Kumbukumbu kadi nyekundu, njano zageuka heshima kwa Messi
Muktasari:
- Mbali na kadi hizo za zawadi, kadi za kinidhamu alizoonyeshwa Messi kwa zaidi ya miaka 20 ya soka la ushindani la zaidi ya mechi 1,100, amepata kadi nyekundu mara tatu, huku za njano zikiwa zaidi ya 100.
Kadi nyekundu na njano ambazo kwa kawaida huwa ishara ya adhabu uwanjani, ziligeuka zawadi ya kumbukumbu kwa Lionel Messi katika usiku wa mwisho wa safari yake ya soka kimataifa akiwa na Argentina.
Mbali na kadi hizo za zawadi, kadi za kinidhamu alizoonyeshwa Messi kwa zaidi ya miaka 20 ya soka la ushindani la zaidi ya mechi 1,100, amepata kadi nyekundu mara tatu, huku za njano zikiwa zaidi ya 100.
Mwamuzi wa Chile, Fernando Vejar, alimkabidhi Messi kadi hizo mbili baada ya filimbi ya mwisho katika mechi yake ya mwisho ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 dhidi ya Benin, uliomalizika kwa Argentina kushinda mabao 3-0.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Monumental, Messi alifunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao, akifunga ukurasa wa miaka 21 ya kuitumikia Argentina kwa namna ya kipekee.
Baada ya mechi, Vejar alimfuata Messi na kumkabidhi kadi alizotumia katika mechi hiyo, pamoja na mpira wa mechi, kama kumbukumbu ya usiku huo badala ya kuwa ishara ya nidhamu aliyokuwa amezoea kuitumia katika maisha yake ya uamuzi.
Kwa mujibu wa gazeti la Italia, La Gazzetta dello Sport, tukio hilo lilitokea baada ya mechi kumalizika, wakati wachezaji wa Benin nao walipomzunguka Messi kumpa heshima katika usiku wake wa mwisho akiwa amevaa jezi ya Argentina.
Taarifa kutoka Argentina, kupitia TN, zilisema baadaye Messi alimkabidhi mwimbaji Soledad Pastorutti kadi hizo, ambaye alitumbuiza katika hafla ya kumuaga nyota huyo.
Kwa kawaida, kadi nyekundu humaanisha mchezaji kutolewa uwanjani, huku ya njano ikiwa onyo. Lakini usiku huo, kadi hizo zilibadilika maana na kuwa alama ya heshima kwa mchezaji aliyebadili historia ya soka la Argentina.
Mchezo huo ulikuwa wa 208 kwa Messi akiwa na Argentina, akifikisha jumla ya mabao 126 na pasi za mwisho 70 katika kipindi chake cha kuitumikia timu hiyo.
MESSI NA MIAKA 22 YA NIDHAMU UWANJANI
Messi amemaliza safari yake ndefu ya soka akiwa ameacha kumbukumbu nyingi uwanjani mabao, mataji, rekodi na tuzo, lakini mojawapo ya sifa ambazo zimeambatana naye kwa miaka zaidi ya 20 ni nidhamu.
Katika kipindi hicho, Messi amepita kwenye ushindani mkali katika ligi mbalimbali, michuano ya Ulaya, Kombe la Dunia, Copa América na mechi za timu ya taifa, lakini idadi ya mara alizoonyeshwa kadi nyekundu imebaki kuwa ndogo ikilinganishwa na muda aliotumia uwanjani.
Katika zaidi ya mechi 1,100 za ushindani, Messi ameonyeshwa kadi nyekundu mara tatu pekee, zote zikiwa ni za moja kwa moja na si kutokana na kukusanya kadi mbili za njano katika mchezo mmoja.
Kadi yake ya kwanza ilikuja wakati ambao wengi walikuwa bado hawajafahamu ukubwa wa kipaji chake.
SEKUNDE 43 ZA KWANZA ZA MESSI ARGENTINA
Agosti 17, 2005 ni siku ambayo Messi aliingia rasmi katika historia ya timu ya taifa ya Argentina, lakini haikuwa kwa namna ambayo angependa kukumbukwa.
Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 18, Messi aliingia kama mchezaji wa akiba katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Hungary.
Hata hivyo, safari yake katika timu ya taifa ya wakubwa ilianza kwa tukio la kushangaza. Sekunde chache baada ya kuingia uwanjani, takribani 43 kulingana na baadhi ya kumbukumbu alionyeshwa kadi nyekundu.
Mwamuzi aliamua kuwa Messi alikuwa amemkabili beki wa Hungary, Vilmos Vanczák, kwa kiwiko wakati beki huyo alipokuwa akimvuta jezi.
Ilikuwa mwanzo mgumu kwa mchezaji ambaye baadaye angekuwa mmoja wa wachezaji mashuhuri zaidi katika historia ya soka. Lakini, kadi hiyo haikuwa ishara ya tabia ambayo ingemtawala Messi katika miaka iliyofuata.
MIAKA 14 BAADAYE AKAPEWA NYEKUNDU TENA
Baada ya tukio hilo la Hungary, Messi alisubiri karibu miaka 14 kabla ya kuonyeshwa kadi nyingine nyekundu akiwa na Argentina.
Julai 6, 2019, katika Copa América iliyofanyika Brazil, Messi alihusika katika tukio lililomkutanisha na nahodha wa Chile, Gary Medel.
Argentina na Chile zilikuwa zikicheza mechi ya kusaka mshindi wa nafasi ya tatu. Mpira ulipotoka nje ya uwanja, Medel alimfuata Messi na kuanza kumkabili kwa nguvu. Wawili hao walikabiliana kwa kusukumana vifua, kabla mwamuzi kuamua kuwa wote wawili walistahili kutolewa.
Kwa Messi, ilikuwa kadi yake ya pili nyekundu akiwa na Argentina.
Tukio hilo lilikuwa tofauti na lile la mwaka 2005 kwa sababu safari hii Messi alikuwa tayari mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi duniani na nahodha wa Argentina.
KADI YAKE PEKEE AKIWA KLABUNI
Kadi ya tatu na ya mwisho nyekundu katika historia ya Messi ilikuja Januari 17, 2021.
Barcelona ilikuwa ikicheza dhidi ya Athletic Bilbao katika fainali ya Spanish Super Cup. Mchezo ulikuwa umefika dakika za mwisho za muda wa nyongeza wakati Messi alipambana na Asier Villalibre. Katika tukio hilo, Messi alimpiga Villalibre kwa nyuma wakati akijaribu kujitengenezea nafasi ya kukimbia.
Mwamuzi alitumia VAR kabla ya kuamua kumwonyesha kadi nyekundu.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza na pekee Messi kutolewa kwa kadi nyekundu akiwa katika klabu.
ZAIDI YA KADI 100 ZA NJANO
Ingawa kadi nyekundu ni chache, Messi hajamaliza safari yake bila kuonyeshwa kadi za njano.
Kumbukumbu za takwimu za maisha yake ya soka zinaonyesha kuwa amekusanya zaidi ya kadi 100 katika kipindi chote cha kucheza kwake.
Barcelona ndiyo iliyochangia sehemu kubwa ya kadi hizo, huku kumbukumbu zikionyesha takribani kadi 82 za njano katika kipindi chake akiwa na klabu hiyo.
Akiwa Paris Saint-Germain, idadi yake ya kadi ilikuwa ndogo zaidi, ikiwa ni moja katika kipindi chake nchini Ufaransa.
Baada ya kuhamia Inter Miami nchini Marekani, Messi ameendelea kuongeza idadi hiyo, huku pia akiwa amekusanya kadi katika safari yake ya baadaye ya soka.
Kwa Argentina, kadi zake zimepatikana katika mazingira tofauti, kuanzia mechi za kirafiki hadi kufuzu na michuano mikubwa.