Magori: Simulizi yangu na Zacharia Hans Poppe

MZEE Zacharia Hans Poppe, Mwamba, Mzee wa supu ya mawe kama alivyokuwa akiitwa na Mashabiki wa Simba, ametangulia mbele ya haki na kuacha mshtuko mkubwa.

Nimepata bahati ya kuwa karibu sana na Mzee Poppe kwa sababu ya shughuli zetu za Simba.

Nimesafiri naye sehemu mbalimbali, hivyo kupata wasaa mzuri wa kujua “sinema” halisi za maisha yake.
Ukikutana na Wanajeshi wenzake, wanakuambia akiwa na umri mdogo wa miaka 19 alitunukiwa cheo cha Luteni usu.

Rekodi iliyodumu kwa miaka mingi na sina hakika kama imevunjwa mpaka sasa.
Huyo ndiye Kapteni Mstaafu na Mtalaam wa Mizinga aliyepigana vita ya Kagera. Shujaa tuliyempoteza.

Mzee Poppe katika kitu ambacho ameondoka nacho na Tanzania imekosa simulizi ya jinsi walivyopanga Mapinduzi ya kumwondoa madarakani Baba wa Taifa Mwl Nyerere.

Mara nyingi nilimsihi sana aandike kitabu chenye kuelezea uhalisia wa yale Mapinduzi, lakini mara zote alijibu bado kuna wahusika wako hai na hawapendi waandikwe kwenye hicho kitabu.

Akaniahidi ikitokea wakakubali au wakafariki dunia kabla yake basi hicho kitabu angekiandika.

Hadithi ya mipango ya Mapinduzi yao ni hadithi tamu mno kuisikiliza hasa kwa watu waliokuwa hai wakati wa utawala wa Mwl Nyerere.

Ni hadithi inayoonyesha ujasiri wa Mzee Poppe, kijana mdogo wa miaka 28, Kapteni wa jeshi alithubutu vipi kushiriki Mapinduzi ya kumwondoa Mwalimu Nyerere, Rais aliyeheshimika sana enzi hizo na kuogopeka?

Kama ambavyo Mzee wetu Poppe hakupenda kuandika kitabu kuhusu Mapinduzi yale na Mimi hadithi hii siwezi kuiandika zaidi ya hapa.

Pengine waliobaki wanaweza siku moja kuwaeleza Watanzania hadithi yenye mafundisho mengi. Kila tukio hapa duniani halikosi mafundisho.

Mzee Poppe anaachiwa jela kwa msamaha wa Rais Mwinyi na kwenda uraiani akiwa na nguo zake tu baada ya kukaa jela kwa miaka 13.

Tofauti na wenzake wengi, Mzee Poppe alitoka jela akiwa na afya njema kimwili na kiakili. Na sababu kubwa ni kuwa wakati wenzake wakisononeka kwa mawazo juu ya kile walichokifanya, yeye alikuwa anawaambia, “uchungu huu wa kufungwa unalingana kabisa na utamu ambao tungeupata kama tungefanikiwa kufanya Mapinduzi.”

Hivyo, yeye aliona ni halali kwake kufungwa na kiakili akawa vizuri. Wazungu wanasema “No regrets”.

Watu wengi wanajiuliza hivi Mzee Poppe aliwezaje kutoka jela 1995 na mara baada ya muda mfupi akawa mfanyabiashara mkubwa?

Mzee wetu hasiti kukupa hadithi hii ya kusisimua alipataje mali zake.

Alianza na Gari moja alilosaidiwa na ndugu zake huku akiendesha mwenyewe. Hakutafuta Dereva, bali aliajiri “Turn Boy” tu. Baada ya kama mwaka akaweza kupata faida ya kupata gari lingine ndipo akaajiri dereva huku yeye bado akiendelea kuendesha.

Aliendelea kuendesha hilo gari karibu miaka mitano ndipo alipoacha baada ya kuanza kuwa na magari mengi hivyo kuhitaji usimamizi.

Ndani ya safari zake huko Congo, Zambia, Rwanda na Burundi kumejaa hadithi nyingi sana za kusisimua na mikasa mingi sana.

Kama kuna wale “Motivational Speakers” wanaoalikwa kutoa semina za walivyoanza maisha yao hadi kufikia kwenye kilele, basi Mzee Poppe ukimsikiliza safari ya maisha yake tangu alivyotoka jela mpaka kuwa Mfanyabiashara mkubwa hutokata tamaa katika maisha yako.

Mzee Poppe kwa wale msiojua alikuwa Mwanamuziki mahiri akipiga gitaa kwenye bendi maarufu sana, Safari Trippers.

Ana simulizi nzuri sana za ujana wake jinsi alivyokuwa akitumia usafiri wa Pikipiki tu. Akiwa kijana barubaru atakusimulia visa na mikasa mingi sana wakati wa ujana wake. Hivi ninavyoandika natabasamu sana.

Kwenye Simba yake sijui niseme nini! Kama Kuna kitu Simba itakosa kwa huyu Mwamba ni uthubutu, ukweli, uaminifu na kujitolea kwa Klabu yake ya Simba.

Nimefanya naye kazi kwenye Bodi ya Simba, Kamati ya Usajili ya Simba, na kwenye Friends of Simba.

Kuanzia mwaka 2004 mpaka wakati mabadiliko ya Simba yanaanza basi huyu Mzee Poppe ndiye alikuwa Tajiri wa Simba. Klabu ilitoa pesa zake, Friends of Simba tulichanga pesa lakini mwisho Mzee Poppe alimalizia nakisi yote ya bajeti.

Wakati wa usajili, alisikika akisema huyo anawasumbua nipeni namba yake. Basi hayapiti masaa matatu anasema leteni mkataba hapa tayari nimeishamalizana nae.

Mzee Poppe alikuwa “mafia” kwenye usajili. Kwa sababu sikupata ruhusa kuelezea baadhi ya simulizi matata sana kwenye usajili nami sitaweza kuziweka hapa.

Lakini atanisamehe niwaeleze hadithi moja ya mwisho kufanya nae usajili kwa “umafia” hivi karibuni.

Tuliondoka usiku Dar kwenda mkoa mmoja wa jirani, yeye akiendesha gari lake la Nissan na Mimi pembeni yake na mtu mmoja wa kufanya hiyo kazi akiwa amekaa kiti cha nyuma. (Hiyo Nissan ilikuwa mpya hivyo haijulikani. Gari nyingine zake zinajulikana hivyo ingekuwa rahisi kubaini kuwa Poppe yupo mji huu.)

Tulifika hapo hotelini saa 6 usiku. Sisi hatukushuka kwenye gari, mhusika akashuka akaulizia kama chumba kipo ndipo aliporudi kuchukua begi lake. Sisi tuliondoka tukaenda kupanga Apatimenti sio hoteli, maana kwa hoteli tungejulikana kirahisi kuwa tupo hapo mjini.

Hiyo ingeleta sintofahamu kwenye kukamilisha zoezi letu.

Huyo mtu wetu aliifanya hiyo kazi alfajiri saa 11 chumbani kwake na kuondoka kuja kwetu Apatimenti akiwa na Mikataba tayari.

Mzee Poppe baada ya kupata ile mikataba akasema sasa naenda kunywa chai pale ili wanione vizuri. Nilimkanya lakini akakataa na kweli akaenda kunywa chai.

Walivyomuona walishangaa sana, wakajiuliza huyu Mzee kaja huku saa ngapi na anafanya nini hapa hotelini?

Huyo ndiyo Mzee Poppe, Mzee wa supu ya mawe. Tutamkumbuka daima. Mzee Jasiri asiyetishwa na lolote. Mzee aliyependa haki sana.
Mzee Poppe amesaidia watu wengi sana. Mzee alikuwa na roho nzuri sana. Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele.



Zacharia, kweli umelala, Mwamba umetulia!
Mara ya mwisho tuliongea kwenye simu kwa shida sana.

Lakini siku nne kabla ya mauti yako nilikuja hapo Aga Khan ICU niweze kukuona, hata hivyo ilishindikana tukaongea kwa video call nikiwa nje ya ICU.

Katika maumivu makubwa lakini ulinionyesha matumaini na mara zote ulimalizia kwa kusema timu yetu inaendeleaje?

Umetuachia pengo kubwa sana, umetuacha upweke, kila jumapili ulitualika nyumbani kwako Ununio kwa nyama choma na mvinyo; mapenzi ya namna gani uliyokua nayo kwa watu wako!


Zachariaaaa…..
kama nilivyozoea kukuita, nawe uliitikia Muraaah… unasemaje..
Vita umevipiga vilivyo vizuri, mwendo umeumaliza na imani umeilinda.
Pumzika kwa amani, Kaka yangu, Ndugu yangu na Mwana Simba mwenzangu.
Tutaonana Mungu akipenda.


Mwandishi wa Tanzia hii ni mwanachama mwandamizi wa klabu ya Simba, Crescentius Magori