Kina nani wanalipwa zaidi NBA msimu huu?
Muktasari:
- NBA kwa sasa inapitia kipindi cha mafanikio makubwa kifedha, ambapo mikataba mipya ya haki za matangazo ya televisheni, ukuaji wa ligi hiyo duniani na kuendelea kupanda kwa viwango vya mishahara vimechochea ongezeko kubwa la thamani ya mikataba ya wachezaji.
WASHINGTON, MAREKANI: ONGEZEKO kubwa la kifedha katika Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA), limeifanya mishahara ya nyota wakubwa kufikia viwango ambavyo ingekuwa vigumu kufikirika miaka 10 iliyopita.
NBA kwa sasa inapitia kipindi cha mafanikio makubwa kifedha, ambapo mikataba mipya ya haki za matangazo ya televisheni, ukuaji wa ligi hiyo duniani na kuendelea kupanda kwa viwango vya mishahara vimechochea ongezeko kubwa la thamani ya mikataba ya wachezaji.
Zamani, kulipwa zaidi ya Dola 30 milioni (takriban Sh79.4 bilioni) kwa msimu ilikuwa ni kwa wachezaji wachache, lakini hivi sasa kuna mastaa kibao wanaolipwa karibu Dola 60 milioni (zaidi ya Sh158.5 bilioni) au zaidi kwa mwaka. Hawa hapa ni wachezaji 10 wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi NBA mwaka huu wa 2026.
10. Jimmy Butler (Sh150.4 bilioni)
Akiwa na umri wa miaka 37, mshambuliaji wa Golden State Warriors, Jimmy Butler, anafunga orodha ya wachezaji 10 wanaolipwa zaidi NBA baada ya kusaini mkataba mkubwa wa kuongeza muda wa kuitumikia timu hiyo, unaomuweka miongoni mwa wachezaji wenye mishahara mikubwa zaidi kwenye ligi.
Kuwasili kwake Golden State kumeimarisha matarajio ya timu hiyo ya kutwaa ubingwa na kuongeza uzoefu katika kikosi kilichozoea kushindania mataji. Kabla ya kupata jeraha kubwa la goti hivi karibuni, Butler alikuwa akionyesha kiwango kizuri na kuendelea kuwa mchezaji muhimu katika safu zote mbili za uwanja, ushambuliaji na ulinzi.
9. Karl-Anthony Towns (Sh151.1 bilioni)
Karl-Anthony Towns anaendelea kuwa miongoni mwa wachezaji wenye mikataba mikubwa zaidi NBA, hadhi ya kifedha inayotarajiwa kuendelea kuwepo akiwa New York. Kwa sasa anafanya mazungumzo kuhusu mustakabali wake na New Knicks, huku dalili zikionyesha kuwa hatimaye atasaini mkataba mwingine wa mamilioni ya fedha utakaomuweka miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi kwenye ligi hiyo.
Thamani yake kubwa ya kimkataba inaakisi uwezo wake wa kubadilisha namna nafasi ya mchezaji wa kati (center) inavyotumika katika mchezo wa kisasa wa mpira wa kikapu. Uwezo wake wa kufunga, hasa tishio lake kubwa la mitupo ya mipira ya pointi tatu, unamfanya kuwa mchezaji wa kipekee na mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi.
8. Devin Booker (Sh151.1 bilioni)
Akiwa na umri wa miaka 29, Devin Booker amejiimarisha kama tegemeo la ushambuliaji la Phoenix Suns na mmoja wa wachezaji wanaocheza nafasi ya shooting guard wenye uwezo mkubwa zaidi kiufundi na waliokamilika NBA.
Uwezo wake wa kufunga akiwa nje ya eneo la karibu na kikapu pamoja na mipira ya umbali wa kati unamfanya kuwa mmoja wa mastaa wanaotegemewa zaidi kwenye timu yake.
Mustakabali wake wa kifedha pia uko salama, kutokana na mikataba yenye thamani kubwa zaidi inayomsubiri katika misimu ijayo, ambayo inatarajiwa kumpandisha zaidi katika orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa NBA.
7. Jaylen Brown (Sh151.1 bilioni)
Mchezaji aliyekuwa MVP wa Fainali za NBA 2024, Jaylen Brown, anaendelea kunufaika na mkataba miongoni mwa mikataba yenye thamani kubwa zaidi kuwahi kusainiwa, akiendeleza hadhi ya kifedha katika maisha yake ya kikapu akiwa na Philadelphia 76ers.
Baada ya kuondoka kwa kushtukiza Boston Celrics ambako aliunda moja ya safu hatari zaidi za ushambuliaji katika ligi akiwa pamoja na Jayson Tatum, Brown sasa anakabiliwa na changamoto mpya Philadelphia akiwa tayari ni nyota mkubwa.
Maendeleo yake makubwa katika ushambuliaji na ulinzi katika misimu ya hivi karibuni aliyoyapata akiwa katika moja ya masoko yenye ushindani mkubwa kwenye ligi, ndiyo hasa ambayo Sixers wanatarajia kunufaika nayo wanapolenga kupambana kwa dhati kuwania ubingwa.
6. Joel Embiid (Sh153.5 bilioni)
Mshindi wa tuzo ya MVP 2023, Joel Embiid, bado ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo wa kutawala mchezo kutokana na mchanganyiko wa ukubwa wa mwili, ufundi na uwezo wa kufunga. Ingawa majeraha yameathiri misimu yake ya karibuni, mchezaji huyo wa nafasi ya center kutoka Cameroon anaendelea kulipwa mshahara unaolingana na hadhi yake ya nyota mkubwa kila anapopata nafasi ya kucheza akiwa fiti.
Bado ndiye tumaini kubwa zaidi la Philadelphia katika harakati za kutwaa ubingwa, jambo ambalo klabu hiyo imekuwa ikilifukuzia kwa miongo kadhaa.
5. Antetokounmpo (Sh154.7 bilioni)
Giannis Antetokounmpo, nyota kutoka Ugiriki ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi NBA na anaendelea kuwa sehemu ya wachezaji bora kabisa katika ligi hiyo. Akiwa bingwa na mshindi mara mbili wa tuzo ya MVP,
Antetokounmpo amejenga mafanikio kwa kuendelea kuwa bora, kufanya kazi kwa bidii na kuwa na mchango mkubwa katika pande zote mbili za uwanja, ushambuliaji na ulinzi. Mambo hayo yote yanahalalisha nafasi yake miongoni mwa wachezaji wenye mikataba mikubwa zaidi kwenye ligi.
Kuwasili kwake Miami Heat kumeibua msisimko mkubwa, huku klabu hiyo ikiendelea kujenga kikosi kipya kitakachoshindania ubingwa kikimzunguka mmoja wa wachezaji waliotawala zaidi mchezo huo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
4. Anthony Davis (Sh154.4 bilioni)
Ni vigumu kupata wachezaji wa nafasi ya center wanaoweza kuchanganya kiwango cha juu cha ulinzi na ushambuliaji kama Anthony Davis wa Washington Wizards, sifa inayomuweka miongoni mwa wachezaji wenye vipaji na thamani kubwa zaidi katika mchezo wa mpira wa kikapu duniani.
Uwepo wake unaweza kubadilisha matokeo ya mchezo kupitia uwezo wake wa kuzuia, kudaka mipira inayorudi kutoka kwenye kikapu (ribaundi) na kufunga.
Ingawa maisha yake ya kikapu yamepitia mabadiliko kadhaa katika misimu ya karibuni ikiwemo kuhama timu na kukabiliwa na matatizo ya mara kwa mara ya kimwili yaliyoathiri upatikanaji wake uwanjani, hadhi yake haijabadilika. Bado ni mchezaji wa kiwango cha juu anayestahili mshahara unaolingana na hadhi yake ya nyota mkubwa.
3. Jayson Tatum (Sh154.4 bilioni)
Jayson Tatum ndiye mhimili wa sasa na mustakabali wa Boston Celtics, akiwa mchezaji asiye na mpinzani katika moja ya klabu zenye historia kubwa zaidi katika michezo Marekani.
Akiwa bingwa wa NBA na miongoni mwa wachezaji wanaowania mara kwa mara tuzo ya MVP, mshambuliaji huyo anahalalisha uwekezaji mkubwa wa Boston kupitia kiwango chake cha kutegemewa, uwezo wa kufunga na uongozi wake ndani ya timu.
Baada ya kupona jeraha kubwa, anaingia katika msimu mpya akiwa na matarajio ya kuwania tena tuzo kubwa binafsi, huku klabu yake ikiendelea kumuamini kwa kumpa mkataba wenye thamani kubwa ambao unaweza kuongezeka zaidi katika miaka ijayo.
2. Nikola Jokic (Sh156 bilioni)
Nyota kutoka Serbia anayekipiga Denver Nuggets, Nikola Jokic, amebadilisha kwa kiasi kikubwa namna nafasi ya center inavyochezwa kupitia uwezo wake wa kuona na kusoma mchezo, kutengeneza nafasi za kufunga, kufunga na kuwafanya wachezaji wenzake kuwa bora kwa namna ambayo siyo rahisi kuonekana kwa mchezaji mwenye ukubwa wa mwili kama wake.
Kiwango chake kikichangiwa na kutwaa tuzo tatu za MVP pamoja na ubingwa wa NBA kimemjengea historia ya mafanikio miongoni mwa wachezaji bora zaidi wa karne hii na kumfanya kuwa mmoja wa vipaji vya kipekee kuwahi kuonekana katika NBA.
Kadiri mapato yake yanavyoendelea kuongezeka, gwiji huyo wa Denver anatarajiwa kuendelea kubaki na timu hiyo kwa miaka mingi ijayo.
1. Stephen Curry (Sh165.4 bilioni)
Stephen Curry bado ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi NBA, akiongoza orodha hiyo kwa msimu wa pili mfululizo.
Akiwa na umri wa miaka 38, mchezaji huyo wa nafasi ya point guard siyo sehemu muhimu tu ya muundo wa kimichezo na kifedha wa Golden State Warriors, bali pia ushawishi wake unajulikana nje ya uwanja.
Anatambulika kwa kiasi kikubwa kuwa mtupaji bora zaidi wa mipira ya mbali kuwahi kutokea baada ya kubadilisha namna mchezo wa kisasa wa mpira wa kikapu unavyochezwa kupitia usahihi wa kipekee wa kurusha mipira akiwa umbali mrefu.
Akiwa ametwaa mataji manne ya NBA na tuzo mbili za MVP, historia yake ya mafanikio imesaidia kuibadilisha Warriors na kuifanya kuwa moja ya klabu zenye thamani kubwa zaidi katika michezo ya kulipwa.