Lyon pungufu yakwea kileleni, Mbappe akiibeba Real Madrid
Muktasari:
- Timu tano zina pointi 14 kila moja kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, huku Lyon ikiwa mbele ya PSG, Paris FC, Lille na Monaco kwa tofauti ya mabao. Ushindi wa Lyon haukuwa rahisi ikicheza mbele ya Paul Seixas, nyota wa eneo hilo ambaye ni dereva chipukizi mahiri wa Ufaransa katika mchezo wa baiskeli. Hali ilikuwa ngumu zaidi baada ya staa wa Lyon, Keito Nakamura kutolewa kwa kadi nyekundu dakika 20 kabla ya mchezo kumalizika.
PARIS, UFARANSA: LYON ikiwa na wachezaji 10 ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nice baada ya kuanza kwa kuruhusu bao, na kupanda kileleni mwa Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) juzi Jumapili, huku Monaco iliyokuwa inaongoza ligi hiyo ikipoteza kwa mara ya kwanza msimu huu.
Timu tano zina pointi 14 kila moja kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, huku Lyon ikiwa mbele ya PSG, Paris FC, Lille na Monaco kwa tofauti ya mabao. Ushindi wa Lyon haukuwa rahisi ikicheza mbele ya Paul Seixas, nyota wa eneo hilo ambaye ni dereva chipukizi mahiri wa Ufaransa katika mchezo wa baiskeli. Hali ilikuwa ngumu zaidi baada ya staa wa Lyon, Keito Nakamura kutolewa kwa kadi nyekundu dakika 20 kabla ya mchezo kumalizika.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Elye Wahi, aliyeifungia Nice bao la kwanza dakika ya 18 ambalo lilikuwa bao lake la pili msimu huu, alinyimwa nafasi ya kusawazisha katika muda wa nyongeza baada ya mwamuzi kuamua kuwa alikuwa ameotea kwa tofauti ndogo.
Mabao mawili ndani ya dakika tatu yaliibadilisha mechi kabla ya mapumziko. Pavel Sulc alisawazisha kwa kuupachika wavuni mpira uliorudi baada ya shuti la awali, kabla ya Tanner Tessmann kuipatia Lyon bao la pili kwa kichwa.
Naye kiungo mkongwe wa Ubelgiji, Axel Witsel, alipiga mpira wa kichwa uliogonga mwamba wa juu wa lango mapema kipindi cha pili. Wahi naye aligongesha mwamba kwa kichwa akiwa karibu na lango, muda mfupi baada ya Nakamura kutolewa kwa kadi nyekundu kutokana na kuinua mguu juu na kumchezea vibaya mpinzani.
Katika mchezo mwingine penalti iliyofungwa kipindi cha pili na Noah Cadiou wa Lorient iliizuia Monaco kurejea kileleni mwa Ligue 1, baada ya timu hiyo kupoteza kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Brittany. Kipa wa kimataifa wa Finland, Lukas Hradecky, alijitupa upande sahihi, lakini Cadiou alipiga penalti na kuuweka mpira pembeni mwa lango, na hivyo kuipa Monaco kipigo chake cha kwanza cha ligi msimu huu.
Monaco ni mojawapo ya timu tano zinazolingana pointi kileleni mwa msimamo. Paris FC nayo iliungana na timu hizo baada ya kuichapa Rennes mabao 4-3, kutokana na penalti iliyofungwa na Lassine Sinayoko katika muda wa nyongeza. Rennes ilishuka hadi nafasi ya tano, ikiwa pointi moja nyuma ya vinara hao, licha ya mshambuliaji wake Esteban Lepaul kufunga penalti tatu katika mchezo huo uliofanyika Paris.
Marseille ilipata ushindi muhimu ili kujitenga na eneo la kushuka daraja, baada ya kuichapa Angers mabao 5-2. Le Havre bado iko mkiani mwa msimamo baada ya kufungwa mabao 3-1 na Auxerre, ambayo ilipata mabao mawili kutoka kwa mshambuliaji wa Cameroon, Danny Namaso.
MADRID YAICHAPA SEVILLA
Kylian Mbappe alifunga mabao mawili na kuisaidia Real Madrid kupunguza pengo la pointi dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Hispania (La Liga), Barcelona, hadi sita, baada ya kuichapa Sevilla mabao 4-1 nyumbani. Ushindi huo umekuja wiki moja kabla ya miamba hiyo kukutana katika El Clasico.
Arda Guler alianza kuifungia Real Madrid dakika ya 30, akipiga shuti kali kutoka nje ya eneo la penalti na kuuweka mpira kona ya juu ya lango, kisha Mbappe aliongeza bao la pili dakika saba baadaye baada ya kugeuka kwa ustadi mkubwa.
Baada ya hapo Mbappe alisababisha penalti na kuifunga mwenyewe dakika ya 63. Nayo Sevilla ilipata bao la kufutia machozi dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika kupitia kwa mchezaji wa akiba Manu Bueno. Hata hivyo, Yan Diomande aliiongezea Real Madrid bao dakika mbili baadaye kwa shuti kali.
Na katika mechi nyingine La Liga, Osasuna iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Racing Santander kutokana na penalti ya mapema ya Ante Budimir na bao la mwisho la Asier Osambela, huku kwingineko Celta Vigo nayo ikiifunga Alaves mabao 2-1 nyumbani.
LEVERKUSEN YACHOMOZA
Ibrahim Maza na Patrik Schick walishirikiana kufunga mabao mawili yaliyoisaidia Bayer Leverkusen kutoka nyuma na kuifunga Freiburg iliyokuwa katika kiwango kizuri kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga).
Baada ya kupoteza kwa kushtua dhidi ya Elversberg, timu iliyopanda daraja, katika mechi ya ufunguzi wa msimu, Leverkusen sasa imekusanya pointi 13 kati ya 18 zilizokuwa kwenye nafasi ya kupatikana ikiwa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi sawa na Freiburg iliyo nafasi ya tatu. Freiburg itakuwa mwenyeji wa Bayern Munich wikiendi ijayo.
Nayo Borussia Monchengladbach inayoshika mkia wa msimamo bado inasaka pointi yake ya kwanza msimu huu baada ya kufungwa mabao 2-1 nyumbani na Hoffenheim, ambayo pia inahangaika kupata matokeo mazuri.
Bambase Conte wa Hoffenheim alifungua ukurasa wa mabao kwa kufunga bao lake la pili katika mechi mbili tangu aitwe kwa kushtukiza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani mwezi Oktoba.
Wael Mohya aliisawazishia Monchengladbach muda mfupi baada ya mapumziko, lakini Alexander Prass aliirejeshea Hoffenheim uongozi muda mfupi baadaye. Wageni hao, ambao watakuwa wenyeji wa Lyon katika Europa League, Alhamisi, walipata ushindi wao wa pili msimu huu.
LAZIO YAIFUMUA JUVENTUS
Wachezaji wawili wa Denmark waliipa Lazio ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Juventus mjini Turin, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kulingana pointi na Inter kileleni mwa Ligi Kuu Italia (Serie A). Oliver Provstgaard alifunga dakika ya 37 akitumia urefu wake kuuelekeza wavuni mpira kwa kichwa ikiwa ni krosi ya Mattia Zaccagni, baada ya Lazio kutengeneza shambulizi kupitia kona fupi upande wa kushoto.
Mdenmark mwenzake, Gustav Isaksen, aliongeza bao la pili dakika ya 66 akipokea pasi kutoka kwa Nuno Tavares upande wa kulia, akauhamishia mpira kwenye mguu wake wa kushoto na kupiga shuti la chini lililoingia kona ya mbali ya lango. Fisayo Dele-Bashiru alikamilisha ushindi huo dakika ya 89 akianzisha shambulizi la kushtukiza akiwa ndani ya nusu ya eneo lao, akapenya hadi eneo la hatari kabla ya kupiga shuti la chini na kufunga. Mashabiki wa Juventus waliokuwa wamekasirika waliendelea kuizomea timu yao hadi kipenga cha mwisho.
COMO YAIKOMOA FIORENTINA
Nayo Como ya kocha Cesc Fabregas ilimaliza mfululizo wa mechi tatu bila ushindi katika Serie A, baada ya kuifunga Fiorentina mabao 3-1 ugenini. Mattia Liberali na Nico Paz waliifungia mabao kipindi cha kwanza na kuitanguliza mbele, huku Marin Pongracic wa Fiorentina akipunguza tofauti ya mabao muda mfupi kabla ya mapumziko.
Anastasios Douvikas wa Como alifunga bao la tatu mapema kipindi cha pili, na hivyo kuzima matumaini ya Fiorentina ya kurejea mchezoni. Fiorentina iliendelea kubaki katika eneo la kushuka daraja ikiwa na pointi nne.
Na katika mchezo mwingine wa ligi hiyo AC Milan ilipanda juu ya Como hadi nafasi ya nne baada ya kunusurika na juhudi za Atalanta za kurejea mchezoni na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Mabao ya Goncalo Ramos, Adrien Rabiot na Mario Gila yaliifanya Milan kuongoza kwa mabao 3-0 baada ya dakika 58. Hata hivyo, Atalanta ilipambana na kufunga kupitia kwa Gianluca Gaetano na Nikola Krstovic. Katika mechi iliyochezwa mapema, Lecce iliichapa Udinese mabao 3-0. Kialonda Gaspar, Konan N’Dri na Jamil Siebert wote walifunga katika ushindi huo.