KONA YA MICHARAZO: TFF wabadili mfumo wa usajili Ligi Kuu Bara twende na wakati
Muktasari:
WAKATI Ligi Kuu ya Soka Bara inaelekea ukingoni harakati za usajili wa wachezaji kwa ajili ya klabu kuimarisha timu zao kwa msimu ujao zimeanza.
WAKATI Ligi Kuu ya Soka Bara inaelekea ukingoni harakati za usajili wa wachezaji kwa ajili ya klabu kuimarisha timu zao kwa msimu ujao zimeanza.
Kwa kawaida kipindi cha usajili wa wachezaji kinakuwa na hekaheka kubwa, kila Klabu inapigania kupata wachezaji hodari kwa ajili ya kikosi chake. Kwa upande mwingine ni kipindi cha mavuno kwa wachezaji hasa wale walionesha kiwango kikubwa katika msimu uliomalizika kwani wanaweza kuvuna dau kubwa la fedha. Lakini pia ni kipindi cha hadhari kwa klabu kwani isipokuwa makini inaweza kujikuta imesajili wachezaji kwa kitita kikubwa cha fedha lakini wasiwe na manufaa kwa timu yao.Vilevile ni kipindi cha mtihani kwa wachezaji kwani wasipokuwa makini wanaweza wakajikuta wanasajiliwa katika timu ambazo watakosa nafasi za kucheza.
Wachezaji wanapaswa waepuke udanganyifu wa kujisajili zaidi ya Klabu moja kwa tamaa ya fedha kwani kufanya hivyo kunaweza kufanya wafungiwe kucheza soka au hata kupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa utapeli.
Timu zisisajili kwa pupa
Klabu zinapaswa kuwa na hadhari katika kipindi hiki cha usajili kwa kuchukua wachezaji ambao watakuwa na manufaa katika timu zao.Usajili wa wachezaji ulenge zaidi katika kuimarisha vikosi walivyonavyo sasa. Timu ambayo itakuwa inabadilisha wachezaji kila msimu haiwezi kuwa na kikosi imara. Jambo la msingi ni kazi ya usajili wa wachezaji kuachwa kwa benchi la ufundi ambalo ndilo linaloelewa upungufu wa timu yao na kazi hiyo isifanywe na viongozi wa klabu.
Benchi la ufundi ndio linalopaswa kupendekeza wachezaji gani wasajiliwe katika timu zao na sio viongozi kusajili kutokana na mapenzi yao kwa wachezaji.
Mikataba iwe safi
Ni jambo zuri kwamba Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) liliweka sheria ya mchezaji kuwa na mkataba anapojisajili kwenye klabu yoyote.
Jambo hilo ni la msingi kwa wachezaji na klabu kwani kila upande unajua wajibu wake na haki yake kwa hiyo la msingi hapo ni kila upande kutimiza wajibu wake. Kuwa na mikataba ni jambo moja lakini kuwa na mikataba mizuri na iliyo wazi na inayojali maslahi ya pande zote ni jambo jingine lakini ndio la muhimu zaidi. Kwa hiyo ni muhimu kwa wachezaji kuhakikisha kwamba kabla hawajaweka saini zao wanaisoma vizuri na kuielewa ili isije ikawa kikwazo baadae. Ni muhimu katika hali ya sasa wachezaji kuacha mtindo wa kufanya mambo yao peke yao bali ni bora kwa faida zao kuwa na mameneja wanaosimamia maslahi yao.
Tarehe za usajili ziwe za kimataifa Miaka michache iliyopita Tanzania ilibadili mfumo wa uendeshaji ligi kuu badala ya kuanza Januari-Februari na kumalizika Novemba-Desemba na kuingia katika mfumo wa kimataifa wa kuanza ligi Agosti na kumalizika Mei.Mfumo huo ndio unaotumika kupanga ratiba za michuano mbalimbali inayosimamiwa na Fifa, CAF zikiwemo mechi za kimataifa za kirafiki.Lakini hivi sasa Tanzania mbali na kufuata mfumo huo lakini katika usajili imekuwa na utaratibu wake ambao bila shaka hauzisaidii klabu.
Usajili wa wachezaji Tanzania unafanyika katika kipindi ambacho ni Tanzania peke yake inaendesha usajili wa wachezaji.Kuna haja kwa TFF kuliangalia upya suala hili ili klabu za Tanzania zifanye usajili wakati soko liko wazi duniani kote kwa hiyo huifanya kazi hiyo kuwa rahisi na nyepesi.Wakati wa usajili wa wachezaji unaendelea duniani kote inakuwa rahisi kupata wachezaji hodari na wazuri kwani klabu itakuwa tayari kuuza wachezaji wake kwa matumaini kwamba itapata fedha na kuzitumia kununua wachezaji wengine kuziba mapengo ya wachezaji waliondoka.
Kwa hiyo itakuwa rahisi kwa klabu za Tanzania kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuziimarisha timu zao na si kutarajia kusajiliwa wachezaji ambao ni huru tu ambao si siku zote wanakuwa katika kiwango kilicho bora.
Lakini pia klabu za Tanzania zitakuwa na nafasi nzuri ya kuuza wachezaji wake nje ya nchi iwapo watatakiwa huko kwa vile zitakuwa zipo kwenye nafasi ya kusajili wachezaji wengine kuziba mapengo yao kwa vile usajili utakuwa unaendelea.
Katika mazingira ya sasa klabu za nje zikiwataka wachezaji wa Tanzania klabu hizo zitakuwa katika ugumu wa kuwauza wachezaji hao na kushindwa kujipatia fedha kwani hawatakuwa na njia mbadala ya kuziba mapengo yao kwa vile usajili wa wachezaji haufanyiki Tanzania katika kipindi hicho.Kwa hiyo kuna umuhimu TFF ikabadili tarehe za usajili wa wachezaji Tanzania ili kwenda katika tarehe za kimataifa ili kuifanya Tanzania kufaidika kama zilivyo nchi zingine duniani.Hili ni jambo rahisi kulitekeleza kwani halina gharama yoyote na wala halina kikwazo chochote katika uendeshaji wa ligi hiyo bali itatoa matunda zaidi na kuifanya ligi hiyo kuvutia zaidi.
Wakati umefika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kuendeshwa kisasa ili iweze kupata mafanikio na pia kuwa katika kiwango kizuri na kuwavutia wadhamini zaidi jambo.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi na Mhariri Mkongwe nchini.
Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020