Klabu zilizotumia mkwanja mrefu kusajili dirisha moja
Muktasari:
- Klabu zimekuwa zikichuana kutengeneza vikosi imara kwenye kila kipindi cha dirisha la usajili linapofika na hapo ndipo zinapoibuka timu zinazofanya usajili wa pesa nyingi kuzidi nyingine katika harakati za kubeba wakali wapya.
LONDON, ENGLAND: MABINGWA wa Ligi Kuu England, Liverpool wanakaribia kuweka rekodi ya kuwa timu iliyofanya matumizi makubwa kwenye dirisha la usajili, orodha ambayo kwa sasa imetawaliwa na Chelsea na Real Madrid.
Klabu zimekuwa zikichuana kutengeneza vikosi imara kwenye kila kipindi cha dirisha la usajili linapofika na hapo ndipo zinapoibuka timu zinazofanya usajili wa pesa nyingi kuzidi nyingine katika harakati za kubeba wakali wapya.
Na sasa Liverpool inatishia uwezekano wa kuvuka Pauni 500 milioni kwenye usajili wa dirisha moja. Hilo litatokea kama itafanikiwa kunasa saini ya Alexander Isak.
Lakini, je timu gani inayoshika namba moja kwenye 10 bora ya klabu zilizotumia pesa nyingi kusajili mastaa wapya ndani ya dirisha moja? Utamu wote upo hapa.
10. Real Madrid – Pauni 218 milioni, 2009-10
Katika dirisha la majira ya kiangazi 2009/2010, Real Madrid ilionyesha jeuri ya pesa wakati rais wake Florentino Perez alifungua pochi kunasa mastaa wa maana katika Galactico ya awali ya pili. Mastaa Cristiano Ronaldo, Kaka, Karim Benzema na Xabi Alonso wote walinaswa kwenye dirisha hilo, huku Ronaldo peke yake aligharimu Pauni 80 milioni, ambayo ilivunja rekodi ya uhamisho wakati huo. Kaka alinaswa kwa Pauni 68.5 milioni na alienda kuchagua mabao 61 katika mechi 120. Ronaldo alifunga mabao 450.
9. Juventus – Pauni 223milioni, 2018-19
Juventus si timu inayotaka kutumia pesa nyingi sana kwenye usajili, lakini Cristiano Ronaldo alikwenda kubadili hilo kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2018/2019. Miamba hiyo ya Italia, ilitumia Pauni 100 milioni kunasa saini ya Ronaldo, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 33 na walifanya hivyo wakiwa na matumaini ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitu ambacho hakikutokea. Joao Cancelo naye alinaswa kwa pesa nyingi, huku ikimrudisha pia Leonardo Bonucci kwenye kikosi. Ronaldo alifunga sana.
8. Barcelona – Pauni 235milioni, 2019-20
Kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi 2019/2020, Barcelona ilifanya matumizi makubwa sana kwenye usajili na jambo hilo liliwaingia kwenye tatizo kubwa ambalo lilikuja kuweka bayana kiuchumi. Miamba hiyo ya Nou Camp, kwanza ilimnasa Antoine Griezmann kwa mkwanja wa Pauni 107 milioni, kisha ikamchukua kiungo Frenkie de Jong kwa Pauni 65 milioni. Sambamba na hilo, kulikuwa na wachezaji wengine pia Neto, Pedri na Junior Firpo kwa kuwataja kwa uchache. Mpango ulikuwa kuijenga Barca kumzunguka Lionel Messi.
7. Chelsea – Pauni 254milioni, 2022-23
Bilionea mmiliki mpya wa Chelsea, Todd Boehly hakutaka kabisa kupoteza muda kwenye ishu ya kufungulia pochi lake baada ya kutua Stamford Bridge, ambapo kwenye dirisha lake la kwanza la majira ya kiangazi, alitumia pesa ndefu kwelikweli. Katika dirisha hilo, Chelsea ilitumia zaidi ya Pauni 250 milioni kunasa huduma za mastaa kama Raheem Sterling, Wesley Fofana, Kalidou Koulibaly, Marc Cucurella na Pierre-Emerick Aubameyang. Usajili huo haukuwa na faida yoyote kwa Chelsea na kumsababishia kocha Thomas Tuchel akifukuzwa kazi.
6. Liverpool – Pauni 263.5milioni, 2025-26
Liverpool bado haijafunga hesabu za usajili kwenye dirisha hili la uhamisho w amajira ya kiangazi, lakini tayari imeshaingia kwenye orodha ya timu zilizotumia pesa nyingi kusajili ndani ya dirisha moja. Kiwango walichotumia hadi sasa ni Pauni 263.5 milioni na inaweza kufikia Pauni 400 milioni kama si kuikaribia kabisa Pauni 500 milioni ukijumlisha na bonasi kwenye dili. Imemsajili Florian Wirtz kwa pesa inayozidi Pauni 110 milioni, lakini pia imetumia pesa nyingi kuwanasa Hugo Ekitike, Jeremie Frimpong, Milos Kerkez na Giorgi Mamardashvili.
5. Chelsea – Pauni 278milioni, 2022-23
Kwenye dirisha la majira ya baridi 2022-23, Chelsea ilionyesha jeuri ya kutumia pesa nyingi katika usajili wa Januari. Mara nyingi, pesa nyingi zimekuwa zikitumika kwenye usajili wa madirisha ya majira ya kiangazi, lakini Chelsea ilionyesha kwamba hata Januari, inaweza kufanya matumizi ya kibabe. Katika dirisha hilo, ilivunja rekodi ya uhamisho Uingereza kwa kumsajili Enzo Fernandez kwa Pauni 107 milioni. Katika dirisha hilo, iliwanasa pia Mykhalo Mudryk, Noni Madueke, Benoit Badiashile na mastaa wengine kadhaa huko Stamford Bridge.
4. Real Madrid – Pauni 279milioni, 2019-20
Kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2019-20, Real Madrid ilikuwa inafanya usajili wa kuimarisha kikosi chake na kukifanya kuwa matata kabisa, jambo ambalo halikuwa na mwisho mzuri. Staa wa Kibelgiji, Eden Hazard aliwasili kwenye kikosi hicho kwa uhamisho wa pesa nyingi na ilionekana kama anakwenda kuziba pengo la Ronaldo, kitu ambacho kilishindwa kutokea na Luka Jovic, naye aliyenaswa dirisha hilo hakuwa na mambo mazuri. Iliwanasa pia Ferland Mendy, Eder Militao na Rodrygo. Hili ni dirisha ambalo Madrid ilitumia pesa nyingi zaidi.
3. PSG – Pauni 295milioni, 2023-24
Kwa miaka mingi, Paris Saint-Germain imekuwa ikihusishwa na mastaa wote wa maana. Mwaka 2023, ilifanikiwa kuwanasa mastaa hao, ambapo ilifungua pochi kunasa wakali wa maana kuwaleta kwenye kikosi chao. Iliwasajili Randal Kolo Muani kwa ada ya Pauni 80 milioni, Ousmane Dembele kutoka Barcelona, Manuel Ugarte kutoka Sporting na Lucas Hernandez kutoka Bayern Munich. Kiwango kilichotumika kilikaribia kabisa Pauni 300 milioni, ambayo ni kama pesa tu ya mfuko wa shati kwa timu hiyo inamilikiwa na Qatar Sports Investments.
2. Al-Hilal – Pauni 298milioni, 2023-24
Saudi Pro League imekuwa gumzo kubwa inapofika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi kwa miaka ya karibuni na Al-Hilal ni moja ya timu zilizotumia pesa nyingi sana kwenye kunasa mastaa wapya. Ilimsajili Neymar kwa ada ya Pauni 78 milioni, huku ikiwanasa pia Aleksandar Mitrovic, Sergej Milinkovic-Savic, Ruben Neves na Kalidou Koulibaly. Hakuna mchezaji mmoja aliyevunja rekodi ya dunia kwenye usajili huo, lakini kwa pamoja wameigharimu pia hiyo pesa nyingi. Pauni 300 milioni zilizotumika na kuifanya Saudia kuwa na ligi bora.
1. Chelsea – Pauni 391milioni, 2023-24
Chelsea tena kwenye orodha hii na safari hii ikishika namba moja kwa kufanya matumizi makubwa kwenye usajili wa dirisha moja. Bilionea Boehly aliendelea kufungua pochi lake na kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2023/2024, miamba hiyo ya Stamford Bridge, ilivuka matumaini ya Pauni 390 milioni ya usajili kwenye dirisha moja. Chelsea ilifanya usajili wa mastaa 11 wa thamani ya Pauni 10 milioni, huku sita wakigharimu zaidi ya Pauni 30 milioni. Moises Caicedo alivunja rekodi ya Uingereza aliponaswa kwa Pauni 115 milioni, huku wakali wengine walionaswa kwa pesa nyingi ni Romeo Lavia, Christopher Nkunku, Axel Disasi na Cole Palmer.