Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanuni Uchaguzi Mkuu TFF zinakiukwa

Muktasari:

KAMA kuna vyombo muhimu kwa sasa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), basi ni Kamati ya Uchaguzi na ya Rufaa za Uchaguzi na Kamati ya Maadili, ambazo zinaweza kuamua mwelekeo wa uchaguzi utakuwaje baada ya usaili na kusikiliza pingamizi.

KAMA kuna vyombo muhimu kwa sasa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), basi ni Kamati ya Uchaguzi na ya Rufaa za Uchaguzi na Kamati ya Maadili, ambazo zinaweza kuamua mwelekeo wa uchaguzi utakuwaje baada ya usaili na kusikiliza pingamizi.

Hadi juzi, kulikuwa hakuna pingamizi dhidi ya mgombea yeyote, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi alipozungumza na Sports Arena ya Wasafi Media.

Pengine hiyo ni kutokana na mabadiliko ya Katiba na Kanuni za TFF kutoa haki ya kuweka pingamizi kwa wanachama wa TFF, viongozi wa kuchaguliwa wa vyama shiriki vya shirikisho hilo pekee.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa awali wakati wadau wa soka kuwasilisha pingamizi kujaribu kuzuia watu wenye matatizo kuingia madarakani kuongoza mchezo huo unaopendwa na mamilioni ya Watanzania.

Kwa hiyo, hata kama walioenguliwa wana hoja na ushahidi kuwa waliopitishwa kugombea wana matatizo yawe ya kimaadili, udhaifu katika uongozi au mengine yoyote yale hawataweza kuwasilisha pingamizi na hivyo mkasi pekee unaoweza kuwaengua ni mchujo wa mwisho utakaofanywa na Kamati ya Uchaguzi, ambayo itahoji wagombea na kuhakiki taarifa zao, ikiwa ni pamoja na vyeti.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni moja ya vyombo huru vitatu vya shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Uchaguzi inatakiwa izingatie kanuni za kidemokrasia, uwazi na pia kutangaza mchakato wa uchaguzi ‘bila kupepesa macho’.

Wakati Abdallah Bulembo, mjumbe wa zamani wa kamati ya utendaji, anasema aliliandikia Baraza la Michezo (BMT) kupinga sifa ya wagombea urais kuwa na elimu ya chuo kikuu, kifungu cha 2 (2) cha Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2021 kinazuia kabisa serikali kuingilia kati mchakato wa uchaguzi.

“Hairuhusiwi serikali kuingilia mchakato wa uchaguzi au kuwa na wajumbe katika kamati ya uchaguzi,” kinaeleza kifungu hicho. “Maana yake, kanuni za serikali za uchaguzi hazitatumika katika vyombo vya kuchaguliwa vya ndani ya Shirikisho na kanuni za uchaguzi za Shirikisho hazitatakiwa kupitishwa na chombo chochote cha serikali.”

Maana yake, hata kama BMT inataka jambo fulani liingizwe katika kanuni za uchaguzi za TFF, haitaweza kulazimisha kwa kuwa hairuhusiwi.

Zamani, uchaguzi wa vyama vyote vya michezo ulikuwa unasimamiwa na BMT ambayo pia ilikuwa inachuja wagombea na kutoa mwongozo wa sifa ambazo wagombea walitakiwa kuwa nazo na ilikuwa msimamizi siku ya kupiga kura.

Zuio hilo la serikali linaweza kutumiwa vibaya na waliopo madarakani, kujilinda kwa kuweka kanuni ambazo zinaweza kukiuka utamaduni au mila za nchi, au likatumiwa vibaya na wanaotaka kuingia madarakani kwa kujenga hoja kuwa sheria na kanuni zote lazima zifuate sheria za nchi.

Hii ni kanuni ambayo imekuwepo tangu katiba ya TFF ilipobadilishwa na kuanza kufuata miongozo ya Fifa.

Kanuni za Uchaguzi pia zinaitaka TFF ilitaarifu Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwezi mmoja kabla na linaupa uongozi uliopo madarakani haki ya kuendelea kuongoza hadi mchakato wa kupata viongozi wapya utakapokamilika.

Yaani iwapo mashauri ya Bulembo na Ali Saleh yatasababisha mchakato wa uchaguzi kusimamishwa, maana yake Wallace Karia na timu yake wataendelea kuwa madarakani hadi hapo uchaguzi utakapofanyika na kupata viongozi wapya.

Kazi za Kamati ya Uchaguzi ni kuandaa na kuendesha uchaguzi wa viongozi wa TFF, Bodi ya Ligi, vyama wanachama, ambavyo ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na ligi.

Hapa pia kuna badiliko jingine. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imepewa mamlaka ya kusimamia na kuendesha hadi chaguzi za vyama wanachama na vyama shiriki, tofauti na kanuni za mwaka 2012 ambazo mamlaka ya kamati hiyo yaliishia uchaguzi wa viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi.

Hii ni kwa sababu TFF si chama bali ni shirikisho ambalo linaundwa na vyama huru vya mikoa, klabu, na vyama shiriki, ambavyo vina katiba na kanuni zao.

Tatizo la mabadiliko hayo ni kwamba uongozi uliopo madarakani unaweza kuitumia Kamati ya Uchaguzi kuchonga uongozi wa vyama vya mikoa na shiriki kwa lengo la kutengeneza wapiga kura katika uchaguzi mkuu.

Kumekuwepo na malalamiko katika chaguzi za vyama kuwa Kamati ya TFF inaingilia na kufanya mambo inavyotaka na hivyo wagombea waliokuwa wanatakiwa na wapiga kura, kuenguliwa.

Unahitaji wajumbe waadilifu na wanaojiamini kuendesha uchaguzi huru wa vyama vya mikoa na shiriki.

Jambo jingine lililoanza kuzungumzwa katika uchaguzi huu ni kuwepo na wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi wenye undugu wa damu na baadhi ya viongozi wa juu ambao pia wanagombea. Kifungu cha 3 (3) cha Kanuni za Uchaguzi toleo la 2021, kinasema mjumbe anatakiwa kujiondoa mara moja katika Kamati ya Uchaguzi ikiwa atakuwa mgombea wa nafasi ya kuchaguliwa, au ana ndugu wa kuzaliwa au wa ndoa na wagombea wa nafasi za kuchaguliwa.

Na sharti jingine ni lile linalozuia mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji Bodi ya Ligi au chombo chochote ambacho ni mwanachama wa kawaida au shiriki.

Wajumbe wa kamati hii hupendekezwa na Kamati ya Utendaji na wanatakiwa waongoze kwa kipindi cha miaka mine, ambacho kinaweza kuongezwa.

Mwenyekiti na naibu wake wanatakiwa wawe na taaluma ya sharia, wakati wengine wanateuliwa kulingana na uzoefu wao katika soka, sifa nzuri, kutokuwa na upande wowote na mchango wake katika maendeleo ya soka.

Kamati inatakiwa kuwa na wajumbe watano, wakati katibu mkuu wa TFF atahudhuria kwa ajili ya shughuli za kiutawala na kutoa ushirikiano wa kiofisi.

Wajumbe wote wa kamati hii wanatakiwa kuidhinishwa na mkutano mkuu baada ya kupendekezwa na Kamati ya Utendaji. Lakini katiba ya TFF inasema wajumbe wanaweza kuenguliwa wakati wowote, ingawa kwa ridhaa ya mkutano mkuu.

Kanuni hii ilikiukwa wakati wa uchaguzi uliomuengua Jamal Malinzi baada ya wajumbe kutimuliwa na uongozi wa muda na kuteuliwa wengine na kuitisha na kuendesha uchaguzi bila ya ridhaa ya mkutano mkuu.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walitaka Malinzi aendelee kuwa mgombea licha ya kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi na utakatishaji fedha, jambo ambalo lilionekana kuwa kinyume na TFF.


Kesho katika mfululizo huu wa Makala kuhusu uchaguzi mkuu TFF, tutaangazia Kamati ya Maadili.


Mwandishi wa safu hii alikuwa katibu mkuu wa TFF