KIJIWE CHA SALIM: Jamatini alipoingia golo
Muktasari:
- Machi, 1971 nilikwenda Moshi nikitokea Arusha nilikokuwa ninafanya kazi kama mwandishi wa magazeti ya Standard (sasa Daily News) kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) ambayo wakati ule ilikuwa porini.
KILA ninapofika Moshi yapo mambo yanayonikumbusha visa na mikasa nilivyokutana navyo kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Machi, 1971 nilikwenda Moshi nikitokea Arusha nilikokuwa ninafanya kazi kama mwandishi wa magazeti ya Standard (sasa Daily News) kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) ambayo wakati ule ilikuwa porini.
Baada ya kutuma habari Dar es Salaam kwa telex nilipumzika kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU) iliopo katikati ya Mji wa Moshi.
Nikiwa nimepumzika jioni, mlango iligongwa na nilipouliza nani nikasikia kicheko cha watu niliowafahamu na kufanya nao kazi Arusha, Patrick Makomu wa magazeti ya Uhuru na Nationalist na marehemu Richard Msaky wa Idara ya Habari.
Kilichowaleta kilinishangaza kwa vile waliniuliza sisi watu wa Zanzibar ni wa aina gani. Sikuwafahamu na nilipowahoji kwa nini waliuliza swali lile, ndipo nilipata mshangao.
Msaky aliniambia timu ya mpira wa magongo (hockey) kutoka Zanzibar kwa mashindano yaliyojumuisha timu za Tanzania, Kenya na Uganda yaliyokuwa yanafanyika Moshi ilikuwa sio ya kawaida.
Tofauti yake ni kuwa na sura tafauti na za timu nyingine za Dar es Salaam, Arusha, Moshi, Tanga na Mombasa zilizokuwa katika mashindano hayo.
Tofauti waliyoigundua wao ni timu ya Zanzibar haikuwa na Wahindi, Wazungu wala Magoa bali ni Waswahili na watu waliochanganya damu za Kiarabu na Ngazija (Comoro). Niliwaeleza hiyo ndiyo Zanzibar na ndiyo maana walikuwa wakiniona baadhi, wakati nilipokuwa Arusha nikicheza kriketi na gofu. Baadaye nilikuja kugundua sio Msaky na Makomu tu walioshangazwa.
Siku ya pili yake watu wengi walifika uwanjani sio kuangalia mashindano hasa, bali kuona Waswahili walivyokuwa wanaumudu mchezo wa magongo na kilichowavutia ni kuona timu ni ya Zanzibar.
Ilikuwa na mchanganyiko wa wachezaji wa rika tofauti, akiwemo kijana wa miaka 16, Islam Ahmed Islam na wenye umri wa zaidi ya miaka 40 kama Abdul Majham na Maulidi Machaprala. Wote hawa waliiaga dunia nyakati tofauti katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Wengine ninaowakumbuka katika msafara ule ni marehemu Zaghalul Ajmi na ndugu yake, Ahmed Himidi Mbaye na kaka yake Babechi, marehemu Abdulla Pakistani na Ahmed Juma.
Hali ile ilinikumbusha nilipofika Dar es Salaam nilipopewa uhamisho na Daily News kutoka Zanzibar mwaka 1966. Nilipambana na mkasa unaotoa tafsiri sahihi ya ule msemo wa Waswahili wa 'Jamatini kaingia Golo'.
Wakati ule alikuwepo jamaa mmoja wa asili ya Goa (India), akitumia jina la utani la 'Flotsam' na daktari wa meno wa hospitali ya Agakhan, Gupta (Singa Singa) wakiandika habari za kriketi, gofu na mpira wa magongo. Wote walikuwa na dharura. Flotsam alikuwa safarini na Gupta asingeweza kuandika kwa vile alikuwa anacheza siku ile. Baada ya majadiliano ya kutafuta atayeandika habari za mchezo mkubwa wa kriketi uliokuwa unafanyika siku ile kwenye uwanja wa Kinondoni nikawaeleza nilikuwa tayari kuandika habari zake.
Wahariri wazungu na waandishi wenzangu walionekana kushangaa na kudhani ninafanya masihara na wakaniambia tutasubiri hiyo ripoti yako ili kujua kama kweli unaijua michezo hii.
Mwandishi mwandamizi, marehemu Nsubisi Mwakipunda alicheka na kuniambia 'acha utani'.
Nilipofika Kinondoni na kwenda kwenye banda la wachezaji na waamuzi ndipo ikawa ile hadithi ya Jamatini kaingia Golo.
Watazamaji na wachezaji walishangaa kuniona na kitabu natafuta maelezo ya wachezaji na mashindano kabla ya mchezo. Waliona kama nilikuwa natania.
Kiongozi mmoja wa kriketi akaniambia isingewezekana kwa vile mchezo wa kriketi ni tofauti na soka. Nilitabasamu tu na kumweleza sio nilikuwa ninajua kuandika habari za kriketi tu, bali nilikuwa ninaucheza.
Nilimwambia habari za wachezaji maarufu duniani kwa wakati ule kama Sir Gary Sobers wa Carribean na Pataudi wa India mbali ya wachezaji maarufu wa Zanzibar kama Sherali Ndege na hata historia maarufu ya Ashes ya mchezo huo.
Mmoja wa watoto wa marehemu Sherally alikuwepo na rafiki zake Bashir Tejani, Mohammed Nathoo na Sajjad Lakha (mtoto wa wakili Lakha) kutoka Zanzibar ambao walikuwa wachezaji wa timu ya Ithnaasheri (Union) siku ile.
Mwanamichezo maarufu wa visiwani, Said Nyanya ambaye alikuwa anauza duka katika kona ya mitaa ya Zanziki na Libya, karibu na makao makuu ya Jukwaa la Wahariri (TEF) ambaye alikuwa kiongozi wa Union pia alikuwepo.
Sherally aliwaeleza niliokuwa nawadadisi ilikuwa sio ajabu kuona ninaelewa mchezo huo, kwa sababu shule nyingi za Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya 1964 zilikuwa na timu za kriketi.
Vile vile tulikuwa tunacheza gofu, mchezo ambao nyota wake Unguja walikuwa wana familia ya Burhani Sadat aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Zanzibar aliyeaga dunia mapema mwaka huu.
Wahindi wa Zanzibar wa wakati ule nao walikuwa wanacheza bao na hata kuwinda ndege na njiwa kwa manati, tofauti na hali ilivyo Bara.
Niliwambia wale jamaa wa Kihindi kutoka Zanzibar, kufika kwangu pale kuandika habari za kriketi ilikuwa ni ile hadithi ya Jamatini kaingia golo. Maana ya golo ni mtu mwenye mchanyiko wa damu wa Mhindi na kabila nyingine.
Walicheka na Nathoo akatia mkono mfukoni, akanipa tambuu na kuniambia nikitafuna hawataniona ni Golo. Nilimwambia ahsante kwani sijawahi kutumia uraibu ule, ijapokuwa mmoja wa mabibi zangu alikuwa ashki mkubwa wa kutafuna tambuu.
Wakati wa mapumziko, mashabiki wengi waliniuliza ilikuwaje? Lakini walipoona ninamwambia nahodha wa timu iliyoelemewa alikosea kwa kuchelewesha kumuingiza mrushaji mpira wa mizunguko (spinner) na badala yake kutumia mrushaji mipira ya wastani (medium pace bowler) inayomruhusu mpigaji makini kufyatua makombora ndipo walipoamini Golo alikuwa anajua kriketi.
Hii ni kumbukumbu iliyoganda kichwani kwangu na kila nikifika Dar es Salaam na kubahatika kwenda kuangalia mchezo huo, nakumbuka Jamatini kaingia Golo.
Nimeielezea kumbumbu hii ili kuwashajiisha vijana wanaoandika michezo, kujifunza michezo mingine ili kuwatendea haki wanamichezo wote kwani soka siyo mchezo pekee unaopendwa nchini.
Kutoa matokeo ya mchezo peke yake bila ya maelezo ijapokuwa kwa ufupi, ushindi ulipatikana vipi haitoshi. Japo soka inapendwa na wengi, lakini mapenzi ya wengi hayana maana wachache wakose haki zao kwani ijapokuwa tunasema demokrasia ni utawala wa wengi, lakini siyo wa kutojali masilahi au matarajio ya wachache. Usahihi wa demokrasi ni wengi wape, lakini wachache nao usiwanyime.