Kocha Msaidizi wa Yanga Princess, Said Maulid 'SMG', amesema ameridhishwa na kiwango cha timu hiyo licha ya kufanya mabadiliko makubwa katika kikosimechi yao ya kwanza ilikuwa muhimu kwa ajili ya kuwaona wachezaji wapya na uwezo wao.
"Baadhi ya wachezaji walionyesha uwezo binafsi, lakini bado kuna kazi ya kufanya katika kuimarisha uchezaji wa timu kwa pamoja, huku tukiendela kufanyia kazi mabadiliko ya mfumo na mikakati kulingana na hali ya mchezo. Mechi dhidi ya Simba Queens imetupa picha ya maeneo yanayohitaji maboresho kwa ajili ya mechi zijazo za ligi."