Prime
Diarra imetosha sasa, lazima abadilike!
DUARA ni umbo la namba sifuri na namba sifuri maana yake hamna kitu. Kipa wa Yanga, Djigui Diarra sasa anaanza kupotea. Anaanza kuwa sifuri. Anaanza kuwa hamna kitu.
Tangu amekuja Tanzania mwaka 2021, Diarra amekuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa kigeni. Uwezo mkubwa langoni, nidhamu kubwa mchezoni. Yeye ni mfano wa makipa wa kisasa, wanaojua kucheza mpira kwa miguu...sio tu kuzuia mashuti kwa mikono.
Diarra anajua kupiga pasi ndefu na fupi na ikafika kwa mchezaji aliyemkusudia...ana uwezo mkubwa sana. Lakini baada ya miaka mitano sasa nchini, sifa mpya imeanza kujitokeza.
Diarra ameanza kuwa mtovu wa nidhamu, mkaidi na muanzisha vurugu. Kwenye mechi dhidi ya Azam, Machi 15, alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa la kutoka golini kwake hadi karibu na goli la Azam kuchochea vurugu.
Kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Machi 21 (siku ya sikukuu ya Idd), Diarra alifanya zaidi ya hapo.
Alitoka golini kwake, akamfuata mwamuzi kutaka kumfanyia vurugu...wenzake wakamzuia lakini bado alikuwa mshari.
Mpira uliopoisha ndiyo ilikuwa zaidi. Akaanzisha ugomvi mwingine wa hali ya juu. Meneja wake wa timu, Walter Harrison, akajitahidi kumzuia lakini aliishia kupigwa kabali ya shingo...roba! Wachezaji wenzake wakashindwa hadi rais wa klabu yake, Hersi Said.
Kama hiyo haitoshi, wakati yeye na wachezaji wenzake wanatoka chumba cha kuvali wapande basi na kuondoka, akaendelea na ukosefu wake wa adabu kwa kuwatukana waandishi wa habari kwa kuwaonesha kidole cha kati.
Diarra aliyekuwa mfano, sasa anakuwa duara...anakuwa sifuri...anakuwa hamna kitu. Na hii yote inatokana na makosa yake uwanjani.
Diarra anafanya vurugu ili kuhamisha mjadala kutoka madhaifu yale ya uwanjani na kuwa gumzo za vurugu.
Bao ambalo Yanga walifungwa na Mtibwa Sugar ni makosa yake yeye binafsi. Kwanza hakuipanga vizuri safu yake ya ulinzi. Kwa kipa mfupi kama yeye, hakutakiwa kuruhusu beki mfupi kama Yao Kouassi kusimama kwenye nguzo ya kwanza.
Mkiwa wafupi wote katika mazingira kama yale, ni hatari kwenu...na Diarra analijua hilo, lakini hakuwa makini.
Suala la pili, alipaswa kuwakumbusha walinzi wake kumtoa yule mchezaji wa Mtibwa aliyesimama mbele yake.
Badala yake akawa anapambana naye kwa kumsukuma na kumghasi akidhani anamtoa mchezoni...kumbe anajighasi mwenyewe na kujitoa mchezoni.
Kona ikaja mbele ya mtu mfupi Yao Koussi, ikampita...nyuma yake alikuwepo mchezaji wa Mtibwa ambaye Diarra alikuwa anahangaika naye hapo awali.
Mchezaji huyu akamziba Diarra kuuona mpira uliomzidi Koussi, akashtukia umefika...ukamshinda, goli.
Sasa kuficha madhaifu haya, akatoka golini kumlalamilia mwamuzi.
Hapa ndipo inapokuja ile kaulimbiu ya VETA, "Fundi asiye na ujuzi, hulaumu vifaa vyake". Diarra alikosa maarifa kwenye kupambana na shambulizi la kona la Mtibwa Sugar...lakini analaumu mwamuzi.
Hii ni dalili mbaya kwake na kwa Yanga kwa jumla. Na hii ni kwa sababu tangu amekuja nchini, hajawahi kupata mpinzani wa kumtia changamoto kwenye nafasi yake.
Amekuwa mfalme kiasi kwamba anachelewa kurudi kazini kutoka kwao, anakuja siku ya mechi ya watani wa jadi ana anapokewa uwanja wa ndege moja kwa moja hadi Uwanja wa Mkapa.
Hii ilitokea Oktoba 19, 2024, siku ya bao la kujifunga la Kelvin Kijiri. Ile siku Diarra aliingia uwanjani wakati wa kupasha misuli moto, akitokea uwanja wa ndege. Sasa kipa kama huyu lazima atabweteka kwa sababu anajua kabisa kawashika pabaya.
Kubweteka kwake husababisha makosa rahisi kama yanayotokea...na kisha kuhangaika kuyaficha kwa matukio ya kibabe. Kipa anawezaje kumpiga kabali meneja wa timu kiasi kile, tena hadharani?
Ule ni uhalifu...ni kosa la jinai ambalo anaweza hata kufungwa nalo jela...siyo tu kufungiwa na kamati ya saa 72.
Diarra ameanza kuwa duara. Ameanza kuwa sifuri. Ameanza kuwa hamna kitu. Ni wakati muafaka kwa Yanga kuanza kujipanga na maisha bila yeye. Miaka mitano kamili aliyohudumu na huu wa sita anaoenda kuumaliza, inatosha.
Siyo lazima kumuacha sasa, lakini kumpatia mbadala wake kwanza. Diarra akipata mpinzani kwenye nafasi yake na akawekwa benchi mechi kadhaa akili itamkaa sawa. Atapata muda wa kutafakari na kujua anakosea wapi. Kipa namba moja wa taifa la vipaji kama Mali anapaswa kufanya zaidi ya anavyofanya.
Kipa namba moja wa klabu kubwa Tanzania kama Yanga, anapaswa kuelewa anabeba ndoto za watoto wengi.
Haya anayofanya ni picha mbaya kwa jamii...akemewe. Mamlaka za mpira zichukue hatua...afungiwe. Hii itaisaidia Yanga kuanza kunusa hatari...kwamba kumbe ipo siku isiyo na jina, hawatokuwa na Diarra kwa sababu yoyote ile.
Kwa hiyo asipokuwepo, maisha yatakuwaje...hilo swali ni muhimu wakaanza kujiuliza sasa.
Pata picha akifungiwa mechi tatu, Aprili 4 ni Yanga dhidi ya Tanzania Prisons, Aprili 8 kuna mechi kati ya Pamba Jiji dhidi ya Yanga ilhali Aprili 16 ni Yanga dhidi ya Mbeya City.
Baada ya hizi mechi, Diarra atakuwa amejifuza na Yanga watakuwa wamejifunza. Maisha baada ya hapo yatakuwa na nidhamu sana kwa pande zote. Usipoziba ufa utaja jenga ukuta!