Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo manne ya kocha mpya Yanga

MAMBO Pict


KLABU ya Yanga imeendelea kulisuka upya benchi la ufundi kwa kumtambulisha kocha mkuu mpya, Romain Folz pamoja na nyota kadhaa wapya na wale walioongezewa mkataba kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2025-2026.


Folz mwenye umri wa miaka 35 ametua Jangwani kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyetimkia Misri kujiunga na Ismailia, lakini akitajwa kuja na kocha wa makipa, Majdi Mnasria, huku aliyekuwa kocha wa viungo wa klabu hiyo, Youssef Ammar akitajwa kurejeshwa Jangwani.


Yanga imetwaa mataji kwa nyakati tofauti makocha mbalimbali wa kigeni, ikiwemo kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku pia ikitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni baada ya miaka 25 kupita.

Wakati mashabiki wengi wakitamani kuona mwendelezo wa mafanikio hayo, uteuzi wa Folz unakuja na mambo kadhaa. Kwa upande mmoja, ni kocha kijana mwenye elimu ya juu, mwenye falsafa ya soka la kisasa na mwenye uzoefu barani Afrika.

Kwa upande mwingine, ni kocha ambaye rekodi zake zinaonyesha hajawahi kudumu kwenye klabu moja kwa muda mrefu, akihama klabu au taasisi karibu kila baada ya miezi mitatu hadi sita.

Katika uchambuzi huu, tutaangazia mambo matatu. Ikiwemo maisha ya ukocha ya Folz, historia yake, falsafa, uzoefu wa kimataifa, changamoto za muda mfupi alizopitia, na kile ambacho Yanga wanapaswa kujifunza kutokana na rekodi zake kabla ya msimu kuanza.

MAM 01

MIAKA NANE, NAFASI 17

Katika kipindi cha chini ya miaka 8, tayari ameshashika nafasi 17 tofauti kwenye klabu na timu mbalimbali akiwa kocha mkuu, msaidizi, mkurugenzi wa michezo au meneja wa utendaji.

Hii ni idadi kubwa kwa muda mfupi na huibua swali la msingi: kwanini hajawahi kudumu sehemu moja kwa zaidi ya miezi sita?

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, muda wa wastani ambao Folz amedumu kwenye nafasi moja ni miezi 4.5 pekee.

 Kwa lugha rahisi, kila baada ya chini ya nusu mwaka, kocha huyu huwa tayari amehamia klabu au taasisi nyingine.

Mfano halisi ni klabu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini alikoondoka baada ya miezi miwili tu akiwa na mechi 6; ama Ashanti Gold ya Ghana ambako alidumu kwa wiki 6 pekee.

Amefanya kazi barani Afrika kwa sehemu kubwa ya maisha yake ya ukocha Ghana, Afrika Kusini, Botswana, Guinea, Algeria, Misri, Mauritania, na Uganda jambo linalompa uelewa wa mazingira ya soka la Afrika.

Hatahivyo, wachambuzi wa soka la Afrika wanadai kwamba ni kawaida kwa kocha wa umri wa Folz kuhamahama kutokana uhalisia wa klabu alizopita, presha na wakati mwingine yeye mwenyewe kutafuta sehemu yenye changamoto ya kukua na kuonyesha zaidi uwezo wake.

MAM 02

FALSAFA YA 4-3-3

Folz ni mmoja wa makocha wachache Afrika wanaopendelea mfumo wa 4-3-3 yaani mfumo wa maumbo matatu mbele lakini wenye kujilinda kwa nidhamu kubwa.

Katika mfumo huu, anasisitiza nidhamu ya ulinzi kabla ya kushambulia tofauti kabisa na mifumo ya kushambulia isiyojali usalama wa safu ya nyuma.

Katika mfumo wa Folz, viungo wa pembeni hawatakiwi kupoteza nafasi kiholela, mabeki wa pembeni wanapewa majukumu ya msingi ya kujilinda kabla ya kushambulia, na kiungo mkabaji hubeba jukumu la kiungo wa mpito (pivot) ambaye huamua kasi ya mchezo.

Ni mfumo unaojenga timu ngumu kufungika lakini pia unahitaji wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu. Kwenye mazingira ya Yanga ambayo imezoea kushambulia kwa nguvu kupitia mawinga kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na washambuliaji kama Prince Dube, mfumo huu waweza kuibua changamoto ya kimbinu iwapo wachezaji hawatamudu mabadiliko hayo.

“Akiwa Township Rollers, Romain Folz alibadilisha aina ya uchezaji. Walikuwa wakishambulia kutoka katikati. Lakini wakatumia pembeni kushambulia.Pia alibadilisha wachezaji sana,"anasema mchambuzi mmoja wa Botswana.


UZOEFU WA KIMATAIFA

Mbali na klabu, Folz amepewa nafasi katika taasisi kubwa kama FIFA, ambako alikuwa Performance Manager kati ya Novemba 2023 hadi Julai 2024.

Hii ni nafasi ya kiufundi yenye heshima kubwa duniani, na inaashiria kuwa ana uelewa wa kisasa wa data, maendeleo ya wachezaji, tafiti za mazoezi na teknolojia ya michezo.

Amefanya kazi na timu za taifa kama Uganda na Mauritania, akifanya kazi kwa karibu na makocha wenye hadhi kubwa kama Sébastien Desabre na Didier Gomes.

Katika klabu kama Pyramids FC ya Misri na Chamois Niort ya Ufaransa, alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lenye maono mapana ya soka la kisasa. Uzoefu huu unamtofautisha na makocha wengi waliopita Yanga kwa kuwa anakuja na maarifa ya juu ya kiufundi.

MAM 03

YANGA NA FOLZ

Wanatambua uwezo wake, elimu yake na mtazamo wake wa soka la kisasa. Rekodi za mitandaoni zinamhukumu kwamba ni kocha ambaye hajawahi kuongoza klabu moja kwa msimu mzima. Malengo yake ni kujenga timu ya muda mrefu lakini akisaka matokeo ya haraka.

Ni wazi kuwa mazingira ya Yanga yanahitaji uthabiti wa kiutendaji. Mashabiki, wachezaji na viongozi wanapenda kuona mwelekeo unaodumu zaidi ya miezi mitatu au sita.

Hili ndilo jambo ambalo litamfanya Folz ama aandike historia mpya au awe sehemu nyingine ya mzunguko wa maisha yake kwa kukaa na timu kwa muda mfupi.

Kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael ambaye pia amefanya kazi Afrika Kusini kwa muda mrefu, ameona ni kama waajiri wake hao wa zamani wamecheza kamari kwa kocha huyo.

“Yanga ni timu yenye presha kubwa hivyo inanipa mashaka kuamini kuona kuwa anaweza kuendeleza kazi nzuri ambayo imefanya na watanguzi wake, binafsi namtakia kila la kheri lakini nafikiri Yanga ni kama imebeti," anasema.


REKODI ZAKE

Bechem United (Ghana) – Jan,2020 hadi Julai 2020 – mechi 11

Ashanti Gold (Ghana) – Machi 2021 hadi Mei 2021 – mechi 6

Mauritania (Msaidizi) – Juni 2021 hadi Desemba 2021

Township Rollers (Botswana) – Desemba 2021 hadi Juni 2022 – Rekodi za mechi hazijawekwa

Marumo Gallants (RSA) – Julai 2022 hadi Septemba 2022 – mechi 6 

AmaZulu FC (RSA) – Oktoba 2022 hadi Aprili 2023 – mechi 19

Horoya AC (Guinea) – Agosti 2023 hadi Oktoba 2023 – mechi 2

Mamelodi Sundowns (RSA)– Julai 2024 hadi Februari 2025 – kocha msaidizi – 22 mechi chini ya Mngqithi, 8 chini ya Cardoso

Olympique Akbou (Algeria) – Machi hadi Julai 2025 – Mkurugenzi wa michezo

Yanga (Tanzania) – Julai 2025 – ?

Mwandishi wa Makala hii ni mshindi wa tuzo za EJAT katika kipengele cha takwimu za michezo mwaka 2023.