Prime
Cape Verde wametupa somo zuri, tuache mazoea
NI miaka michache iliyopita tuliwazuia Cape Verde kwenda fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Misri baada ya kuwachapa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kushika nafasi ya pili kwnye kundi letu nyuma ya Uganda.
Ushindi wa mabao 2-0 na ule wa mechi ya mwisho dhidi ya Uganda ndio ulisimika nafasi yetu ya pili kundini na kufuta kile kipigo ambacho hatukukitarajia cha mabao 3-0 mjini Praia, Cape Verde uliotishia nafasi yetu ya kufuzu kwenda Misri 2021.
Miaka mitatu baadaye Cape Verde wakashindwa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON zitakazofanyika mwakani baada ya kupata ushindi katika mechi moja tu wakati wa michuano ya kufuzu.
Hata hivyo, Cape Verde hawakumtimua kocha wao, Pedro Leitao Brito na kumuamini kuiongoza timu katika michuano ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dnia zitakazofanyika Mexico, Canada na Marekani,
Brito alijenga timu yenye muundo wa kujihami, ikielewana sana uwanjani na kuwa na kasi wakati inapopokonya mpira na kwenda lango la wapinzani, mbinu ambayo iliifanya iwe inapata ushindi kirahisi.
Huku mlango wa kuingia fainali hizo ukiwa umepanuliwa baada ya Fifa kuongeza timu hadi kufikia 48, Imani ya viongozi wa soka wa Cape Verde imelipa baada ya timu yao ya taifa kuishinda Eswatini kwa mabao 3-0 na hivyo kushika nafasi ya kwanza kwenye kundi lililojumuisha pia wazoefu wa fainali hizo, Camertoon ambao walilazimishwa sare ya bila kufungana na Angola na hivyo kuzidiwa kwa tofauti ya pointi nne na vijana hao wa visiwani.
Pengine ushindi dhidi ya Eswatini unaweza kuonekana mwepesi, lakini safari ya Cape Verde haikuhusu mechi dhidi ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika pekee, bali dhidi ya Cameroon na Angola ambazo pia zilipata vipigo kwenye safari hiyo.
Tanzania haijapata hata tiketi ya kwenda michuano ya mchujo ambayo itatoa timu ya ziada kutoka Afrika kufuzu kwa fainali hizo baada ya kukutana na vipigo mbele ya Morocco, Niger na Zambia vilisababisha isiweze kutumia vizuri matokeo ya mechi za kwanza ilipomudu kupata ushindi ugenini dhidi ya Zambia na Niger na hivyo kumaliza mashindano ikiwa na pointi 10.
Cape Verde ilianza vibaya mashindano kwa kulazimishwa sare nyumbani na baadaye kuchapwa kwa mabao 4-1 na Cameroon ugenini, lakini ikakomaa na kurekebisha mambo. Ilishinda mechi saba kutoka sare mbili na kufungwa mechi moja tu na hivyo kuandika historia yake ya kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza, huku ikiandika historia nyingine ya kuwa nchi ndogo ya pili kufuzu baada ya Iceland. Cape Verde ina watu 525,000 tu.
Mafanikio hayo hayajaja kama mvua bali kwa mipango ya muda mrefu ya taifa hilo ambalo soka ilikuwa ikichezwa kwa nadra sana miaka 25 iliyopita.
Uwekezaji katika miundombinu ya mpira wa miguu kama viwanja na matumizi mazuri ya program za Fifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja kwa ajili ya mechi za kimataifa, mafunzo kwa walimu wa shule za msingi kwa ajili ya kufundisha mpira wa miguu, program za vijana na jitihada za kusaka wachezaji wao vijana waliolowea barani Ulaya ni baadhi ya mambo yaliyosaidia kuamsha hamasa kwenye soka na kukuza vijana katika misingi ya soka.
Cape Verde pia imenufaika na uraa wan chi mbili unaowezesha kupata wachezaji wazuri waliokuzwa kisoka barani Ulaya lakini hawana nafasi ya kuchezea timu za taifa za nchi kama Ureno, Ufaransa na Uholanzi na hivyo kushawishika kurudi Afrika.
Nchi hiyo imeunda mfumo endelevu ambao unaandaa vijana wa ndani kula, kunywa na kucheza soka katika misingi sahihi. Lakini pia uzoefu hauwezi kusahaulika.
Ryan Mendes, anayechezea Lille ya Ufaransa, Dylan Tavares (Sochaux, Ufaransa), Jamiro Monteiro (PEC Zwolle, Uholanzi) na kipa Vozinha (Chaves) ambaye ameshacheza katika ngazi ya klabu nchini Angola, Moldova, Ureno na Cyprus na kushiriki fainali nne za AFCON, walikuwa muhimu wakati wote wa kampeni hiyo ya kihistoria.
Kwa kuangalia mafanikio hayo ya Cape Verde, Tanzania ina mengi ya kujifuza, hasa nidhamu katika program za maendeleo na kutumia watu sahihi katika kila Nyanja.
Tulishakuwa na program ya walimu wa wanafunzi (coach educators) ambayo ililenga kutoa mafunzo ya msingi kwa watoto wa shule za msingi kwa kutumia vipindi vyao vya michezo, lakini natumaini program hiyo, iliyoongezwa nguvu na serikali, sasa haipo tena. Na sijui kama kuna sababu.
Kwa walimu 38 kupata mafunzo ya stadi za msingi za soka katyika nchi yenye watu takriban 500,000 ni idadi kubwa inayotosheleza kwa kiasi fulani mahitaji ya nchi.
Hakuna nguvu yoyote inayotumika kuzilazimisha klabu za Ligi Kuu kuwa na timu za watoto, badala yake tunazitumia kulazimisha klabu za Ligi Kuu kuwa na timu za watoto ambazo ndio msingi wa mafanikio katika soka la dunia. Tumeziruhusu kuwa na wachezaji 12 wa kigeni, lakini hatuzilazimishi kushiriki katika program za maendeleo kwa kuwa na timu za watoto na vijana wadogo.
Badala yake tunaziruhusu kutafuta kundi la wachezaji kwa ajili ya kushiriki mashindano ya wiki mbili ya wachezaji walio na umri chini ya miaka 20. Matokeo yake ni kupata vi[paji vya kushtukiza kama Clement Mzize ambaye ameonekana tayari akiwa na miaka 20. Huko alikotoka alipata mafunzo sahihi katika umri sahihi?
Hatuwezi kutegemea timu ya taifa ya vijana inayopatikana bila ya kuwa na mfumo wa mashindano. Leo hii wachezaji wanakusanywa na watu wanaowajua na si kwamba walionekana kwenye mashindano fulani.
Bado tunahangaika na benchi la ufundi hadi wakati fulani kulikuwa na wasaidizi watatu. Inaonekana kama hatujui tufanye nini na kwam kutumia uzawa na mafanikio ya mwanzoni, tunataka tuaminike kuwa tuna mtu sahihi anayeongoza benchi hilo.
Lakini sidhani kama hata Hemed Morocco ana uhakika kuwa ataendelea kuongoza benchi hilo na sidhani kama hata waajiri wake wanaridhika kuwa wana mtu sahihi au si sahihi.
Lakini Cape Verde walijenga Imani kwa Pedro Brito tangu Januari, 2020 walipomtangaza kuwa kocha mkuu. Aliipeleka nchi kwenye fainali za mwaka 2021 na za mwaka 2023 wakati nchi hiyo ilipoishia robo fainali.
Yapo mengi ya kujifunza kutokana na mafanikio, sit u ya Cape Verde, bali nchi nyingine nyingi ndogo katika soka ambazo zimeonyesha nidhamu ya hali ya juu katika programu za maendeleo na zimeanza kuwa tishio, kama zile za ukanda wa kusini mwa Afrika zinazounda Cosafa.
Kuendesha mambo kwa mazoea kutatufanya kila siku tusifie mafanikio kwa kulinganisha na viongozi waliopita badala ya kufanya makubwa kama ya Botswana.
Mazoea hayajawahi kusaidia mtu kuendelea kwa sababu maendeleo yanataka uachana na desturi na kukubali kupoteza baadhi ya mambo na si kubaki vilevile.
Cape Verde wametoa somo jingine kati ya mengi yanayotolewa nan chi mbalimbali. Ni jukumu letu kumeza au kutema.