Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kioo kitamdanganya Cristiano Ronaldo mpaka lini?

Muktasari:

  • Alitua akiwa mchanga kama alivyo. Sura yake nzuri isingekupumbaza. Miguu yake ilikuwa inachanganya kwa haraka. Uzuri ni kwamba miguu yake na ubongo wake vilikuwa vinahafikiana. Vilikuwa pacha.

CRISTIANO Ronaldo dos Santos Aveiro kila siku anasimama mbele ya kioo chake. Anajitazama. Anajipenda. Anajikubali. Hatuelewi. Anajiona ni yule yule aliyetua uwanja wa ndege wa Manchester Juni 2003 akitokea uwanja wa ndege wa Humberto Delgado pale Lisbon.

Alitua akiwa mchanga kama alivyo. Sura yake nzuri isingekupumbaza. Miguu yake ilikuwa inachanganya kwa haraka. Uzuri ni kwamba miguu yake na ubongo wake vilikuwa vinahafikiana. Vilikuwa pacha.

Jumatano mchana kwa saa za Houston Marekani huku Afrika Mashariki ikiwa ni usiku Ronaldo alikuwa hana madhara mbele ya mabeki wa kati wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Steve Kapuadi na Axel Tuanzebe. Nyakati zimekwenda wapi?

Miaka kadhaa nyuma Ronaldo angewatekeza. Jaribu kuwakumbuka mabeki ambao waliwahi kuteketezwa na Ronaldo. Miamba na miamba. Leo alikuwa akidhibitiwa na Tuanzebe na kapuadi. Hapana, nimekosea, alikuwa anajidhibiti mwenyewe. Wala hawakutumia juhudi kubwa kumdhibiti.

Nini kinatokea kwa Ronaldo? Siwezi kusema ni mbinafsi. Hapana. Anatushangaa sisi ambao tunamshangaa. Kuna wanadamu wapo kama yeye. Haoni kama ana tatizo lolote na anachokifanya. Zaidi ya kila kitu ana njaa. Ana njaa ile ile ya kucheza mpira ambao haijaondolewa katika mwili wake na kitu chochote kile.

Hata pesa ambazo anamiliki hazijamuondolea njaa aliyonayo. Kutoka katika umaskini kule Madeira alikokulia mpaka leo, Ronaldo anamiliki ndege yake binafsi anayomiliki ambayo thamani yake ni dola 75 milioni. Ndege aina ya Bombardier Global Express XRS.

Ana boti yake ya kifahari (Yatch) aliyonunua dola milioni 7. Inaitwa Azimut Grande 27 Metri. Ana hoteli tano katika miji tofauti duniani. Hoteli anazomiliki kwa pamoja na kampuni ya Pestana. Zipo miji ya New York, Madrid, Marrakech, Lisbon na kwao Madeira.

Yote haya hayajamuondolewa Ronaldo njaa ya kucheza mpira. Ana kiu. Kiu ambacho kinawatesa makocha wengi wa timu ya taifa ya Ureno. Ronaldo anataka kucheza. Ronaldo ni nahodha wa Ureno. Ronaldo ni alama ya Ureno. Ronaldo kando ya Messi ni alama ya mpira kwa vijana wa kizazi kipya.

Kocha wa Ureno, Roberto Martinez anawezaje kumuita Ronaldo katika chumba chake na kumwambia kwamba hatacheza pambano lake la kwanza la kombe la dunia mwaka 2026. Kocha aliyepita, Fernando Santos alijaribu lakini mpaka leo haongei na Ronaldo.

Hatujawahi kuvaa viatu vya Martinez. Inahitajika roho ngumu. Erik Ten Hag ndiye mwanaume ambaye alijaribu zaidi. Ronaldo akaishia kumnunia na kuongea mbovu katika mahojiano yake na mwandishi rafiki yake, Piers Morgan.

Ronaldo hataki kuanzia benchi, Ronaldo hataki kutolewa wakati mechi ikiendelea. Ronaldo anajiona yule yule tu. Anajiona Ronaldo wa mwaka 2003. Anajiona Ronaldo wa mwaka 2009. Anajiona Ronaldo wa mwaka 2014. Anajiona Ronaldo wa mwaka 2019. Mpaka leo ameendelea kujiona yule yule tu.

Sisi ndio ambao tunajua kwamba Ronaldo amechoka. Zamani wakati akiwa ameanza kuchoka alihamia kucheza kama mshambuliaji wa kati. Aliendelea kucheza vizuri. Sasa hivi hata hiyo nafasi ya mshambuliaji wa kati haitendei haki. Amechoka.

Hajihangaishi sana pale mbele. Kwa mujibu wa rekodi zake katika pambano dhidi ya Congo ni kwamba hakufunga bao, hakupiga pasi ya bao, hakupiga shuti lililolenga lango, hakuweza kukamilisha kukokota mpira wowote ule, hakutengeneza nafasi, hakupiga pasi muhimu.

Tatizo kila akirudi katika chumba chake anasimama mbele ya kioo na kujiona ni yule yule tu. Anampa wakati mgumu Martinez. Wanahitajika makocha kama Jose Mourinho au Pep Guardiola kumuweka nje katika kikosi cha Ureno.

Wakati mwingine makocha hawa wangeenda mbali zaidi na huenda wasingemuita katika kikosi. Hata hivyo Ronaldo anataka sio tu kuitwa bali pia kucheza. Na sio tu kucheza bali vile vile asitolewe uwanjani.

Martinez angewezaje kumuweka nje Ronaldo katika pambano dhidi ya Congo wakati jana yake tu hasimu wake Messi alikuwa amepiga hat trick katika pambano dhidi ya Algeria. Ingekuwa vita kubwa kwa Martinez.

Jumanne Wareno watarudi uwanjani kucheza na Uzbekistan. Tutaona kama Martinez atakuwa na nguvu ya kumrudisha uwanjani. Sijui. Labda. Kama akimrudisha atakuwa haitendei timu ya taifa ya Ureno.

Nimewasikiliza wachambuzi wengi wa nje wote wanakubaliana katika kile ambacho mashabiki wanakiona. Kwamba Ureno huwa ni kama inacheza pungufu pindi wanapompanga Ronaldo wa leo. Ni ukweli unaouma.

Tofauti ya yeye na hasimu wake Messi ni moja. Wote wawili wamechoka lakini Ureno inaweka nje vipaji vingi kwa ajili ya kuhakikisha Ronaldo anacheza. Kule Argentina Messi hajazungukwa na vipaji vingi ambavyo unaweza kusema kwamba vinakatiliwa kwa Messi kucheza.

Kule Ureno akina Joao Felix, Concalo Ramos na wengineo ambao damu zao ni changa wanakaa nje kwa ajili ya kumpisha Ronaldo acheze. Na sio kucheza tu, inabidi acheze dakika zote kwa sababu akitolewa atanuna. Aliwezaje kumaliza dakika zote 90 na za nyongeza katika pambano dhidi ya Congo? Ni swali ambalo wengi tumejiuliza. Kwa jambo gani hasa ambalo alifanya uwanjani?

Binafsi nalitazama jambo hili katika pande mbili. Kwanza nataka kumuona Ronaldo ni mbinafsi. Labda angejitafakari na kuwapunguzia mzigo makocha. Lakini hapo hapo nashangazwa na kiu yake iliyopitiliza ya kupenda kucheza.

Anamiliki karibu kila kitu ambacho sisi wengine huwa tunavipata ndotoni tu. Bado Ronaldo anataka kucheza tena na tena. Sio kwa sababu ya pesa, Hapana, anapenda tu kucheza. Na hata anapojitazama katika kioo chake huwa anajiona yeye ni yule yule tu.