Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu ni wakati wa waandishi kuwa makomandoo-2.

Muktasari:

“Wako wagombea watakaojitokeza ambao walishakuwepo kwenye kila ngazi ya uongozi na kuthibitika kuwa hawana uwezo. Hao watapewa nafasi kwenye vipindi vya redio na televisheni na hata kuandaliwa midahalo ili kuwaaminisha watu kuwa wao ndio wanaofaa kuongoza na makosa waliyofanya huko nyuma ni ya kuonewa, hata kama ni dhahiri.

MZEE wa Kutibua amezoea kuonekana kwenye ukurasa huu lakini ameamua kutoa nafasi kuhitimisha waraka aliotumiwa na Mwanandinga ambao ulianza wikiendi iliyopita. Endelea kumsoma Mwanandinga:
“Wako wagombea watakaojitokeza ambao walishakuwepo kwenye kila ngazi ya uongozi na kuthibitika kuwa hawana uwezo. Hao watapewa nafasi kwenye vipindi vya redio na televisheni na hata kuandaliwa midahalo ili kuwaaminisha watu kuwa wao ndio wanaofaa kuongoza na makosa waliyofanya huko nyuma ni ya kuonewa, hata kama ni dhahiri.

“Waandishi wataingia kwenye chaguzi hizo za Simba na Yanga, wakiwa tayari wana mgombea wao mara nyingi ni yule anayemwaga fedha na watafanya kampeni kubwa kutaka kuwaaminisha wanachama kuwa huyo wanayempigia debe ni mtu anayefaa kuongoza.

“Wapo wanachama werevu na wenye akili ambao watagundua uozo huo. Maana yake hapa, si ajabu utakaposikia mwandishi au mtangazaji mmoja amenusurika kupigwa au ametangaziwa karantini ya kutofika kwenye maeneo ya moja ya klabu hizo.

Hii ni kawaida na pengine itafikia wakati wanachama watakaofanya vituko hivyo wataonekana kuwa ni sahihi kwa kuwa waandishi wanazidi kukiuka maadili ya kazi zao.

“Ndio maana nasema uchafu huu unazidi kushusha hadhi ya vyombo vya habari na kuwafanya waandishi wasiaminike tena kwa sababu wanatanguliza maslahi yao kwanza bila ya kujali mustakabali wa klabu na soka kwa ujumla.

“Ni vizuri vyombo vya habari vikawa makini sasa na kudhibiti uozo wowote unaofanywa na waandishi wanaojali maslahi yao. Vyombo vya habari vianze kwanza kukememea uozo wa wanahabari wake kabla ya kukemea uozo kwa wanachama.

“Ni kwa jinsi hiyo tu, hadhi ya vyombo vya habari itaweza kulindwa. Na ikitokea mwandishi ameshambuliwa kwa sababu ametimiza wajibu wake na amefanya kazi yake kwa weledi na uadilifu, itakuwa sahihi kwa vyama vya waandishi kusimama na kumtetea mwandishi huyo.

“Lakini tukiachia waandishi wajiingize kwenye siasa za uchaguzi na mmoja wao kushambuliwa kwa sababu hiyo, haitakuwa sahihi mwandishi huyo kutetewa, bali itakuwa sahihi kwake kukemewa na kuchukuliwa hatua na chombo chake.”

“Kwani atakuwa ameipaka matope taaluma ya uandishi wa habari na atastahili kuadhibiwa kutokana na matendo yake.

“Waandishi wa habari tuendelee kuangalia yanayotokea katika chaguzi hizi na kuzipa haki sawa katika kuripoti kuliko kuendekeza matumbo yetu.

“Tutoe haki sawa kwa wagombea bila ya kujali majina yao wala hadhi zao katika jamii, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetimiza majukumu yetu na kulisogeza mbele soka la Tanzania.

“Ikumbukwe viongozi bora huanzia kwenye klabu kama tukiwapitisha wababaishaji kwa ajili ya kushibisha matumbo yetu, tutakuwa tumelikosea Taifa la Tanzania kwa kulididimiza katika nyanja ya michezo.

Huu ndio ukweli, laiti kama kutakuwa na watu watanichukia itakuwa ni kwa sababu ya maslahi yao binafsi.

Nimelazimika kusema haya kwa nia nzuri tu ya kuwa na wanataaluma makini katika sekta hii ya habari ambayo mbali ya kazi ya kuhabarisha umma, pia inao wajibu wa kuelimisha.

Pia maoni yangu yanalenga kuzipatia klabu zetu za soka viongozi safi wenye dira za kweli za maendeleo na mtazamo chanya.

Ni kwa njia hii ndio naamini siku moja nasi tutafanikiwa kama wenzetu.