Mbappe aamriwa kuilipa PSG
Muktasari:
- Uamuzi huo uliotolewa Septemba 14, 2026, unahusiana na hasara za kifedha ambazo PSG ilidai ilipata baada ya akaunti zake za benki kuzuiwa kwa muda kufuatia hatua za kisheria zilizochukuliwa na mawakili wa Mbappe.
PARIS, UFARANSA; MZOZO wa kisheria kati ya mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe, na klabu yake ya zamani ya PSG umechukua sura mpya baada ya Mahakama ya Rufaa ya Paris kumuamuru mchezaji huyo kulipa Euro 60,000 (takribani Sh 180 milioni) kwa timu hiyo.
Uamuzi huo uliotolewa Septemba 14, 2026, unahusiana na hasara za kifedha ambazo PSG ilidai ilipata baada ya akaunti zake za benki kuzuiwa kwa muda kufuatia hatua za kisheria zilizochukuliwa na mawakili wa Mbappe.
Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, mahakama imekubali kwamba PSG ilipata gharama baada ya kulazimika kutafuta njia ya dharura ya mkopo ili kukabiliana na changamoto za ukwasi wakati akaunti zake zilipokuwa zimezuiwa. Hata hivyo, mahakama imekataa madai mengine ya PSG yaliyohusisha na fidia kwa kile klabu hiyo ilichodai kuwa ni madhara kwa maadili, taswira na sifa yake.
Majaji pia walikataa hoja za viongozi wa PSG kwamba hatua hizo za kisheria zingeweza kusababisha mgawanyiko ndani ya klabu au hata kuchukuliwa hatua za kinidhamu na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), wakisema madai hayo hayakuwa na msingi wa kutosha wa kimazingira.
Mzozo huo ulianza kuibuka Mbappe alipoondoka PSG na kujiunga na Real Madrid 2024, baada ya kipindi kirefu cha mvutano kuhusu hatma yake katika klabu hiyo ya Ufaransa. Baada ya kuondoka, Mbappe aliitaka PSG imlipe takribani Euro 60 milioni zilizohusishwa na bonasi na malipo mbalimbali ambayo alidai klabu hiyo ilikuwa haijamlipa.
Kesi hiyo inahusu kipindi cha siku 45, kuanzia Aprili 10 hadi Mei 25, 2025, ambacho PSG ilidai kuwa ilikumbwa na changamoto za kifedha kutokana na zuio hilo.
Mchezaji huyo alidai kuwa fedha hizo zilikuwa sehemu ya stahiki zake kutokana na makubaliano ya awali. Ingawa Kamati ya Sheria ya Ligi ya Hispania ilimuunga mkono Mbappe katika hatua fulani ya mzozo huo, suala hilo halikupata ufumbuzi wa haraka.
Mbappe baadaye alifungua kesi katika mahakama ya kazi nchini Ufaransa 2025 akitaka kulipwa fedha hizo.
Wakati mchakato huo ukiendelea, mawakili wa Mbappe walichukua hatua nyingine kwa kuomba mahakama izuie kwa muda baadhi ya fedha za PSG katika akaunti zake za benki. Hatua hiyo ya kisheria ililenga kuhakikisha kwamba iwapo Mbappe angepewa ushindi katika madai yake, angekuwa na uhakika wa kupata fedha hizo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo ilichukuliwa bila PSG kuwa na taarifa mapema na ilisababisha fedha za klabu hiyo kusimamishwa wakati mahakama ikiendelea kushughulikia mgogoro.
PSG ilipinga hatua hiyo ikidai kwamba ilikuwa na uwezo wa kifedha wa kutekeleza uamuzi wowote ambao ungetakiwa kulipa, na kuishutumu timu ya Mbappe kwa kuchukua hatua hiyo kwa kile ilichokiita "sababu za kutafuta umaarufu kwenye vyombo vya habari."
Mahakama hata hivyo iliondoa zuio hilo mwezi Mei 2025.
Miezi sita baadaye, Desemba 2025, mahakama ya kazi iliipa PSG jukumu la kumlipa Mbappe kiasi kikubwa zaidi, Euro 61 milioni.
PSG ilitekeleza uamuzi huo, ingawa kwa kusita, na hivyo kuonekana kana kwamba mzozo huo ulikuwa umefikia mwisho, lakini karibu mwaka mmoja baadaye, upande wa pili umejikuta nao ukitakiwa kulipa.