Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ilipofikia ishu ya Mlandege, Pamba Jiji

USAJILI Pict

Muktasari:

  • Wachezaji hao tayari wamecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara ambapo Pamba Jiji ilikabiliana na Simba na Azam.

TIMU ya Mlandege inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), imewasilisha malalamiko Shirikisho la Mpira wa Tanzanzia (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) ikidai Pamba Jiji imewatumia wachezaji wake wawili, Nonyem Okorocha na Vellim Nashon Opondo, wakati mchakato wa uhamisho wao haujakamilika.

Wachezaji hao tayari wamecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara ambapo Pamba Jiji ilikabiliana na Simba na Azam.

Taarifa iliyotolewa na Mlandege Agosti 23, 2026, ilisema licha ya timu hizo mbili kuwa na makubaliano ya mauziano wachezaji hao, lakini Mlandege inadai kuwa haijapokea malipo yoyote kutoka Pamba Jiji.

“Mlandege inathibitisha kulikuwa na mauziano kwa wachezaji hao kuhamia Pamba Jiji, hata hivyo timu haijapokea malipo ya aina yoyote yanayohusiana na uhamisho wa wachezaji hao,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema, Mlandege imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasilisha barua ya malalamiko TFF na ZFF ikiziomba mamlaka hizo kuchukua hatua kwa kuhakikisha matumizi ya wachezaji hao yanafuata kanuni na taratibu za usajili na uhamisho.

Mbali na hilo, Mlandege imesema ipo tayari kumaliza suala hilo kwa maelewano endapo Pamba Jiji itaheshimu makubaliano yaliyofikiwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Mlandege, Hussein Ahmada, alisisitiza kuwa bado wachezaji hao wana mkataba na timu yao.

Amesema, tangu wametoa taarifa hiyo, viongozi wa Pamba Jiji hawajafanya jitihada yoyote ya kuwasiliana nao, hivyo kilichobaki wanasubiria majibu ya mamlaka kwani wamesema wanalifuatilia suala hilo.

“Tamko hilo sio hatua ya mwanzo kwa sababu tulifanya juhudi mbalimbali kabla dirisha kufungwa ikiwemo kuwaandikia barua ingawa hawaoneshi ushirikiano wowote,” amesema Ahmada.

Katibu huyo, ameziomba mamlaka zifanye uamuzi kwa kuzingatia sheria na kanuni, lakini kama hawataridhishwa na majibu ya mamlaka hizo hazitoishia hapo.

USAJ 01

KAULI YA ZFF

Katibu wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ZFF, Kassim Mahmoud Abdalla, amesema timu ya Pamba Jiji haijafuata kanuni na sheria kufanya uhamisho kwa wachezaji hao.

Amesema, ili wachezaji hao kuwa halali upande wao walipaswa kuvunja mkataba walionao kwa timu ya Mlandege ndipo wawatumie.

“Wachezaji hao sio halali kwa Pamba Jiji kwani bado wana mikataba na Mlandege, wamefanya uhamisho bila kuzingatia sheria na kanuni za TFF na ZFF,” amesema.

“Pamba Jiji haikuzingatia uhamisho kutoka kwa klabu kwani wachezaji walipaswa kuwa na barua maalumu zilizotolewa na timu ambayo walikuwa na mkataba nao awali ndipo wawe halali upande wao.”

USAJ 03

WASIKIE PAMBA JIJI

Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William, akizungumzia hilo, amesema: “Bahati nzuri wewe utakuwa unaelewa utaratibu, mpaka mchezaji anaruhusiwa kucheza mechi ya mashindano chini ya Shirikisho la soka na Bodi ya Ligi maana yake amekidhi vigezo, ili mchezaji aruhusiwe kucheza anakuwa amekidhi vigezo, ili mchezaji anapewa leseni ya kucheza lazima kuna vitu unakuwa umeweka vizuri mkataba ukiwemo, kwa hiyo yote unayoyafahamu tumeyafanya.

Na hayo hamuwezi kuyafanya klabu moja peke yenu, lazima mfanye na klabu anapotoka. Kwa hiyo mtiririko wote tumeufanya ndiyo maana wale wachezaji mnawaona.

USAJ 02

“Kinachotokea sasa hivi sijui nitumie lugha gani, lakini sisi Pamba Jiji hatupo kwenye nafasi nzuri ya kulisemea hilo lakini ukweli ni kwamba yapo wanayoyazungumza mule kwenye taarifa yao yapo ni ya ukweli na yapo ambayo si ya ukweli.

“Ya ukweli ni kwamba, yapo makubaliano ya taasisi mbili kwa maana ya Pamba Jiji na Mlandege, sasa inawezekana hayo makubaliano hayajatekelezwa, aidha muda wa kutekelezwa bado au kuna vitu havijafanywa, kwa sababu ni mambo ya kitaasisi siwezi kuyaweka hapa.

“Tunawaheshimu Mlandege, kama kuna hoja za kitaasisi naamini tayari zimeshazungumza na mambo yanakwenda vizuri, ni kutokufuata tu taratibu naweza kusema ndio kumeleta haya, lakini hatuna changamoto, sisi tunaendelea kuzungumza na jambo litamalizika vizuri wala sisi hatuna sababu ya kuanza kujibu kile ambacho wamekisema.” 

Okorocha ni Mnigeria na Opondo ni Mtanzania, ni mabeki ambao walitua Mlandege katika dirisha dogo la usajili 2026, huku wakiwa sehemu ya nyota walioimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo iliyomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar 2025-2026, ikiruhusu mabao 25 katika mechi 30. Nyota hao wametua Pamba Jiji dirisha kubwa la msimu huu 2026-2027, huku Okorocha akifunga bao moja dhidi ya Azam katika kipigo cha mabao 2-1 ilichopokea Pamba Jiji.

USAJ 04

KANUNI ZINASEMAJE

Kwa mujibu wa kanuni za uhamisho wa wachezaji, Shirikisho la Mpira wa Soka Tanzania (TFF), imebainisha kuwa hakuna uhamisho utakaotambulika kisheria kama hautapitia mfumo rasmi wa FIFA Connect.

Ili mchezaji akamilishe usajili wake mpya, klabu zinapaswa kuwasilisha nyaraka muhimu zikiwemo mkataba mpya wa ajira, fomu ya vipimo vya afya (Medical Test), na Hati ya Kuachwa Huru (Release Letter) au mkataba wa mauzo kutoka klabu ya zamani.

Kwa wachezaji huru wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na kusaini mikataba mipya moja kwa moja bila kuhusisha klabu zao za zamani, mradi tu kuwe na thibitisho la kumalizika kwa mkataba uliopita.

Kuhusu wachezaji wanaotoka nje ya nchi, TFF imesisitiza kuwa lazima klabu zinazowasajili ziombe Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kupitia mfumo wa FIFA TMS.