Kombe la Dunia U-20, kundi A la Moto
Muktasari:
- Ni kundi lenye sura mbili tofauti. Upande mmoja kuna timu zenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa kama Argentina na Mexico, upande mwingine kuna Poland na Benin ambao wote wanaingia kwenye fainali hizo kwa mara ya kwanza.
SAFARI ya Kombe la Dunia la FIFA U-20 la Wanawake 2026 inaanza rasmi leo, Septemba 5 nchini Poland, huku macho yakielekezwa kwenye Kundi A ambalo limewakutanisha wenyeji Poland, Argentina, Mexico na Benin.
Ni kundi lenye sura mbili tofauti. Upande mmoja kuna timu zenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa kama Argentina na Mexico, upande mwingine kuna Poland na Benin ambao wote wanaingia kwenye fainali hizo kwa mara ya kwanza.
Mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 2002 nchini Canada huku Marekani akiandika historia ya kuwa timu ya kwanza kubeba taji hilo ambalo kwa mwaka huu inakuwa toleo lake la 12.
Poland ambao ndiyo wenyeji, Benin nao ni miongoni mwa timu sita ambazo ni mara yao ya kwanza kushiriki fainali hizo.
Wenyeji wamepangwa kundi hilo ambalo linaanza kwa kishindo leo, wakati Poland watakapokutana na Argentina huko Katowice, huku Mexico ikicheza dhidi ya Benin.
Mwanaspoti linakuchambulia makundi hayo na timu gani ina nafasi ya kufanya vizuri na kuandika historia.
POLAND NA HISTORIA
Poland ndiyo timu yenye hadithi ya kipekee zaidi katika kundi hili.
Hawajawahi kushiriki Kombe la Dunia la U-20 la Wanawake, lakini wamepata nafasi hiyo kwa kuwa wenyeji wa mashindano.
Wanaingia wakiwa na nafasi ya kuandika historia kwa mara ya kwanza.
Faida yao kubwa ni mashabiki. Kuanzia mchezo wa kwanza dhidi ya Argentina, Poland watakuwa na nguvu ya kucheza mbele ya mashabiki wao. Hilo linaweza kuwapa morali, hasa katika dakika ambazo mchezo utakuwa mgumu.
Lakini kwenye faida hiyo ya kuwa wenyeji timu hiyo itakuwa na presha.
Mashabiki watataka kuona wenyeji wakishinda, na presha hiyo inaweza kuwa mzigo kwa kikosi ambacho hakijawahi kucheza fainali.
Poland wanaweza kutumia faida ya nyumbani kwa kucheza kwa ujasiri, lakini wanahitaji nidhamu kubwa hasa wanapokutana na Argentina na Mexico ambao wana uzoefu zaidi wa mashindano haya.
ARGENTINA
Argentina wanaingia kwenye fainali hizo hii ikiwa ni mara yao ya pili mfululizo baada ya kushiriki mara ya kwanza mwaka 2024 walipoishia hatua ya 16 bora.
Hivyo timu hiyo inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa tayari imeonja joto la ushindani wa Kombe la Dunia.
Walifuzu baada ya kufanya vizuri kwenye Mashindano ya Amerika Kusini ya U-20 mwaka 2026, wakashindi mabao 3-0 dhidi ya Colombia katika mchezo wa mwisho wa kufuzu. Mercedes Diz alifunga mabao yote matatu katika mchezo huo.
Argentina walimaliza hatua ya awali wakishinda mechi zote nne, wakifunga mabao 12 na kuruhusu mawili pekee kabla ya kuingia hatua ya mwisho.
Hilo linaonyesha kwamba wanaweza kuwa timu yenye uwezo mkubwa wa kufunga na pia kudhibiti wapinzani.
Miongoni mwa nyota wenye mchango mkubwa kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji Mercedes Diz ambaye alifunga hat-trick iliyoipeleka Argentina Kombe la Dunia.
MEXICO
Mexico ni moja ya timu ambazo hazipaswi kupuuzwa kwenye kundi hili.
Mexico imecheza mara 10 kwenye Kombe la Dunia la U-20 la Wanawake, huku mafanikio yao makubwa yakiwa ni kufika robo fainali nne mwaka 2010, 2012, 2016 na 2022 na mwaka 2024 walifika hatua ya 16 bora.
Hiyo inamaanisha Mexico wanaingia Poland wakiwa na uzoefu mkubwa kuliko Poland na Benin, na pia wamekuwa wakishindana mara kwa mara na mataifa makubwa ya soka la vijana.
Mexico imekuwa ikisogea karibu na mafanikio makubwa lakini haijawahi kucheza fainali. Kwenye mashindano ya Concacaf ya U-20 mwaka 2025, Mexico ilifika fainali na kupoteza dhidi ya Canada kwa mabao 3-2 baada ya muda wa ziada. Hata hivyo, ilikuwa ni kampeni iliyowawezesha kufuzu Poland na kuonyesha uwezo wao wa kushindana.
Mchezaji wa kuangaliwa kutoka kikosi hicho ni Montserrat Saldívar, ambaye alitwaa tuzo ya mchezaji bora na pia kiatu cha dhahabu katika mashindano ya Concacaf ya 2025 baada ya kufunga mabao manane. Alifunga pia mabao mawili katika fainali dhidi ya Canada ni aina ya mchezaji ambaye anaweza kubadilisha mchezo kwa muda mfupi.
BENIN
Kama ilivyo kwa Poland, Benin inacheza kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia
Lakini safari yao ya kufuzu inaonyesha kwamba hawakufika Poland kwa bahati. Katika raundi ya tatu ya mchujo wa Afrika, Benin walionyesha ubora dhidi ya Misri, wakisonga mbele baada ya ushindi mkubwa wa 4-0 katika mchezo wa pili.
Katika raundi ya mwisho, Benin walikutana na Ivory Coast katika pambano la kutafuta tiketi ya Poland.
Walishinda kwa jumla ya mabao 5-2, na hivyo kukata tiketi yao ya kwanza kwenye fainali za dunia za U-20 za wanawake.
Hapo ndipo nguvu yao ilipo Benin wanaingia bila presha kubwa ya historia.
Wengi wanawachukulia kama timu ndogo kwenye kundi lakini inaweza kuonyesha maajabu.
KUNDI A NANI ANA NAFASI?
Kwa kuangalia historia na uzoefu, Argentina na Mexico wanaonekana kuwa na faida kubwa zaidi kwenye kundi hili.
Argentina wanaingia wakiwa wametoka kwenye kampeni nzuri ya Amerika Kusini, wakati Mexico wana historia ndefu ya mashindano hayo na walifika fainali ya Concacaf mwaka 2025.
Poland wana faida ya nyumbani, jambo ambalo linaweza kubadilisha hesabu zote kwa Benin upande mwingine, wanaweza kuwa kikosi cha kushtukiza.
Mfumo wa mashindano unaipa nafasi timu mbili za juu kutoka kila kundi kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora, huku pia timu nne bora zilizomaliza nafasi ya tatu zikiingia hatua hiyo hivyo timu hizo zina nafasi kama zitamaliza na pointi nyingi.