Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIJIWE CHA SALIM SAIDI SALIM: Magwiji wa kriketi na magari walioacha rekodi

SIKU hizi kila napotembelea baadhi ya viwanja vya michezo sehemu mbalimbali za mikoa ya Bara hujikumbusha mabadiliko makubwa yaliyofanyika nchi hii katika medani ya michezo.
Kabla na miaka michache baada ya uhuru baadhi ya michezo Tanganyika ilionekana kama ya watu wa kabila au tabaka fulani, tofauti na ilivyokuwa Zanzibar.
Miongoni mwa michezo ilionekana Bara kuwa ni ya kina fulani na sio yetu ni mpira wa magongo, kriketi, gofu, tenisi na hata vishale (darts).
Wachezaji karibu wote walikuwa Wazungu na Wahindi (hasa Magoa na Masingasinga) wakati Zanzibar ilikuwa mchanganyiko wa mchafukoje. Mpira wa magongo ulichukua sura mpya Bara mwanzoni mwa miaka 1970 pale vijana wa Zanzibar waliohamia Dar es Salaam walipounda timu iliyoitwa Bantus.
Timu hii ilikuwa bingwa wa mchezo huu Bara na Viswani na kung’ara Afrika Mashariki kwa muda mrefu mpaka baadhi ya wachezaji walipostaafu kutokana na umri mkubwa na wengine kwenda nchi za Ghuba kutafuta maisha bora.
Timu zilizotamba wakati ule katika kriketi ni Sikh Union, Goan Institute (baadaye Dar Institute) na Gymkhana. Jeshi nayo iliunda timu ya mpira wa magongo kwa msaada wa wachezaji kutoka Zanzibar na kufanya vizuri na baadaye zilichomoza timu za Arusha Twiga na Tanga Institute.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Magongo Tanzania (THA), Tarlochan Singh Sandhu alifanya juhudi kubwa za kuupeleka mchezo huu shuleni, lakini mafanikio hayakuwa mazuri.
Hivi sasa mchezo huo umefifia jeshini na katika klabu mbalimbali, lakini zimechomoza timu za vijana pamoja na katika baadhi ya shule kuupenda mchezo huu.

Baada ya wachezaji wa Bantu kupumzika kutokana na umri mkubwa na wengine kuondoka nchini klabu hiyo nayo ikatoweka na kuwa sehemu ya historia ya mchezo wa mpira wa hoki nchini.
Kriketi nayo ilichezwa sana na Wahindi wa makabila yote na Wazungu wa klabu za Gymkhana. Waafrika waliojitokeza kucheza kriketi walikuwa wachache hadi mwishoni mwa miaka ya 1980 walipohamia Dar es Salaam vijana wengi wa Zanzibar.
Mchezo wa kriketi ulikuwa na uongozi mzuri na kuweza kualika timu za nchi jirani, India na Uingereza. Wachezaji kadhaa wa Tanzania walijitokeza kuwa na ustadi mkubwa. Miongoni mwao ni Visant Tapu na Pranlal Divecha. Wote wawili walishawishiwa kwenda Uingereza kuchezea klabu za huko kwa miaka mingi. Miongoni mwa watu walioutumikia sana mchezo huu nchini ni daktari maarufu wa meno, Kulbir Gupta.

Timu ya taifa ya kriketi ya Tanzania ilichukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mara nyingi na kwa ujumla ilikuwa tishio kusini mwa Jangwa la Sahara.
Michezo ya mpira wa wavu na wa mikono haikuwepo nchini hadi mwanzoni mwa miaka ya 1970 na ni katika miaka ya klabuni ndio kasi ya kupendwa imekuwa kubwa.

Mashindano ya mbio za magari yaliwavutia sana Watanzania. Kila yalipofanyika palikuwepo mvuto wa aina yake hasa kwa mashindano ya East African Safari na Tanganyika 1000. Miongoni mwa wawakilishi wa Tanzania walioiletea sifa nchi hii ni Waingereza waliokuwa wakifanya kazi kampuni ya magari ya Tanganyika Motors, Bert Shankland na mwenzake Chris Bates.
Majina yao yalikuwa maarufu katika masikio ya Watanzania miaka ya 1960 hadi 1970 kutokana na kuwashinda waendeshaji magari maarufu duniani kama Joginder Singh wa Kenya na wengine kutoka Finland, Ujerumani na Uingereza. Mwaka 1968 wakati wa Pasaka nikiwa mwandishi wa Daily News nilikwenda Milima ya Usambara na mpigapicha maarufu Ardash Nayar kusubiri magari kufika eneo hilo.

Tulitegesha pale Mlalo ambapo lilikuwepo dimbwi la maji na matope kwenye masafa kama robo kilomita. Hapo tulipata habari na picha nzuri kwa ajili ya gazeti.
Tulifika katika Milima ya Usabara Jumatatu alfajiri baada ya kulala Tanga na magari yalifika eneo hilo lililojaa matope saa sita mchana. Dereva wa kwanza kuchomoza alikuwa Bert Shankland na alipomaliza kupita sehemu hiyo iliyokuwa na matope mengi mpira mmoja wa gari yake ya nyeupe ya Peugeot 404, namba TDN 5 ulipasuka.

Sitasahau kasi iliyotumika kufungua mpira uliopasuka na kuweka wa akiba. Haikuchukua zaidi ya dakika tatu, lakini wakati wakimalizia kufunga zilichomoza gari nne, ya mbele ikiwa ya Joginder Singh. Shankland aliondoka akiwa wa tano na kuelekea Mombo na baadaye Korogwe kwa hatua ya mwisho ya kuelekea Dar es Salaam.

Mara baada ya hizo gari kupita tuliingia katika gari letu la aina ya Land Rover kuelekea Korogwe. Tulipofika huko tuliambiwa Shankland alifika hapo akiwa wa pili, dakika kama mbili baada ya kupita Joginder Singh. Safari yao ilikuwa kueleka Ubena Zamozi na Morogoro na baadaye hatua ya mwisho ya mbio hizi za siku nne kwenda Dar es Salaam.
Taarifa tuliyoipata usiku wa manane ilieleza kuwa Shankland alikuwa wa kwanza kufika Morogoro na kumuacha Joginder Suingh kama mita 100 nyuma. Siku ya pili asubuhi Shankland na Bates waliugusa utepe mwanzo Hoteli ya Kilimanjaro na Singh alikuwa wa pili dakika nne nyuma. Mashindano ya mwaka ule yalivutia sana na kufanyiwa filamu maalumu.

Bert Shankland ambaye ushindi wake wa mbio za East African Safari Rally mara mbili 1966 na 1967 na katika mashindano ya mbio ya magari za kimataifa uliipatia umaarufu Tanzania na kusaidia kuutangaza utalii. Shakland ambaye alikuwa meneja wa kampuni ya magari ya Tanganyika Motors alifanya kazi Tanzania tangu 1950 hadi mwishoni mwa miaka ya 1970 aliporudi kwao Scotland kwa mapumziko.

Aliiaga dunia Januari 2012 akiwa na miaka 80 na mazishi yake yaliyofanyika kijiji alichozaliwa cha Perth, Scotland yalihudhuriwa na Watanzania wengi waliopo Uingereza wakiwemo wa ofisi yetu ya ubalozi. Hadi leo picha ya Shankland na Berth zinapamba kumbi za klabu nyingi za michezo na ofisi za Tanganyika Motors hapa nchini.