Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Morocco alivyodhulumiwa haki yake Taifa Stars

NONDO Pict


UMESALIA kama mwezi mmoja na ushei kabla ya kuanza kwa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco.


Fainali hizo za 35 zinatarajiwa kuanza Desemba 21 mwaka huu hadi Januari 18 mwakani ikishirikisha jumla ya nchi 24 zitakazochuana kwenye viwanja tisa zilivyopo katika miji sita tofauti.


Tanzania ni miongoni mwa nchi shiriki za fainali hizo ikiwa ni mara ya nne baada ya ya kufanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023, huku ikifuzu safari hii kwa mara ya kwanza ikiwa chini ya kocha mzawa, Hemed Suleiman 'Morocco'.

Hata hivyo, Kocha Morocco hatakuwa miongoni mwa makocha watakaoshiriki fainali hizo baada ya kusitishiwa mkataba aliokuwa nao wa kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ndio waajiri wa Morocco, walitangaza kuachana naye, huku mwenyewe akinukuliwa kutokuwa na taarifa rasmi zaidi ya kusikia na kuona mtandaoni na mbadala wa kocha huyo ni Miguel Gamondi raia wa Argentina.

NON 01

Gamondi amepewa nafasi ya kuiongoza Stars katika fainali hizo za Morocco kuchukua nafasi ya kocha Morocco.

Morocco ametemeshwa kibarua akiwa ameiongoza timu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na miezi takriban 10 tangu alipoachiwa alipokaimishwa ukocha wa Stars Januari mwaka jana baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Adel Amrouche kufungiwa na CAF.

Amrouche aliadhibiwa na CAF kwa kusimamishwa mechi nane na kutoza faini ya Dola 10,000 kwa tuhuma za kutoa kauli tata dhidi ya shirikisho hilo kwa Morocco na Januari TFF ikatangaza kumsimamisha na kumteua kocha Morocco kumaliza mechi na kumkaimisha cheo hadi mapema wiki hii walipotangaza kuachana naye na kumteua Gamondi.

Gamondi anayeinoa pia Singida Black Stars sasa ana jukumu la kuiandaa Stars ili kwenda nayo kwenye fainali hizo.

NON 02

Licha ya kwamba kiuhalisia hakuna muda sahihi wa kubadilisha kocha, lakini kuna njia ambazo hushauriwa juu ya uamuzi wao kwa mustakabali wa timu husika.

Hata hivyo, hapa mjadala siyo kubadilishwa kwa Morocco na kuingia kwa Gamondi, ishu ni sababu za mabadiliko. Je ni ya dharura au mwalimu aliyekuwepo hana uwezo wa kwenda na timu katika fainali hizo?

Binafsi naona ni kama tumemkosea heshima kocha Morocco, ambaye kwa moyo wake alijitoa kuhakikisha anafanikisha malengo aliyopewa ya kuipeleka timu katika fainali hizo za Afcon bila kujali matatizo na changamoto zilizokuwepo.

NON 03

Changamoto ambazo ni za kuanzia katika benchi hadi kwa wachezaji, kwani mazingira ambayo taasisi zetu za michezo zimekuwa zikijitahidi zisiwatokee makocha wa kigeni tofauti na kwa wazawa.

Kwangu naona Morocco ni shujaa wa taifa aliyedhulumiwa haki yake ya kuondolewa kwa heshima baada ya fainali za Afcon 2025 na kuruhusu mpango mpya wa Afcon 2027 tukiwa wenyeji kama kulikua na ulazima. Watu wanasema mnyonge mnyongeni...!

Najua watu wengi wanatazama matokeo ya mechi na sio mwisho wa michuano, huenda ni sawa, lakini katika soka kuna matokeo matatu, kushinda, kushindwa na sare ila mwisho wa mashindano ndio muhimu zaidi.

Chini ya kocha Morocco tulikuwa tumeshafuzu Afcon 2025 Morocco na pia kulikuwa na mbio za kuwania Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (Chan) 2024 ambazo imefanyioka mwaka huu Tanzania ikiwa wenyeji sambamba na Kenya na Uganda.

NON 04

Morocco alitufikisha katika fainali hizo za tatu baada ya zile za 2009 na 2020 tulizopelekwa na makocha wa kigeni, Marcio Maximo na Etienne Ndayiragije, lakini alikuwa na kazi ya kuisaka tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026 tulizokwama jioni.

Kama kushindwa kwenda Kombe la Dunia 2026 ndio kipimo cha kumng'oa Morocco, basi tunatakiwa kumuomba radhi kwani tumemvunjia heshima hata kama ni kweli tulikuwa na nafasi kubwa ya kuingia katika mechi za play-off.

Inawezekena ni kweli Morocco sio kocha mzuri, lakini ndiyo tumhukumu kwa kuzikosa fainali za Kombe la Dunia ambazo rekodi zinaonyesha Afrika licha ya kuwa na nchi nyingi duniani, lakini ni mataifa machache yasiyofikia hata 10 yaliyowahi kushiriki.

Ieleweke wazi sipingi kuondolewa kwa kocha Morocco, ila naona utanzania wake ukimhukumu zaidi kuliko kazi kubwa aliyoifanya wakati akiinoa Stars ikiwa kuweka rekodi ya kuiwezesha Tanzania kufika robo fainali ya CHAN 2024 na kushinda mechi za makundi katika ushiriki wake wote wa michuano ya kimataifa tangu tupate uhuru.

NON 05

Nalisema hili kwa sababu sisi ndio tuliowashangilia baadhi ya walimu waliofanikisha sisi kwenda Afcon mbona kwa Morocco inaonekana kawaida na kuonekana kufeli.

Ndiyo, tunahitaji mafanikio zaidi ila tunapaswa kuheshimu na kuthamini yale tuliyonayo japo mabadiliko sio jambo baya ila tusimnyime heshima yake Hemed Morocco, kwani hii itakuwa ni sawa na kumdhulumu kwa mazuri aliyoifanyia Stars na kutupa heshima.

Gamondi kama rubani mpya katika chombo kile kile kwa utaratibu ule ule wa kukaimu, japo najua hauwezi kuwa sawa na mzalendo mwenzangu Hemed Morocco, kwa sababu tunaficha vyombo vya zamani na kutoa vipya kwa ajili ya wageni huku familia zetu zikitumia vyombo vikuu kama baadhi ya familia huwafanyia vijana wazawa.

Hizi ndizo tabia tunazoziendeleza katika nyanja mbali mbali ikiwemo michezo, kisha mwishowe tunaishia kujilaumu kwa kushindwa kuwa na makocha na wachezaji wenye uzalendo kwa kutambua, hata wanaliofanya huwa halina thamani mbele ya wageni.

Pumzika kwa heshima kocha Morocco, Mzalendo kutoka visiwani, mtu wa boli na karibu Gamondi, twende Afcon 2025 kwa nia ya kulinda hadhi ya Stars na ikiwezekana tuweke rekodi nyingine tamu kimataifa, kwani hakuna kisichowezekana chini ya jua.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars!