Mahenge: Hivi ndivyo tunavyoijenga Volleyball mpya
Muktasari:
- Leo, mjadala wa mpira wa wavu hauishii tena kwenye mashindano ya siku chache, bali umeanza kugusa ligi ndefu, mikataba ya wachezaji, vituo vya vipaji, timu za Taifa, mashindano ya vijana, ushiriki wa wanawake na hata fursa za wachezaji kucheza nje ya nchi.
KWA miaka mingi, mchezo wa mpira wa wavu (Volleyball) Tanzania umekuwa ukichezwa kwa vipaji, mapenzi na juhudi za watu wachache, lakini safari ya kuufanya kuwa taaluma yenye mfumo, ligi, ajira na biashara imeanza kuchukua sura mpya.
Leo, mjadala wa mpira wa wavu hauishii tena kwenye mashindano ya siku chache, bali umeanza kugusa ligi ndefu, mikataba ya wachezaji, vituo vya vipaji, timu za Taifa, mashindano ya vijana, ushiriki wa wanawake na hata fursa za wachezaji kucheza nje ya nchi.
Katika mahojiano maalum ya Mwanaspoti na Mkurugenzi wa Utawala wa Shirikisho la Mpira wa Wavu Tanzania (TVF), Riziki Godwin Mahenge, anaeleza hatua zilizopigwa, changamoto zilizopo na mpango wao wa kuufanya mchezo huo uwe na uwezo wa kujiendesha.
Mahenge amezungumza mambo mengi na Mwanaspoti, lakini hakuacha suala la udhamini, udhaifu wa timu za Taifa, muda wa kambi, vipaji vya shule na mtaani, nafasi ya wanawake, ligi ndefu pamoja na aina ya urithi anaotaka kuacha katika mchezo huo.
MPIRA WA WAVU UMETOKA MBALI
Mahenge anasema tofauti kati ya mchezo wa mpira wa wavu kwa sasa na miaka sita au saba iliyopita ni kubwa, akitaja kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa ligi na kuongezeka kwa mwonekano wa mashindano.
“Mpira wa wavu umepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka sita au saba iliyopita. Kipindi hicho haukuwa na mfumo rasmi wala ligi, lakini sasa tuna ligi rasmi inayochezwa na mfumo umeanza kurasimishwa. Mashindano pia yanaonyeshwa mubashara katika Azam TV na vyombo vingine vya habari.”
WACHEZAJI SASA WANALIPWA
Moja ya mabadiliko anayoyaona Mahenge ni kuanza kwa wachezaji kupata mikataba rasmi na klabu, jambo linalofanya mchezo kuanza kuwa chanzo cha kipato. “Wachezaji wameanza kupata mikataba rasmi na klabu zao na hiyo inawafanya waweze kulipwa mishahara ya kila mwezi. Hii ni hatua muhimu kwa sababu tunataka mchezaji aone volleyball kama kazi na siyo mchezo wa kujitolea tu,” anasema.
MASHINDANO YAMEONGEZA BURUDANI
Kwa upande wa mashabiki anasema mashindano mbalimbali yameongeza nafasi ya watu kuufuatilia mchezo huo, akitaja National League, Nyerere Cup na Taifa Cup.
“Tumejaribu kutengeneza mashindano yenye ushindani na burudani ambayo mashabiki wanaweza kuyafuatilia. National League, Nyerere Cup na Taifa Cup ni sehemu ya kujenga mazingira ambayo mashabiki wanaweza kuutazama mechi hata katika televisheni na simu zao.”
MFUMO WA KLABU NA MIKOA
Anasema maendeleo haya hayahusu wachezaji pekee, bali pia viongozi wa mikoa na klabu ambao wameanza kupata mifumo ya kuwasaidia kuendesha shughuli zao na kutafuta wadhamini.
“Umeweka mifumo inayowasaidia viongozi wa mikoa na klabu kuendesha shughuli zao vizuri na pia kutafuta wadhamini. Tunataka kila upande wa mchezo uwe na mfumo unaoeleweka.”
MIUNDOMBINU MWEMBE YANGA
Katika eneo la miundombinu anataja uwepo wa uwanja wa kisasa uliopo Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam, utasaidia pia maandalizi ya timu za Taifa.
“Tumepata uwanja wa kisasa eneo la Mwembe Yanga, ambao utakuwa na ofisi pamoja na nyumba za kulala wachezaji kwa ajili ya kambi za timu ya Taifa. Hii ni sehemu ya kujenga mazingira bora ya mchezo.”
UKATA BADO NI KIKWAZO
Pamoja na hatua hizo, Mahenge anasema fedha bado ni changamoto kubwa katika kuendesha mchezo wa mpira wa wavu Tanzania.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni ukata na ukosefu wa rasilimali za fedha za uhakika. Ndiyo maana azma yetu ni ‘Make it standable’, yaani kutengeneza vyanzo vya uhakika vya fedha ili mpira wa wavu uweze kujisimamia wenyewe badala ya kutegemea michango ya muda mfupi.”
LIGI NDIO BIDHAA KUU
Ili kuuongezea umaarufu, anasema wanataka kutumia ligi kama bidhaa kuu ya kuufikisha mchezo wa mpira wa wavu kwa Watanzania wengi zaidi.
“Tunataka kutumia Ligi Kuu kama bidhaa yetu kuu ya kuitangaza kupitia televisheni na mitandao ya kijamii. Pia tunataka kuwashirikisha wasanii na watu maarufu kwenye matamasha ya uzinduzi wa ligi ili waweze kuvuta mashabiki wao.”
VIPAJI VINAPOANZIA
Anasema mpango wa kukuza vipaji hauwezi kutenganishwa na shule na maeneo ambayo watoto wanakutana na kucheza mchezo wa mpira wa wavu.
“Tunataka kuhamasisha uchezaji wa mpira wa wavu shuleni, kwenye klabu na mtaani. Tulichotaka kwanza ni kutengeneza soko na masilahi kupitia ligi kuu ili mtoto akigundulika awe na mahali rasmi pa kwenda na kupata ajira.”
VITUO VINAANZA
Kwa mujibu wake anasema jitihada hizo zimeanza kuzaa mfumo wa vituo vya kulea vipaji.
“Kwa sasa tumetambua vituo rasmi tisa na kuna vituo visivyo rasmi zaidi ya 30 vya kulelea watoto. Hii inaonyesha msingi wa kuibua vipaji unaanza kujengwa,” anasema.
TIMU ZA TAIFA BADO ZINA KAZI
Anasema licha ya maendeleo kwenye ligi, kiwango cha timu za Taifa bado kinahitaji kuboreshwa baada ya kutofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Kwa sasa Almas Kings kwa wanaume na Almas Queens kwa wanawake bado hazijawa na uwezo mkubwa wa kushindana kimataifa. Hivi karibuni ziliondolewa katika hatua za awali za kufuzu Kanda ya Tano. Hili tunaliona na tunajua kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya.”
WACHEZAJI WA KIGENI
Katika kujenga ushindani wa ndani, anaona umuhimu wa kuwa na utaratibu unaodhibiti idadi ya wachezaji wa kigeni.
“Tunapaswa kuweka ukomo wa wachezaji wa kigeni ili wale wanaokuja walete ushindani na uzoefu kwa wachezaji wetu wa ndani. Wakati huohuo tunahitaji kuvisukuma vilabu vya ndani kushiriki mashindano ya kimataifa.”
KAMBI HAZITOSHI
Mkurugenzi huyo anasema maandalizi ya timu za Taifa yanakabiliwa na changamoto ya muda mfupi wa kambi, akitaja pia suala la fedha na uthibitisho wa ushiriki.
“Kambi za wiki mbili hadi nne hazitoshi. Tatizo ni kwamba tunakosa fedha za uhakika na wakati mwingine uthibitisho wa ushiriki kutoka Serikali au Baraza la Michezo la Taifa unachelewa. Hilo linaathiri maandalizi.
“Tunapaswa kuwa na kambi za mara kwa mara chini ya kocha mkuu Emmanuel Esayas. Pia tunahitaji ligi ndefu yenye mfumo wa kupanda na kushuka daraja ili wachezaji wawe wanacheza kwa muda mrefu na kupata ushindani wa kutosha.”€
WACHEZAJI WANAPELEKWA NJE
Kwa upande wa wachezaji wanaotafuta uzoefu nje ya Tanzania, anasema TVF imekuwa ikisaidia katika kutafuta fursa hizo.
“Tunasaidia wachezaji kupata fursa za nje. Kwa sasa Omari Bure yupo Jisagara Rwanda, Lamek yupo Burundi, Ramadhani yupo Rwanda na Jackson Mari yupo Ujerumani. Hussein yuko kwenye hatua za kwenda majaribio Hungary na Good Fudi anatarajiwa kwenda Rwanda.”
LIGI INABADILIKA
Mahenge anasema Ligi ya Mpira wa Wavu imeondoka kwenye mfumo wa mashindano mafupi na inaelekea kwenye ligi inayochezwa kwa muda mrefu.
“Tumetoka kwenye mashindano ya siku tano au sita mwaka 2021 na sasa tunaelekea kwenye Ligi Ndefu, yaani ‘Full Swing’, kuanzia mwezi wa 10 au 11 hadi mwezi wa sita kwa kufuata kalenda ya FIVB. Tunatarajia kuwa na timu 10 za wanaume na timu nane za wanawake zikiwa na mfumo wa kupanda na kushuka daraja.”€
UDHAMINI BADO
“Kwa sasa bado hatuna mdhamini mkuu wa muda mrefu wa ligi. Tupo kwe nye hatua ya uwe kezaji na kujitangaza, huku tukipata ushirikiano kutoka Azam TV, Natkin na Vodacom Tanzania. Tunahitaji wadhamini zaidi na wa muda mrefu.”
MEDIA
Kuhusu kwa nini mchezo wa mpira wa wavu haupati nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari kama baadhi ya michezo mingine, anasema suala hilo linahusisha pia nguvu ya kibiashara ya mchezo.
“Vyombo vya habari vinatafuta habari zinazouzika na zenye mashabiki wengi kibiashara. Mpira wa wavu bado tunajenga mashabiki na ushawishi huo ili uwe bidhaa inayoweza kujiendesha kibiashara.”
RATIBA ITAFUATA KALENDA
“Tunataka kutengeneza kanuni rafiki na kufuata kalenda ya FIVB ili ligi na mashindano mengine kama Taifa Cup na Tuzo za TVF yafanyike kwa wakati bila kuvuruga ratiba,” anasema.
VOLLEYBALL SI MCHEZO WA KUJITOLEA TU
“Tunataka kuondoa uendeshaji wa kujitolea tu na kuifanya volleyball kuwa biashara yenye maslahi. Milango ipo kwa vijana kuwa wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi, wataalamu wa takwimu na hata madaktari. Mchezo una nafasi nyingi zaidi ya kucheza tu,” anasema.
WANAWAKE WAPO SAWA
Katika upande wa wanawake, Mahenge anasema TVF imeweka ushirikishwaji wao katika nafasi muhimu za mchezo.
“Wanawake wanashiriki kikamilifu na kwa usawa. Zawadi za washindi ziko sawa na za wanaume, huku nafasi mbalimbali za uongozi kama makamu wa rais, mkurugenzi wa jinsia, makamishna na wajumbe wa bodi zikishikiliwa na wanawake.”
VIJANA U15 NA U19
Mahenge anasema hatua nyingine ni kuongeza mashindano ya vijana ili vipaji viweze kuonekana mapema.
“Tuna mpango wa kuandaa mashindano maalum ya vijana chini ya miaka 15 na chini ya miaka 19. Tunataka watoto waanze kuingia kwenye mfumo wa mashindano mapema na vipaji vyao vifuatiliwe.”
WANAWAKE KUJITEGEMEA
Mbali na mashindano ya vijana, Mahenge anasema kuna mpango wa baadaye wa kuyafanya mashindano ya wanawake yawe na nafasi yake kamili.
“Tunataka kufika mahali ambapo mashindano ya wanawake hayataonekana kama nyongeza ya mashindano ya wanaume. Tunataka yajitegemee na yawe na mfumo wake ambao utawapa wanawake nafasi kubwa zaidi ya kuendelea.”
KIPAJI HAKIPOTEI
Mahenge anasema jukumu la TVF haliishii kwenye kugundua kipaji, bali ni kuhakikisha kinapata mazingira ya kukua.
“Vipaji bora tunavyovigundua tunavitafutia fursa za kwenda kucheza nje ya nchi au tunavielekeza kwenye klabu za taasisi ambazo zina nidhamu nzuri ya mazoezi. Hatutaki kipaji kigundulike halafu kiishie hapo,” anasema.
MALENGO
“Mchezo ukishakuwa wa kibiashara na kutoa kipato cha uhakika, wachezaji wataweza kuwekeza nguvu, kutafuta wakufunzi binafsi na kutumia muda zaidi kugeuza vipaji vyao kuwa taaluma rasmi. Hapo ndipo tutakapokuwa tumefanikiwa,” anasema.
URITHI WAKE
Akiangalia nafasi yake kama Mkurugenzi wa Utawala, anasema kipaumbele chake si kuacha majina bali mfumo ambao utaendelea kufanya kazi hata viongozi wakibadilika.
“Kipaumbele changu kikubwa ni kuweka mfumo rasmi wa uendeshaji wa shirikisho na mchezo wa wavu Tanzania. Sitaki uendeshaji wa holela au ule wa ‘familia ya kambale’. Tunahitaji mfumo unaoongozwa na sheria na kanuni,” anasema.
Anakiri pia kwamba bado kuna eneo linalohitaji nguvu zaidi, hasa katika kutafuta wadhamini wa kutosha na wa muda mrefu.
“Bado tunahitaji kuongeza jitihada katika kupata wadhamini wa kutosha na wa muda mrefu ambao watasaidia kuendesha shirikisho. Hili ni eneo ambalo tunahitaji kufanya zaidi.” anasema.
Kuhusu urithi anaotaka kuuacha, anasema anataka kizazi kijacho kikute mfumo uliojengwa kwa misingi ya sheria na kanuni.
“Ningependa kuacha mfumo rasmi wa uendeshaji unaoongozwa na sheria na kanuni imara zilizotengenezwa chini ya Idara ya Sheria na Nidhamu. Huo ndio urithi ninaotaka kuuacha,” anasema.
WADAU SIKILIZENI
Akijibu wadau wanaosema mchezo wa mpira wa wavu bado haujaendelezwa kwa kiwango kinachostahili, Mahenge anasema wanatambua matarajio hayo huku akisisitiza kwamba hatua zimeanza kuonekana.
“Wadau wengi wanatambua na kupongeza hatua kubwa ambazo zimepigwa, ingawa wapo wachache ambao wanatamani kuona mchezo ukienda mbali zaidi. Sisi tunaliona hilo na tunajua bado kuna kazi ya kufanya,” anasema.
Kama angepewa rasilimali zote anazohitaji leo, Mahenge anasema angeanzia kwenye jambo moja litakaloweza kubadili kila kitu kingine mashabiki.
Jambo la kwanza ningefanya ni kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye uhamasishaji na ujenzi wa mashabiki. Mchezo ukiwa maarufu, ukawa unatazamwa hata kwenye vibanda, milango yote ya udhamini, fedha na Serikali itafunguka yenyewe.