Jeuri ya Maximo ilivyomnyima historia CHAN
Klabu ya KMC ya Dar es Salaam imemtambulisha Marcio Maximo kama kocha wao mpya kuelekea msimu wa 2025/26.
Hii ni mara ya tatu kwa raia huyo wa Brazil kuja Tanzania kufundisha soka, baada ya Taifa Stars (2006-2010) na Yanga (2014).
Maximo anarudi Tanzania katika mwaka ambao nchi yetu inaandaa mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambayo yeye akiwa kocha wa timu yetu ya taifa, alishiriki yalipoanza mwaka 2009.
Yaani Marcio Maximo akiwa kocha wa Taifa Stars, alitusaidia kufuzu CHAN ya kwanza kabisa iliyofanyika Ivory Coast.
Sasa Tanzania inaandaa CHAN, na yeye amekuja Tanzania bila shaka amekuja kuwa tena sehemu ya historia kama alivyokuwa mwaka ule.
Historia itamkumbuka Maximo kwa kuisaidia Stars kufuzu CHAN kwa mara ya kwanza, lakini ingeweza kumkumbuka zaidi ya hapo endapo yeye mwenyewe angetaka.
Maximo alichagua kukukumbukwa kidogo na historia na kukataa kukumbukwa kwa ukubwa mkubwa.
KIVIPI?
Kocha huyo raia wa Brazil aligombana na wachezaji muhimu wa timu kwenye mashindano hayo na kuidhoofisha timu.
Wachezaji hao walikuwa Haruna Moshi 'Boban' na Athuman Idd 'Chuji'. Akiliongoza jeshi lake vitani, kamanda Maximo alikubali kuwapoteza askari wake muhimu na hatimaye kushindwa vita. Lakini akasimamia alichokiamini.
Licha ya jitihada za serikali chini ya waziri wa michezo wakati huo, Seif Khatib, kusuluhisha mgogoro ule, lakini kocha hakusikiliza na mwishowe kuigharimu timu.
Wachezaji hao bora ambao Tanzania ilibahatika kuwa nao, na tena wakiwa katika ubora wao wa hali ya juu, wakakosekana katika wakati muhimu.
Boban alicheza mechi moja tu, tena chini ya dakika 30, na Chuji ndio hakucheza kabisa. Chanzo cha mgogoro wao kilitajwa kuwa ni NIDHAMU, lakini haikuwahi kutajwa zaidi ya hapo kwamba nidhamu imefanya nini na kivipi.
Naam, nidhamu ni kitu muhimu sana, na hakina mjadala lakini nyoka anapoingia ndani ya nyumba yenu, hata kama mna ugomvi, unganeni kwanza mumtoe halafu muendelee na ugomvi wenu, bila hivyo atawang'ata na mtakufa. Hiki ndicho ninachomaanisha na ndicho kilichotokea.
Maximo alipaswa kufunika kombe mwanaharamu apite sasa hivi angekuwa mtu wa mfano. Aliwatuhumu wachezaji wale kukosa nidhamu na kuamua kuwarudisha nyumbani baada ya mechi ya kwanza tu, dhidi ya Senegal.
Stars ilipoteza mechi hii kwa bao 1-0 huku kiungo mchezeshaji aliyekuwa bora zaidi nchini wakati huo, Haruna Moshi, akipangwa kama winga wa kushoto.
Akacheza dakika zisizozidi 30, akatolewa na ndio hakucheza tena hata benchi hakuwahi kukaa.
Athuman Idd 'Chuji' kiungo bora zaidi wa ulinzi nchini kwa wakati ule, ndio hakuvaa jezi hata mara moja.
Baada ya mechi ya kwanza, Marcio Maximo akatoa amri wachezaji hao warudishwe Tanzania.
Waziri wa michezo wa wakati ule, Seif Khatibu, akafanya kikao na kocha na viongozi wa TFF na serikali waliokuwa kule kujaribu kutuliza hali.
Wakakubaliana kwamba wachezaji hao wasirudishwe nyumbani kwa sababu italeta mtafaruku.
Wakabaki na timu lakini mechi zote zilizobaki walikaa jukwaani kama mashabiki. Taifa Stars iliyopangwa kundi A, sambamba na wenyeji Ivory Coast, Zambia na Senegal, ilimaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 4, moja nyuma ya vinara Zambia na Senegal.
Timu mbili za juu zilitakiwa kufuzu nusu fainali moja kwa moja hakukuwa na hatua ya 16 bora wa robo fainali wakati ule.
Baada ya kupoteza 1-0 kwa Senegal, Stars ikashinda 1-0 dhidi ya Ivory na kutoka sare ya 1-1 na Zambia kwenye mechi ya mwisho.
Kwenye makaratasi kundi la Stars lilikuwa gumu sana na nafasi ya Tanzania kupenya ilikuwa ndogo.
Lakini uwanjani hali ikawa tofauti, Tanzania ingeweza kabisa kufuzu nusu fainali kama sio mgogoro wa Maximo na wachezaji wake muhimu.
Na mechi iliyowaumiza zaidi Watanzania ni dhidi ya Zambia kwa sababu Stars ilipata bao la kuongoza dakika ya 88 ikashindwa kulinda, Zambia wakasawazisha dakika ya 90+4, kwa kushindwa kulinda kona.
Endapo Stars ingeshikilia bomba zile dakika 5 za nyongeza, basi ingefuzu nusu fainali.
Japo mpira hautabiriki, lakini unaweza kabisa kuthubutu kusema Boban na Chuji wangekuwepo kwenye hizi mechi na wakacheza kwa nafasi zao, matokeo yangeweza kuwa tofauti.
Na hata kabla ya mashindano haya, Maximo alimuacha kipa bora wa nchi wa wakati huo, Juma Kaseja.
Kaseja ambaye mgogoro wake na Maximo ulianzia Brazil kwenye kambi ya mwaka 2008, hakuwa tena sehemu ya timu licha ya kuwa kipa bora namba moja nchini.
Endapo Maximo angeweka pembeni matatizo yake binafsi na wachezaji hawa muhimu, yawezekana hali ingekuwa tofauti na historia ingemkumbuka tofauti.
Lakini akachagua kuoneshana ubabe na sio tu kuigharimu nchi, bali heshima yake mwenyewe.
Makocha wengine wakubwa duniani huepuka mutafaruku kama hii, au huweka pembeni matatizo yao binafsi na kuweka mbele maslahi ya timu.
Roberto Mancini wa Manchester City alikorofishana na Carlos Tevez wakati wa harakati za kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2011/12.
Tevez akakasirika na kurudi kwao Argentina na kupumzika.
Mancini akamuita na kumtaka amsaidie kushinda ubingwa na akamsaidia, ndio ule msimu wa Aguerooooooo!
Leo hii Mancini anakumbukwa kama kocha aliyeipa ubingwa wa kwanza Manchester City baada ya miaka zaidi ya 40.
Hakuna anayemkumbuka kama kocha aliyempigia magoti Carlos Tevez.
Sasa hivi Maximo angekuwa anakumbukwa na taifa kama kocha aliyeifikisha Tanzania nusu fainali.
Tena kwa kumtolea mfano kwamba aliweka pembeni matatizo yao binafsi na kutanguliza maslahi ya timu.
Lakini hakuchagua hilo...