Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Le Blues wanavyotua kambini wakishindana nje ya uwanja

FRANCE Pict

Muktasari:

  • Kwa Afrika, kuanzia Alhamisi kutakuwa na mechi za kirafiki kati ya nchi na nchi, huku kukiwa pia na michuano ya kuwania kufuzu fainali za Mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 zinazotarajiwa kufanyika kwa pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwakani, na tayari nyota wa wameshaitwa kujiandaa na kipute hicho.

PARIS, UFARANSA: TIMU ya taifa ya Ufaransa chini kocha mpya Zinedine Zidane imeshaanza kukusanyika kambini tayari kwa ajili ya mashindano ya Ligi ya Uefa (Uefa Nations League) inayopigwa katika kipindi hiki cha mapumziko ya kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), ambapo nchi mbalimbali zimeita vikosi kucheza mechi na mataifa mengine.

Kwa Afrika, kuanzia Alhamisi kutakuwa na mechi za kirafiki kati ya nchi na nchi, huku kukiwa pia na michuano ya kuwania kufuzu fainali za Mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 zinazotarajiwa kufanyika kwa pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwakani, na tayari nyota wa wameshaitwa kujiandaa na kipute hicho.

Hata hivyo, kinachovutia wakati wakijiunga na vikosi vya timu zao huwa ni namna wanavyoshindana kuwasili kambini wakiwa katika mapigo tofauti, huku wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa (Les Blues) wakiongoza kwa kupiga pamba na na viatu vinavyokwenda na fasheni ya kisasa.

Kwa mashabiki wa soka wanaifahamu vyema kipindi kinachopatikana katika kila kalenda ya soka kinachojulikana kama ‘international break’ au mapumziko ya mechi za kimataifa.

Mastaa wa soka huchukua mapumziko mafupi kutoka katika shughuli zinazohusisha klabu ili kushiriki na kuziwakilisha timu zao za taifa katika majukumu ya soka la kimataifa.

Lakini bila kutarajiwa, kipindi hiki kimebadilika kwa haraka kutoka kuwa muda wa shughuli za soka na kuwa kama jukwaa la mitindo kwa baadhi ya wanasoka kwenye mitindo zaidi duniani.

Mitindo ya mavazi na soka ghafla ilianza kwenda pamoja, ikionyesha mabadiliko katika mwenendo wa jamii. Hali hiyo ilianza kuwafurahisha na kuwavutia mashabiki duniani ambao hufuatilia kwa karibu namna wachezaji wanaowapenda wanavyoendelea kuvutia mipaka ya mitindo.

Katika ulimwengu wa sasa wa burudani, ambapo mitindo ya mavazi inakutana na soka, wachezaji walianza kuja na mitindo yao bora ya mavazi nje ya uwanja kila waliposafiri kwenda kuziwakilisha nchi zao.

Katika mtindo huu mpya, kila michezo ya klabu inapositishwa kutokana na mapumziko mengine ya mechi za kimataifa na wachezaji  tunaowapenda wanapowasili wakiwa wamevalia mavazi yao maridadi zaidi, inakuwa vigumu kutomfikiria Zidane na kikosi chake cha timu ya taifa ya Ufaransa unapozungumzia kipindi cha baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

Wanaojulikana kwa jina la Les Bleus, timu ya taifa ya wanaume ya Ufaransa hurudi katika kambi yao ya timu ya taifa, kama ilivyo kwa nchi nyingine, kujiandaa kwa ajili ya majukumu ya kitaifa.

Lakini jambo lingine ambalo limekuwa muhimu zaidi siku hizi ni mwonekano wao wanapowasili, hasa mtindo wa mavazi ambao kila mchezaji huja nao anapowasili katika kambi ya Clairefontaine.

Ni kweli kwamba Wiki ya Mitindo ya Paris maarufu kama Paris Fashion Week inaweza kuwa ilishapita. Hata hivyo, jukwaa la mitindo liko hai kila timu ya taifa ya Ufaransa inapofanya matembezi yake maarufu kutoka kwenye teksi za mastaa hadi kwenye ngazi za kituo cha timu hiyo ya taifa.

Kila mara mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Dunia wanapowasili, mastaa huonyesha mavazi mapya na kuigeuza kambi yao iliyopo Clairefontaine kuwa eneo la mitindo ya mavazi makali ya mitaani.

Kuwasili kwa timu ya Ufaransa kwa ajili ya majukumu ya timu ya taifa kumekuwa kama utamaduni. Matembezi ya kwenda Clairefontaine huwa yamejaa mavazi ya chapa maarufu, viatu vya michezo vilivyotengenezwa kwa matoleo machache na mavazi yaliyobuniwa kwa ajili ya mtu binafsi. Kuanzia umaridadi wa kawaida wa Kylian Mbappe, Jules Kounde, Marcus Thuram na Ibrahima Konate hadi mtindo wa kifahari wa Michael Olise, Bradley Barcola na Mike Maignan. Je, kuna kikosi cha timu ya taifa ambacho kina mtindo zaidi nje ya uwanja zaidi yao?

 Kumbuka kwamba kocha Zidane kawapiga biti mastaa kutovaa mavazi ya ajabu wanapokwenda katika kambi ya timu ya taifa. Twende nao!


FRA 06

KYLIAN MBAPPE

Anajulikana kwa kasi yake kubwa na umaliziaji bora uwanjwani, lakini Mbappe pia anapenda mitindo ya mavazi ya kiwango cha juu. Mara nyingi huonekana akiwa amevalia mitindo maridadi, akichanganya chapa za wabunifu wakubwa na mavazi ya kawaida.

Mtindo wake akiwa nje ya majukumu ni wa kawaida, lakini wenye mvuto huku umakini wake katika kila kitu ukiwa wa kiwango cha juu.

Mbappe daima huonekana nadhifu kama alivyofanya alipokuwa akijiunga na kikosi cha Ufaransa kwa ajili ya usajili kabla ya mechi zao za kufuzu EURO 2027, akiwa amevalia Nike LeBron 17 ‘Future Air’ ya mtindo wa michezo.


FRA 05

JULES KOUNDE

Katika safari zake za hivi karibuni, Jules Kounde amekuwa akiwasili katika kambi ya Ufaransa akiwa amevalia mavazi ya kuvutia na maridadi.

Kama kawaida, beki huyo amekuwa akionyesha mfululizo wa mitindo ya kipekee, na mwamba huyo wa Barcelona anajulikana kwa mitindo mikali na ya kipekee. Alijitokeza katika majukumu ya timu ya taifa mapema mwaka huu akiwa amevalia alivyopenda, akionekana na viatu vya Timberland, fulana ya kubana isiyo na mikono na sketi, mapigo aliyoyarudia majuzi.

Pia, aliwahi kuvutia akiwa amevalia mavazi ya ajabu na jozi ya buti nyeusi maridadi na kuna wakati akiwa na viatu virefu.

Hata hivyo, Kounde anafurahia kuvaa kwa namna ya kipekee, jambo linalovutia macho na kuwafanya watu kujiuliza kulikoni mtu mpole awe alivyo?

Ni rahisi kudhani kwamba mchezaji huyo ataendelea kuvuka mipaka ya mitindo ya mavazi ya wanaume, kwani huwa hakosi linapokuja suala la mtindo, huku akiwa na mwelekeo bora kwa wachezaji wenzake wa Ufaransa.


FRA 04

IBRAHIMA KONATE

‘Ibou’  kama anavyojulikana kwa jina la utani, mara nyingi huonyesha namna ya kutengeneza mwonekano wa pekee akivutia vyombo vya habari kila mahali na kuwashangaza wachezaji wenzake pamoja na mashabiki kwa namna yake ya kipekee anapowasili kambini.

Akiwa miongoni mwa wachezaji wanaopendwa na mashabiki, beki huyo wa kati wa Real Madrid, Ibrahima Konate alifika katika kituo cha Clairefontaine mara ya mwisho akiwa amevalia vazi la kawaida pamoja na kikoti cha rangi ya njano iliyong’ara, kiasi cha kumfanya asitambulike. Konate alionyesha kuwasili kwake kwa kushusha kofia ya ‘hoodie’ kabla ya kuwapigia picha wapigapicha, kana kwamba kujiamini kwake bado hakukutosha kufanya utambulisho wake uwe wazi. Wachezaji wenzake walijibu kwa utani uamuzi wake huo wakijaza sehemu za maoni kwenye mitandao ya kijamii kwa maoni yao.


FRA 02

MICHAEL OLISE

Mchezaji huyo mwenye mtindo wa kipekee ni gwiji wa mitindo kwa namna yake. Winga wa Bayern Munich na aliyewahi kucheza Crystal Palace mara nyingi huvaa mavazi yenye rangi kali na mvuto, yanayoongeza umaridadi wa mtindo wake.

Kwa Olise mara nyingi huchagua mwonekano wake wa kipekee ambao sasa umeanza kumtambulisha. Nyota huyo anajua kinachopendeza na daima hufanikiwa kukibeba vizuri. Mara ya mwisho akiwa Clairefontaine, Olise alifika akiwa amevalia koti linalofanana na ngozi, jeans pana za kawaida na begi jeusi.


FRA 01

MARCUS THURAM

Hakuna aliyetahadharisha kwamba Marcus Thuram angejitokeza katika kambi ya Ufaransa akiwa amevalia miongoni mwa mavazi ya kipekee ambayo umewahi kuyaona katika kambi za wachezaji kwa ajili ya timu ya taifa.

Akiwa amevalia koti la Louis Vuitton na miwani ya Prada katika vazi lililofanana na mtindo wa ‘Terminator’, nyota huyo wa Inter Milan alifanya kila kitu ili kuacha alama kubwa.

Thuram hasiti kujieleza kupitia mavazi yake, hivyo unaweza kumtaja kwa kujiamini kama alama ya mitindo na daima huvutia macho kwa mtindo wake wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa


FRA 03

BRADLEY BARCOLA

Mavazi ambayo Bradley Barcola huvaa anapowasili kwa ajili ya majukumu ya timu ya taifa yamekuwa ya kifahari, kipekee na mtindo uliopo sokoni.

Akiwa amevutia ulimwengu wa soka, winga huyo sasa anaonekana kama anayeshindania nafasi katika kila kazi ya uanamitindo. Hawezi kuzuilika.

Barcola aliheshimu urithi wake kwa njia ya kipekee kwa kuvaa mavazi fulani hivi, lakini yaliyotajwa kuwa ya heshima mbele ya kocha mpya, Zidane.