Furahisha: Kutopigana kunawashusha viwango mabondia
Muktasari:
- Furahisha, ambaye amekuwa katika mapambano mbalimbali ya ngumi za kulipwa, amesema bondia anahitaji kuwa na mwendelezo wa mapambano ili kuendelea kujiweka katika ushindani na kulinda kiwango chake.
BONDIA Hamadi Furahisha amesema kutopigana mara kwa mara ni moja ya sababu zinazoweza kuwafanya mabondia kushuka viwango, akimtaja Hassan Mwakinyo.
Furahisha, ambaye amekuwa katika mapambano mbalimbali ya ngumi za kulipwa, amesema bondia anahitaji kuwa na mwendelezo wa mapambano ili kuendelea kujiweka katika ushindani na kulinda kiwango chake.
Kauli hiyo inakuja wakati Mwakinyo akiwa ametoka kupigwa na Michel Soro wa Ivory Coast kwa TKO raundi ya tisa, Juni 10, 2026, katika pambano la kuwania mkanda wa IBO uzito wa kati.
Furahisha alisema sio kwamba kiwango cha Mwakinyo kimeshuka lakini rekodi za Afrika ambazo huwa zinatoka kila mwezi zinaachiwa kulingana na idadi ya mapambano.
“Mfano Mwakinyo amecheza mwezi uliopita mwezi huu hajacheza sasa watamtathmini vipi ndio maana unaona kuna muda bondia anapanda kuna muda anashuka inategemea na idadi ya mapambano aliyoshinda.” Mwakinyo, maarufu kama Champez, alikuwa na rekodi ya kuvutia kabla ya kipigo hicho. Kwa mujibu wa takwimu za mapambano zilizopo, ana ushindi 25, vipigo vinne na hajawahi kutoka sare, huku ushindi 18 ukiwa kwa KO/TKO.
Kinachoweka uzito kwenye hoja ya Furahisha ni ratiba ya mapambano ya Mwakinyo katika miaka ya karibuni. Baada ya kumshinda Mardochee Kuvesa Katembo kwa pointi Aprili 2023, alikaa takribani miezi tisa kabla ya kupanda ulingoni Januari 2024, alipomchapa Elvis Ahorgah kwa TKO raundi ya saba.
Mwaka 2024 alipigana mara tatu; kwanza alimtwanga Ahorgah Januari 27, kisha Patrick Allotey Juni 1 kwa TKO raundi ya tatu na Daniel Lartey Novemba 16 kwa TKO raundi ya tisa.
Baada ya hapo, Mwakinyo alikaa zaidi ya mwaka mmoja bila pambano jingine hadi Desemba 26, 2025, alipomchapa Mnigeria Stanley Eribo kwa TKO raundi ya pili. Pambano hilo lilimalizika baada ya dakika 1:16 za raundi ya pili.
Kabla ya kipigo cha Soro mwaka huu, Mwakinyo alikuwa ameshinda mapambano yake manne yaliyotangulia, jambo linaloonyesha kwamba licha ya vipindi vya kukaa nje ya ulingo, bado alikuwa akipata matokeo mazuri aliporejea.