Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makocha Waingereza wanavyochemsha kwenye soka

Muktasari:

  • Walikuwa na mafanikio pia ya kushinda mataji mbalimbali. Mastaa hao baada ya kustaafu soka waliamua kugeukia ukocha lakini mambo yanaonekana kuwa magumu, baadhi wameendelea kukomaa wakizidi kufanya vibaya kila timu wanayoenda, wengine walijaribu na kuamua kuachana kabisa na kazi hiyo.

LONDON, ENGLAND: KUNA orodha kubwa ya wachezaji wa England ambao walitamba sana kuanzia miaka ya 2000 hadi sasa ambao walikuwa na mchango mkubwa katika timu zao hadi kufikia kustaafu kwao.

Walikuwa na mafanikio pia ya kushinda mataji mbalimbali. Mastaa hao baada ya kustaafu soka waliamua kugeukia ukocha lakini mambo yanaonekana kuwa magumu, baadhi wameendelea kukomaa wakizidi kufanya vibaya kila timu wanayoenda, wengine walijaribu na kuamua kuachana kabisa na kazi hiyo. Hawa hapa wachezaji watano waliowahi kung’ara katika kikosi cha timu ya taifa ya England ambao wanapata tabu katika ukocha.


Wayne Rooney

Wayne Rooney alianza maisha yake ya  ukocha katikati ya msimu wa 2020-21, akiwa na Derby County iliyokuwa inaburuza mkia kwenye Ligi Daraja la kwanza.

Alianza vizuri, akiitoa Derby katika eneo la kushuka daraja baada ya kukusanya pointi 31 kati ya 54 katika mechi zake 18 za kwanza.

Hata hivyo, mambo yalibadilika baadaye. Derby ilinusurika kushuka daraja kwa pointi moja kabla ya kunyang’anywa pointi 21 na kushushwa hadi daraja la pili. Hii ikasababisha Rooney ajiuzulu.

Alihamia Marekani kuiongoza DC United aliyoichezea mwishoni, huko pia hakudumu, akarejea England kuchukua mikoba ya kuinoa  Birmingham City kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu.

Kujiunga kwake na timu hiyo kulishangaza watu wengi, hasa baada ya kocha wa awali, John Eustace, kuachishwa kazi wakati timu ikiwa nafasi ya sita.

Baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya 15 na Birmingham kushuka hadi nafasi ya 20, Rooney alitupiwa virago na timu hiyo miezi mitatu tu baada ya kuanza kazi.

Aliamua kupumzika msimu wote kisha Mei mwaka jana akachukua mikoba ya kuifundisha Plymouth ambayo aliachana nayo Desemba 31, 2024 baada ya msururu wa matokeo mabaya.


Gary Neville

Alikuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha  uchezaji wake.  Gary alishinda jumla ya mataji manane ya Ligi Kuu ya England, makombe mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia alicheza mechi 85 kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England.

Hivi karibuni, amekuwa sehemu muhimu ya matangazo ya soka kwenye Sky Sports kupitia televisheni na podikasti.

Hata hivyo, kabla ya kuamua kugeukia media moja kwa moja, Gary alipata nafasi ya ukocha kwa mara ya kwanza kukinoa kikosi cha Valencia, iliyokuwa ikipitia kipindi kigumu.

Gary alipewa nafasi hiyo na mshirika wake wa biashara Peter Lim  Desemba 2015.

Lakini baada ya kushinda mechi kumi tu akipata pia kipigo cha mabao 7-0 kutoka kwa Barcelona katika mechi 28, Neville alifutwa kazi. Tangu wakati huo, hajawahi kurudi kwenye kazi ya ukocha.


Paul Scholes

Baada ya kununua hisa katika klabu ya Salford City mwaka 2014, Scholes alichukua jukumu la kuwa kocha wa timu hiyo kwa muda mfupi mwaka 2015, akiongoza mechi moja pekee na kushinda.

Februari 2019, alipata shavu la ukocha katika kikosi cha Oldham, lakini alijiuzulu baada ya mechi saba tu, akishinda moja pekee.

Mwaka 2020, alirejea tena kama kocha wa muda wa Salford, akishinda mechi mbili kati ya tano alizoongoza.

Tangu wakati huo, Scholes amejikita zaidi kwenye uchambuzi wa soka, hasa kwa TNT Sports.


 Steven Gerrard 

Baada ya kuwa kocha wa timu za vijana za Liverpool, Steven Gerrard alipata nafasi ya kuwa kocha mkuu kwa mara ya kwanza kati ya 2018–2021 alipoajiriwa kuifundisha  Rangers, iliyokuwa ikipitia kipindi kigumu.

Gwiji huyo wa Liverpool aliwasaidia Rangers kuwa washindani tena katika msimu wa kwanza ambapo pia ilifikia hatua ya 16 bora ya Ligi ya Europa msimu wa 2019-20. 

Katika msimu uliofuata, Rangers ilishinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Scotland kwa alama 102, ikifanikiwa kuizuia Celtic, kushinda taji la kumi mfululizo. 

Baada ya hapo alirejea Ligi Kuu England alipopata nafasi ya kuwa kocha wa Aston Villa, Novemba 2021, akichukua nafasi ya Dean Smith.

Hata hivyo, mambo yalikuwa magumu kwani msimu wake wa kwanza aliingoza timu hiyo kumaliza nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi.

Baada ya ushindi wa mechi mbili pekee kati ya mechi 12 za mwanzo za msimu uliofuata wa Ligi Kuu, Gerrard alifutwa kazi.

Baada ya hapo alitimkia zake Saudi Arabia kuifundisha  Al-Ettifaq ambako mambo sio mazuri na msimu huu ameshinda mechi nne tu kati ya 13 za Ligi Kuu.


Frank Lampard 

Kama Rooney, lejendi huyu wa Chelsea alianza kazi yake ya ukocha katika timu ya vijana ya Chelsea kabla ya kupewa shavu la kuifundisha Derby County.

Akiwa katika kikosi hicho kilichokuwa na mastaa kama Mason Mount, Fikayo Tomori na Harry Wilson, waliokuwa kwa mkopo, Lampard aliiwezesha timu hiyo kufika hadi fainali ya mtoano ya kuwania kupanda Ligi Kuu mwaka 2019 na isivyo bahati wakapoteza mbele ya Aston Villa.

Baada ya hapo alirudishwa Chelsea Julai mwaka huo na akaiwezesha kumaliza katika Top 4 licha ya kufungiwa kusajili.

Hata hivyo, msimu uliofuatia mambo yalikuwa magumu licha ya kufanyika kwa usajili mkubwa wa mastaa kama Kai Havertz na Timo Werner, akafutwa kazi baada ya nusu msimu tu.

Baada ya mwaka mmoja kuwa nje ya kazi, Lampard alipewa nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu  England, kuifundisha  Everton, akichukua nafasi ya Rafael Benitez.

Akiwa amejiunga na klabu ikiwa katika nafasi ya 16 na pointi nne juu ya eneo la kushuka daraja, Lampard aliiongoza Everton kujinasua kutoka kwenye hatari.

Lakini baada ya ushindi mmoja tu kutoka kwa mechi 11 msimu uliofuata, alifutwa kazi katika viunga hivyo vya Goodison Park.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Lampard alirudi Chelsea Aprili, 2023 kama kocha wa mpito, akichukua nafasi ya Graham Potter.

Hata hivyo, hali ya Chelsea iliendelea kuwa mbaya na ikamaliza msimu katika nafasi ya chini kwa mara ya kwanza tangu 1996.