Hii ndo Arena Rwanda anayoiwaza Diamond Platnumz
Muktasari:
- Kauli ya Diamond miezi mitatu iliyopita ilizua mjadala mkubwa nchini. Wapo waliomuunga mkono wakisema Tanzania imechelewa kuwa na Arena ya kisasa licha ya kuwa na soko kubwa la muziki, michezo na idadi kubwa ya watu.
WAKATI mjadala wa ujenzi wa Arena ulipoibuka kutokana na kauli ya supastaa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, alipoeleza umuhimu wa kuwa na ukumbi wa kisasa wa matamasha na michezo, majirani Rwanda walikuwa wanatuchora tu, kwani tayari walishavuka hatua hiyo kwa kujenga BK Arena, mradi uliobadili sura ya burudani, michezo na utalii wa nchi hiyo.
Kauli ya Diamond miezi mitatu iliyopita ilizua mjadala mkubwa nchini. Wapo waliomuunga mkono wakisema Tanzania imechelewa kuwa na Arena ya kisasa licha ya kuwa na soko kubwa la muziki, michezo na idadi kubwa ya watu.
Serikali nayo ilieleza ipo katika mipango ya kujenga ukumbi wa aina hiyo.
Lakini ukifika Kigali, hutahitaji maelezo mengi kuelewa kwa nini Rwanda imekuwa kitovu cha matukio makubwa Afrika Mashariki. BK Arena imekuwa moja ya alama za maendeleo ya nchi hiyo.
MRADI WA MABILIONI
BK Arena ambayo awali ilijulikana kama Kigali Arena, ilifunguliwa Agosti 2019 ikiwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 10,000.
Ukumbi huo ulijengwa kwa gharama zinazokadiriwa kufikia Dola 104 milioni (Sh270 Bilioni) na ulijengwa na kampuni ya SUMMA kutoka Uturuki ndani ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja.
Kwa mtazamo wa kawaida unaweza kuona ni ukumbi wa mpira wa kikapu lakini kwa Rwanda ni zaidi ya hapo. Ni jukwaa la biashara, utalii, muziki, michezo na mikutano ya kimataifa.
KUBWA KULIKO
Ndani ya BK Arena zimefanyika fainali za Basketball Africa League (BAL), mashindano ya Afrobasket, mechi za kufuzu Kombe la Dunia la FIBA, matamasha ya wasanii wakubwa wa Afrika na dunia pamoja na mikutano ya kimataifa.
Ukumbi huo pia hutumika kwa maonyesho ya biashara, kongamano, hafla za kitaifa na shughuli nyingine zinazovutia maelfu ya wageni kila mwaka.
Kwa lugha nyingine, Rwanda haikujenga ukumbi kwa ajili ya mchezo mmoja bali ili kujenga uchumi unaotokana na matukio.
MSIKIE MTAALAMU
Mkurugenzi Mtendaji wa QA Venue Solutions Rwanda, Guy Hedderwick, kampuni inayosimamia BK Arena, anasema lengo lao ni kuhakikisha ukumbi huo unafanya kazi kwa viwango vya kimataifa, pia unatumika mara kwa mara.
“Dhamira yetu ni kuendesha ukumbi kwa viwango vya kimataifa, pia kuhakikisha unatumika. Tuko tayari kufanya mazungumzo na waandaaji wa matukio ili kupata suluhisho linalomnufaisha kila mmoja,” anasema Hedderwick.
Kwa mujibu wake, ukumbi usiotumika ni hasara kwa sababu siku iliyopotea haiwezi kurudi tena.
“Kama hakuna tukio leo, huwezi kuuza siku hiyo kesho. Ni bora kupata namna ya kuhakikisha tukio linafanyika kuliko kuacha ukumbi ukiwa tupu.” Kauli hiyo inaonyesha namna Rwanda ilivyobadili fikra kutoka kujenga miundombinu hadi kuhakikisha inazalisha mapato.
ARENA KWA BIASHARA
Kwa mujibu wa QA Venue Solutions, BK Arena sasa huandaa takribani matukio 180 kwa mwaka na lengo ni kufikia zaidi ya matukio 225 kila mwaka. Hiyo ina maana karibu kila baada ya siku mbili kuna shughuli kubwa ndani ya ukumbi huo.
Matukio hayo yanazalisha fedha kwa sekta nyingi; hoteli hujaa wageni, kampuni za usafiri hupata wateja, migahawa huuza zaidi, wafanyabiashara wadogo huongeza mapato na serikali hukusanya kodi.
RWANDA ILIVYOWEKA MKAKATI
Kwa miaka kadhaa sasa, Rwanda imekuwa ikiwekeza katika kile kinachoitwa ‘sports and entertainment tourism’ yaani michezo na burudani kiutalii.
Kupitia Rwanda Convention Bureau, nchi hiyo imejipanga kuvutia mikutano, mashindano ya michezo na matamasha makubwa ya kimataifa kwa kutumia miundombinu ya kisasa kama BK Arena, Kigali Convention Centre na Uwanja wa Amahoro.
Ripoti ya Rwanda Convention Bureau inaonyesha mwaka 2023 pekee sekta ya mikutano na matukio iliingizia nchi zaidi ya Dola 95 milioni huku zaidi ya matukio 160 yakifanyika na kuhusisha zaidi ya washiriki 65,000 kutoka mataifa mbalimbali.
DIAMOND ALIKUWA ANAONA NINI?
Kauli ya Diamond Platnumz haikuhusu muziki pekee kwa mtazamo wa kiuchumi, Arena ni sehemu ambayo inaweza kuunganisha muziki, michezo, biashara, maonyesho, filamu na utalii katika eneo moja.
Leo hii wasanii wengi wakubwa wa Afrika wanachagua Kigali kwa sababu wanajua kuna ukumbi wenye viwango vya kimataifa, teknolojia ya kisasa, usalama na uwezo wa kupokea maelfu ya mashabiki bila changamoto.
KUHUSU TANZANIA
Iwapo Tanzania itakamilisha ujenzi wa Arena ya kisasa, manufaa yake yanaweza kuwa makubwa zaidi kutokana na ukubwa wa soko lake.
Kwanza, wasanii wa Bongo Fleva watapata ukumbi wa kudumu wa kufanya matamasha makubwa bila kutegemea viwanja vya wazi vinavyoathiriwa na mvua na changamoto za kiufundi.
Pili, mpira wa kikapu utaweza kuvutia mashindano ya BAL, FIBA na matukio mengine ya kimataifa ambayo kwa sasa huenda katika nchi zenye miundombinu bora.
Tatu, mchezo wa ngumi utaweza kuandaa mapambano ya kiwango cha dunia, jambo litakalovutia watalii na kuongeza mapato.
Nne, Arena inaweza kutumika kwa volleyball, netball, e-sports, maonesho ya biashara, mikutano ya kimataifa na hafla za kitaifa.
Tano, sekta ya utalii itanufaika kwa sababu kila tukio kubwa huvutia wageni wanaolala hotelini, kutumia usafiri, kula kwenye migahawa na kufanya manunuzi.
SOMO KUTOKA KIGALI
Rwanda imeonyesha Arena siyo matumizi mabaya ya fedha za Serikali wala mradi wa kujionyesha. Ni uwekezaji wa muda mrefu unaozalisha ajira, kodi, utalii na kuitangaza nchi kimataifa.
Ndiyo maana leo BK Arena imekuwa moja ya alama zinazotambulisha Kigali, kama ilivyo O2 Arena jijini London au Accor Arena ya Paris.
Kwa Tanzania, ikiwa ndoto ya Arena itatekelezwa, haitakuwa ushindi wa Diamond Platnumz pekee wala wa wanamichezo pekee.
Itakuwa uwekezaji utakaofungua milango ya matukio makubwa ya kimataifa, kuongeza mapato ya sekta ya utalii na kuiweka nchi kwenye ramani ya burudani na michezo duniani.
Kwa kifupi, Rwanda ilitangulia kuona fursa. Tanzania bado ina nafasi ya kujifunza na kuigeuza ndoto hiyo kuwa mradi utakaobadilisha uchumi wa michezo na burudani kwa vizazi vijavyo.