Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Irankunda kutoka Kigoma hadi Bayern Munich

Familia yake ilikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe  huko Burundi vilivyodumu kuanzia 1993 hadi 2005 na kuingia Kigoma pasipo hata kuwa na fikra kuwa siku moja itazaa mtoto ambaye atakuja kuwa nyota atakayetikisa kwenye medani ya soka duniani.

Ni kumbukumbu tamu ya kijana aliyezaliwa miaka 17 iliyopita katika kambi za wakimbizi Kigoma, Nestory Irankunda ambaye muda mfupi ujao huenda akakamilisha usajili wa kujiunga na miamba ya soka duniani, Bayern Munich kwa uhamisho unaotajwa kuwa wa Pauni 3 milioni, kiasi ambacho kitaongezeka zaidi kulingana na namna atakavyoonyesha kiwango bora ndani ya timu hiyo.

Jina la Irankunda lilianza kutajwa kuanzia mwaka juzi kama miongoni mwa wachezaji chipukizi wanaotegemewa kuwa mastaa wakubwa wa soka siku za usoni kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha akicheza kama winga.

Ni kiwango chake cha kuvutia ambacho kilimfanya kuwa mchezaji tegemeo wa Adelaide United licha ya umri wake mdogo akiwa pia mchezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Australia chini ya umri wa miaka 17.


Historia ya kipekee

Alizaliwa Februari 9, 2006 katika kambi ya wakimbizi mkoani Kigoma ambako familia yake ilikimbilia ili kutafuta hifadhi kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo ilidumu kwa muda mrefu Burundi.

Akiwa na umri wa miezi mitatu tu, familia yake ilihamia Australia ambako Irankunda alianza kuonyesha mapema kipaji cha soka alichonacho kwa kucheza na watoto wenzake mahali ambako familia yake ilikuwa inaishi.

Maskauti wa timu ya Adelaide Croatia Raiders iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza walimuona na kumchukua akiwa na umri wa miaka 12 na aliitumikia hadi 2021 aliponaswa na Adelaide United ambayo ilivutiwa na kipaji chake.

Baada ya hapo taarifa za kipaji chake zilisambaa Australia nzima na miongoni mwa walioshangazwa naye ni mkuu wa idara ya skauti ya Adelaide United, Airton Andrioli aliyesema kwamba kinda huyo ni wa aina yake.

“Zawadi ya ufahamu na kuusoma mchezo aliyonayo Nestory hauwezi kuiona  sana kwa wachezaji wa Australia,” alinukuliwa Andrioli.


Namba zinaongea

Sio jambo la bahati mbaya kuona timu ya Bayern Munich inamhitaji Irankunda na ni matokeo ya kiwango bora ambacho anakionyesha uwanjani kikibebwa na takwimu bora alizonazo licha ya umri mdogo.

Katika mechi 39 alizoichezea Adelaide United tangu alipojiunga nayo mwaka 2021, ameifungia mabao tisa na kupiga pasi za mwisho mbili takwimu ambazo kocha Thomas Tuchel anaona zinatosha kumpa jezi ya Bayern Munich.

Hata hivyo, baada ya kumsajili, Bayern Munich inaripotiwa kwamba itamuacha kwa mkopo wa mwaka mmoja katika kikosi cha Adelaide United ili aimarike zaidi.


Azitoa udenda timu za taifa

Kikanuni, Nestory Irankunda anaruhusiwa kuchezea timu mojawapo kati ya tatu za taifa ambazo ni Australia, Tanzania na Burundi kutokana na kukidhi vigezo vya kuchezea yoyote kati ya hizo.

Anaweza kuitumikia timu ya taifa ya Burundi kutokana na asili ya wazazi wake ambao wote ni raia wa nchi hiyo.

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inaweza kupata huduma yake kwa vile mchezaji huyo alizaliwa katika ardhi ya Tanzania.

Australia ambayo timu yake ya vijana chini ya umri wa miaka 17 imeshafaidi huduma yake na kikosi cha wakubwa kinaweza kumtumia kwa vile amekulia nchini humo.


Muendelezo wa kumbukumbu

Historia inaonyesha Irankunda sio mchezaji wa kwanza staa kuwa na fursa ya kuichezea Tanzania ambapo wapo walioitumia na kuna walioamua kuikacha na kutumikia mataifa mengine.

Nyota wa Denmark, Yusuf Poulsen angeweza kuichezea Taifa Stars kwa vile baba yake ni Mtanzania lakini akaamua tofauti.

Mfano mwingine ni Bernard Kamungo ambaye hivi karibuni aliamua kutumikia timu ya taifa ya Marekani licha ya awali kuitwa kuichezea Taifa Stars katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Niger, lakini hakucheza mechi hiyo.