Prime
Humud: Maumivu ya mapenzi hayachagui sura
MAPENZI ndiyo yanayoendesha dunia na huwa hayachagui ni nani wa kupata maumivu. Ukiyavamia tu, ujue kuna mawili, kupata furaha au maumivu.
Hayachagui wa mumpa raha na maumivu, uwe tajiri, uwe masikini, hayachagui sura, hayaangalii una mwonekano gani.
Wapo mastaa wengi duniani mapenzi yamewatenda pamoja na kuwa na uwezo wa kifedha na ushawishi. Kwa kiungo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Abdulhalim Humud, yeye ni nani yasimkute?
Nyuma ya Kamera ilimtafuta nyota huyo ambaye anasimulia kwa masikitiko namna alivyokumbana na hali hiyo, huku akilengwa na machozi kwa namna allivyopigwa tukio na mpenzi wake.
Ingawa alishindwa kulisimulia tukio ambalo ndiyo limesababisha asiamini katika mapenzi, anasisitiza hataki hata kuyasikia kwani tayari anajua upendo wa furaha na maumivu.
“Niliwahi kumpenda sana mwanamke mmoja, lakini ambacho kilikuja kunikuta siwezi hata kusimulia, maana maumivu yanaweza yakarudi na yatanitoa machozi,” anasema Humud na kuongeza;
“Kwa sasa nayachukulia mapenzi kama moja ya changamoto ambazo naweza kukutana nazo muda wowote katika maisha, kwanza siamini katika mapenzi na sitaki hata kuyasikia, kwasababu nilishawahi kupenda najua maumivu yake pia najua utamu wake.
“Mbaya zaidi jamii inayokuzunguka inakuchukulia muda wote una furaha, haijui kuna wakati tunapitia maumivu makali, hivyo kujulikana siyo kigezo cha kuondoa ubinadamu, vipaji vyetu ndivyo vilivyotutambulisha kwa watu.”
Ukiachana na tukio la kuumizwa na mwanamke aliyempenda kumsaliti, matukio ya kuumizwa kimapenzi yametokea kwa nyakati tofauti, kwani inakuwa ngumu kuwatambua watu wema na wabaya wanaokuja kwenye maisha yao.
“Watu unaowaamini ni sahihi ndiyo wanaokuumiza, mbaya zaidi kipindi ambacho mtu sahihi anatokea wewe unakuwa huamini tena katika mapenzi, kwa sababu wanawake hawajawahi kueleweka wanataka nini kwa mwanamume,” anasema Humud na kuongeza;
“Ukiwa maarufu anakutumia kama daraja la yeye kujulikana, ukiwa na pesa anakufanya sehemu ya kutimiza malengo yake, ukimwonyesha upendo anakuwa anakuhisi una mwanamke mwingine, kuna kitu unakificha, hivyo anayeitwa mwanamke katika suala la mapenzi hajawahi kujulikana anataka nini, kusema ukweli mtu maarufu ngumu kupata mtu sahihi.
“Maumivu yamechukua nafasi kubwa ila tayari nimesamehe katika kila kilichotokea na kusababisha maumivu, ndiyo maana siamini tena katika mapenzi.”
Mbali na mapenzi anasema kuna nyakati wanakosa wanachokitaka, lakini bado jamii inawaona muda wote wanapata kila wanachohitaji:
“Wakati mwingine mtu ambaye hajulikani anakuwa na maisha ya uhuru zaidi.
Anaongeza: “Naamini katika mipango ya Mungu, nikipata Alhamdulillah nikikosa Alhamdulillah, hiyo ndiyo maana ya maisha nakuishi, hatupaswi kushukuru nyakati za furaha pekee.”
Ingawa jambo la msingi kwake anasisitiza wakati wa kazi hana mzaha, hata likija suala la mapenzi linakaa pembeni:
“Kila kitu kinakaa mahali pake ndiyo maana siyumbi kwenye majukumu yangu.
Anaongeza: “Kitu pekee kinachoumiza ni hatujui anayekuja kwenye maisha yetu ana lengo gani moyoni mwake, kwasababu mwingine anakuja kwako kwasababu wewe ni maarufu, mwingine anakuja kwasababu ya muonekano wako, mwingine anaamini atapata kila anachotaka kwa muda anaotaka, mwingine anakuja ili watu wajue upo naye, hawajui tuna malengo nje na kazi zetu za uwanjani.”