Malawi yaandika rekodi, historia ya kushangaza
Muktasari:
- The Scorchers imeishangaza dunia baada ya kutinga nusu fainali ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo, ikiifunga Ghana mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Al Medina, jijini Rabat.
HISTORIA imeandikwa Wafcon baada ya timu ya taifa ya wanawake ya Malawi kufuzu fainali za Kombe la Dunia la Wanawake zitakazofanyika Brazil 2027, baada ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Wafcon inayoendelea Morocco.
The Scorchers imeishangaza dunia baada ya kutinga nusu fainali ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo, ikiifunga Ghana mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Al Medina, jijini Rabat.
WAMEFIKAJE?
Ikiwa ndo mara ya kwanza inashiriki fainali hizo, wengi hawakutarajia itafanya vizuri kutokana na uwepo wa timu zenye uzoefu katika kundi lao C na ilifanya maajabu kwa kumaliza kileleni.
Katika kundi hilo, Malawi ilimaliza ikiongoza na pointi sita sawa na Nigeria na Zambia zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Misri ikimaliza yua mwishio bila pointi.
Ilianza kwa kuichapa Nigeria ambao ni mabingwa watetezi mabao 3-2, kabla ya kukutana na Misri na kuifunga 3-1 na kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Zambia ikipoteza kwa mabao 2-1.
Katika hatua ya robo fainali, ilikutana na Ghana na kushinda mabao 2-1 na kutinga nusu gainali ambayo imeihakikishia kushiriki fainali za kombe la dunia na katika hatua hiyo, itacheza dhidi ya Algeria.
Katika mechi hiyo ya robo fainali, Ghana ilitangulia kufunga kwa bao la Chantelle Boye-Hlorkah, kabla ya Malawi kusawazisha kupitia kwa nyota wake Temwa Chawinga na Rose Kadzere kufunga bao la ushindi dakika ya 79.
HISTORIA IMEANDIKWA
Malawi imeweka rekodi ya kwanza katika historia ya fainali hizo, ikiwa ni timu ya kwanza tangu michuano hiyo ianzishwe mwaka 1998, kushiriki kwa mara ya kwanza na kufika hatua za juu (nusu fainali) na kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia.
KUPANDA VIWANGO
Kabla ya fainali hizo, Malawi ilikuwa nafasi ya 153 kwa viwango vya soka la wanawake duniani, na mafanikio yao hadi sasa ikifika nusu fainali, ni wazi itapanda kutoka nafasi hiyo.
Mbali na kufuzu nusu fainali na Kombe la Dunia, sababu nyingine ni kuzifunga timu vigogo vya soka Afrika zikiwamo Nigeria na Ghana ambazo zimekuwa zikitamba kwenye soka la wanawake.
ushindi dhidi ya Nigeria na Misri unaonyesha ina uwezo wa kupambana na si kubahatisha, huku ikiacha wengi na maswali kutokana na kutokuipa nafasi ya kufika mbali.
NDUGU WAWILI WAIBEBA
Mafanikio ya Malawi katika fainali hizo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ndugu wawili wanaokipiga katika ligi kubwa duniani na kwa pamoja wameisaidia timu yao kufika hatua hiyo, kutokana na uzoefu walio nao.
Nyota hao, Thabitha Chawinga anayekipiga Olympic Lyon ya Ufaransa, amechangia mabao sita akifunga mawili na kuasisti manne, huku mdogo wake anayekipiga Kansas City ya Ligi Kuu Marekani katika mechi nne alizocheza katika fainali hizo amefunga mabao manne.
SAFARI HAIJAISHA
Dada hao pamoja na nyota wengine wa kikosi hicho, licha ya kufuzu nusu fainali, wana kazi nyingine ya kuhakikisha wanafuzu fainali na kuendelea kuandika rekodi katika michuano hiyo.
Malawi inasaka taji lake la kwanza ikiwa pia ndiyo mara ya kwanza kushiriki fainali hizo ambazo bingwa mtetezi Nigeria imeshaondolewa baada ya kufungwa bao 1-0 na Cameroon.
Nigeria ndiyo timu yenye mataji mengi, ikishiriki mashindano hayo mara 13 na kubeba 10 na kuondolewa kwake kunazipa nafasi timu nyingine ikiwamo Malawi kubeba kwa mara ya kwanza.
MSIKIE CHAWINGA
Akizungumzia rekodi hiyo Thabitha alisema ni moja ya mafanikio makubwa kwenye taifa la Malawi na kizazi kijacho ambacho kitendelea kukumbukwa.
“Ni jambo ambalo halielezeki kwa sababu hatukuwa tunapewa nafasi ya kufanya vizuri lakini Mungu mkubwa tumefanya yale ambayo watu hawakutarajia,” alisema Thabitha na kuongeza;
“Nimpongeze mdogo wangu Temwa kwa kiwango bora alichokionyesha na kwa pamoja kusaidia timu, namwona akiwania tuzo ya mchezaji bora wa dunia ‘Ballon D’or.”