Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Labda Simba na Mpanzu wameacha urafiki wa mashaka

HISIA Pict


MAISHA yameendelea kuwa matamu Msimbazi. Siyo sana lakini kuna unafuu wa mambo. Juzi Simba alikuwa akimkandamiza TRA bila huruma. Mabao 3-0. Jana Simba waliachia picha za Tajiri wa Simba akiwa na Ellie Mpanzu Kibisawala. Amesaini mkataba mpya wa miaka miwili Msimbazi.


Hili la kwanza limekuwa muhimu. Mbio za ubingwa msimu huu zinazidi kuwa tamu. Wakubwa wamekuwa wakitoa sare zisizotarajiwa. Unapopata pointi muhimu zinakuwa muhimu kweli. Ni tofauti na misimu iliyopita.


Hili la pili la Mpanzu linaacha ukakasi kidogo. Maisha ya Mpanzu Simba yamekuwa na milima na mabonde. Jinsi kijana alivyoanza kujaribu kuibeba Simba wakati ikiwa na wachezaji wengi wasio na uwezo lilikuwa jambo la kusisimua.

Mpanzu alionekana kama Diego Maradona wa Argentina iliyotwaa kombe la dunia mwaka 1986. Alionekana mwokozi. Wakati mtani akiwa na mastaa wengi lukuki kina Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Clatous Chama, Maxi Nzingeli na wengineo, Simba walikuwa na Mpanzu.

Katika lile sakata la ‘hatuchezi’ watani wakaambiwa hauwezi kutwaa ubingwa bila ya kumkaba Mpanzu. Alikuwa wa moto kweli kweli. Hata hivyo, taratibu akaanza kupotea. Fomu ikafifia. Binafsi nilikuwa siipendi lugha yake ya mwili.

Nilikuwa namwona anacheza bila ya furaha. Hana tabasamu usoni. Wenzake wakifunga bao pia hana tabasamu usoni. Baadae watu wa Simba wakaanza kumgeuka. Ikaanza minong’ono mwili wake ulikuwa Simba, lakini akili yake ilikuwa Yanga.

HISI 01

Kwamba Mpanzu akaanza kuonekana kama msaliti. Kama vile alikuwa anaihujumu timu. Simba hawajawahi kukosa watu wa namna hii klabuni. Kina Chama na Aishi Manula wamewahi kupitia kipindi hiki. Kwamba unaishi na watu, lakini wanakuona sio mwenzao.

Kuna wale mashabiki nguli wa timu walikuwa wanasikika wakidai kama Mpanzu alikuwa anataka Kwenda Yanga basi ni bora aende tu. Kwamba walikuwa hawataki kuishi na watu mamluki ndani ya timu. Simba walionekana kuwa na jinamizi la watu kama hawa.

Wakati Simba wakiishi kwa hisia hizo, kuna watu wa Yanga wakiongozwa na msemaji wao, Ally Kamwe walionekana kutoa maneno ya kwamba Mpanzu alikuwa ni mchezaji wao lakini alikuwa anavaa jezi nyekundu na nyeupe. Kwamba lilikuwa jambo la muda tu.

HISI 02

Msimu huu siyo mzuri sana kwa Mpanzu hasa ilipofika Januari. Simba ilileta watu wa maana katika nafasi yake. kule pembeni Simba wamewaleta Libassa Gueye na Anicet Oura ambao wameiimarisha timu tofauti na zama za kina Joshua Mutale.

Lakini, ghafla Simba wamemuongezea mkataba wa miaka miwili Mpanzu. Wakati umuhimu wake ukiwa umepungua klabuni wameamua kumuongezea mkataba mpya wa miaka miwili.

Tukiwa wakweli Simba wamemuongezea mkataba wa miaka miwili huku kukiwa hakuna upinzani wa maana kutoka kwa maadui, labda wanapambana kumchukua.

HISI 03

Ishara ni nyingi hapa. Ukweli ni kwamba Simba wamewahi kumuona Mpanzu katika ubora wake. Wanajua tu kuna makandokando mengi yamepita hapa karibuni lakini Mpanzu ni mchezaji bora kwao.

Labda kuna mazungumzo ya kina yamepita kati yao na Mpanzu na kujua tatizo lake lilikuwa nini. Labda Simba wamegundua tatizo na wanajua Mpanzu atarudi katika ubora wake punde si punde.

Pia labda mkataba wa miaka miwili utamtuliza Mpanzu. Kwamba kwa sasa anajua hana sehemu yoyote ya kwenda na analazimika kuvaa jezi nyekundu na nyeupe kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

HISI 04

Inawezekana kuna sehemu alihisi anatakiwa na ikamuathiri kisaikolojia kiasi cha kushusha kiwango chake. Kwamba alikuwa anavaa jezi nyekundu na nyeupe huku mawazo yake yakiwa katika jezi nyingine. Huwa inawatokea wachezaji wengi hata katika zile nchi ambazo zimeendelea.

Cristiano Ronaldo aliwahi kuchezea Manchester United huku akili na Mawazo yake vikiwa Santiago Bernabeu. Uhamisho wake wa kwanza kwenda Real Madrid ulikwama na akili yake haikukaa sawa mpaka Sir Alex Ferguson alipomhakikishia atamuuza Kwenda Hispania msimu unaofuata.

Lakini inawezekana kuna maongezi mazito yamepita nyuma ya pazia na Mpanzu ameamua kusaini mkataba mwingine na sasa labda tunaweza kumuona yule wa miezi ya mwanzo pale Simba.

HISI 05

Mkataba wake una maana mbili. Kwanza kabisa amewahakikishia Wanasimba yeye ni Simba kweli. Lakini pili labda ameamua kurudisha umuhimu wake klabuni. Siku hizi wala sio mchezaji tegemeo kama zamani. Wamekuja watu wapya kutoka Afrika Magharibi na wanapiga kazi.

Inaonekana ameamua kurudisha heshima yake Simba na anapaswa kupambana hasa. Siku hizi hata akikaa benchi hakuna shabiki wa Simba anayeshtuka. Na kitu kizuri zaidi ni timu yenyewe inafanya vizuri. Inateleza hapa na pale lakini kwa jumla imekuwa ikifanya vizuri zaidi kuliko wakati wa akina Mutale na wakati wake akiwa staa.

Kitu cha msingi zaidi kwa pande zote ni inawezekana huu ni mwisho wa uhusiano wa mashaka baina yao. Hapo Katikati hawakuwa vizuri. Na watu wa Simba wana kumbukumbu mbaya namna uhusiano wao wa mashabiki na Chama ulipoishia. Alikwenda Yanga.

Kwa Mpanzu na Simba huu labda ni ukurasa mpya wa kupiga kazi. Kitu kizuri hata akipiga kazi sana lakini Simba wamepunguza umuhimu wake uliotukuka klabuni. Wakati mwingine wachezaji wazuri wanahitaji jambo hili. Hasa wachezaji wenye tabia ya maringo. Unawaletea wapiga kazi wengine ili wawe na adabu katika kazi yao. Kila la kheri kwa ukurasa mpya kati ya Simba na Mpanzu.