Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ishu ya Amorim, Rashford sio yeye tu

Muktasari:

  • Rashford amekuwa nje ya kikosi cha Man Unied kwa muda sasa licha ya kuonekana mara kadhaa mazoezini lakini Amorim hamjumuishi kabisa katika kikosi cha kinachoanza au hata benchini.

MANCHESTER, ENGLAND: MOJA kati ya mambo yanayoendelea England kwa sasa ni sakata la kocha Ruben Amorim na staa wake Marcus Rashford ambaye hivi karibuni aliweka wazi kwamba yupo tayari kuondoka na kwenda kutafuta changamoto mpya kwingineko.

Rashford amekuwa nje ya kikosi cha Man Unied kwa muda sasa licha ya kuonekana mara kadhaa mazoezini lakini Amorim hamjumuishi kabisa katika kikosi cha kinachoanza au hata benchini.

Inaelezwa kocha huyu ambaye awali alimjumuisha Alejandro Garnacho katika hili, anamweka nje Rashford kutokana na kutofuata kile ambacho yeye anakihitaji, pia amekuwa na baadhi ya mambo ya nje ya uwanja ambayo yeye Amorim na benchi lake hawaoni kama ni sahihi.


Roy Keane - Man United 

Watu wengi wanaijua hadithi hii. Roy Keane, mchezaji wa zamani wa Manchester United aliyehudumu  kwa miaka 12 na nahodha wa mashetani wekundu hao kwa miaka minane kati ya hiyo, alifikia mwisho wa maisha yake kwenye viunga hivyo mara baada ya kugombana na kocha wake Sir Alex Ferguson.

Keane aliingia katika mgogoro na Fergie, baada ya kufanya mahojiano na  MUTV ambapo aliwakosoa wachezaji kadhaa wa timu hiyo baada ya kupoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Middlesbrough  Oktoba, 2005. Fergie alizuia mahojiano hayo yasirushwe, na baadaye mkataba wa Keane ulivunjwa mwezi uliofuatia, kisha akatimkia zake  Celtic.


Dele Alli - spurs

Alikuwa akipanda kwa kasi sana akionekana kama mmoja kati ya nyota ambao wangeweza kufanya makubwa sana England. Alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Tottenham.

Alifanikiwa pia kushinda tuzo ya  Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa PFA mwaka 2016. Hata hivyo, kufukuzwa kwa Mauricio Pochettino na ujio wa Jose Mourinho mwaka 2019 vilimpoteza kabisa.

Mourinho alikuwa akimsema staa huyu kuwa ni mvivu katika suala la kukaba, hivyo hakuwa anampa nafasi ya kucheza na tangu hapo hakuwahi kurudi tena kwenye kiwango chake licha ya kuondoka Spurs na kwenda Everton na Besiktas.

Katika mahojiano yake na  Gary Neville hivi karibuni alikiri kwamba wakati wa uongozi wa Mourinho, aliwahi kuamka siku moja na kufikiria kustaafu soka. 


Ruud van Nistelrooy - Man United 

Baada ya kushinda kiatu cha dhahabu msimu wa 2002/03 na kufunga mabao zaidi ya 20 katika misimu minne tofauti ya Ligi Kuu ya England, mshambuliaji huyu wa zamani wa Uholanzi alihesabiwa kuwa mmoja wa wafungaji bora barani Ulaya kwa wakati huo. 

Lakini muda wake katika kikosi cha Man United ulifikia ukingoni mwaka 2006. Si tu kwamba alikaa benchi wakati wa fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Wigan Athletic, tukio ambalo Rio Ferdinand anaamini lilichangia kuondoka kwake,  pia aliachwa benchini katika mechi sita za ligi mfululizo. Ingawa alirejea kwenye kikosi cha kwanza baada ya hapo, aliukosa mchezo wa mwisho wa msimu wa 2005/06 dhidi ya Charlton Athletic.

Alikumbana na hali hii baada ya uhusiano wake na Ferguson kuvurugika kutokana na kauli yake juu ya baba wa Ronaldo. Baada ya hapo aliondoka katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2006.


Mesut Ozil - Arsenal 

Alipowasili Arsenal akitokea Real Madrid mwaka 2013, alionyesha kiwango bora kiasi cha mashabiki wa timu hiyo kumpenda sana.

Ozil ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za kiufundi, mwisho wake katika kikosi cha washika mitutu hao ulikuwa mbaya chini ya Mikel Arteta ambaye anadaiwa kuwa alimweka nje kutokana na sababu za nje ya uwanja na sio uwezo wake.

 Arteta aliamua kumwacha nje ya kikosi cha Arsenal kwa mechi za Ligi Kuu na Europa League, kabla ya kufikia makubaliano ya kuvunja rasmi mkataba wake Januari 2021 na hatimaye akatimkia Fenerbahce ya Uturuki.

                               

Ronaldo - Man United     

Kurudi kwa Cristiano Ronaldo katika kikosi cha Man United lilikuwa ni moja ya matukio makubwa ya msimu wa 2021/22.

Ingawa msimu wake huo wa kwanza haukuwa mzuri kwa timu walimaliza katika nafasi ya sita, Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, alionyesha kiwango bora akifunga mabao 18 ya Ligi Kuu katika mechi 30 alizocheza.

Lakini mambo yalibadilika haraka katika msimu uliofuatia baada ya ujio wa Erik ten Hag ambaye alikuwa akimweka benchini na mwisho Ronaldo alifanya mahojiano yaliyoibua mambo mengi ambayo ndani yake aliweka wazi kwamba hakuwa na maelewano mazuri na Ten Hag. Baada ya mahojiano hayo Ronaldo alivunja mkataba na Man United kisha akatua zake Al Nassr.