Prime
Hongera Simbu, aibua jambo zito
Muktasari:
- Na kati ya hao wachache waliojua, wengi wao hawakuwa na matumaini kwamba mwanariadha huyo wa mbio ndefu angeibuka na medali ya dhahabu katika mashindano hayo magumu yanayoshirikisha wanariadha nyota d
KATIKA nchi yenye wendawazimu wa mpira wa miguu, inawezekana ni watu wachache sana walijua kuwa Alphonce Felix Simbu alikuwa ameenda nchini Japan kushiriki mashindano ya ubingwa wa riadha duniani.
Na kati ya hao wachache waliojua, wengi wao hawakuwa na matumaini kwamba mwanariadha huyo wa mbio ndefu angeibuka na medali ya dhahabu katika mashindano hayo magumu yanayoshirikisha wanariadha nyota duniani.
Pamoja na ushindi ambao Simbu amekuwa akipata katika mashindano tofauti, isingekuwa rahisi kutegemea kuwa angeweza kupambana na Waethiopia, Wakenya na wenyeji na kuwashinda na kuwa bingwa wa dunia wa marathoni.
Inaweza kuwa ni Simbu pekee ndiye aliyeamini kuwa ataweza kushinda baada ya kushika nafasi ya pili wakati mashindano hayo yalipofanyika London, Uingereza mwaka 2017. Na hata kauli yake baada ya ushindi huo wa kihistoria inaonyesha kuwa alitegemea kuwa angeshinda.
“Nakumbuka mwaka 2017 katika mashindano ya Ubingwa wa Dunia wa Riadha jijini London, nilishinda medali ya shaba. Baadaye nikashiriki mara nyingi bila ya kushinda medali yoyote,” alisema Simba baada ya mbio hizo za Japan.
“Hatimaye ikawa hapa. Wakati nilipofika hapa, nilijiambia mwenyewe kuwa sitakubali,” alisema Simbu baada ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa ubingwa wa dunia wa marathoni katika mashindano hayo makubwa.
Simba alishinda mbio hizo katika hatua ya mwisho alipochomoka kwa kasi baada ya kuingia Uwanja wa Taifa wa Japan, akiwa katika nafasi ya pili nyuma ya mwanariadha wa Ujerumani, Amana Petro.
Simbu aliweka akili yake katika kumaliza huku Amana akigeuka takriban mara tatu kumuangalia Simbu, kitu ambacho, inaaminika humpoteza hatua kiasi mwanariadha. Kadiri alivyogeuka ndivyo Simbu alivyokaza macho mbele, kuongeza kasi hadi akampita katika hatua ya mwisho na kuwahi kuvuka kamba.
Alishinda kwa kutumia saa 2:09:48 huku Amana akitumia saa 2:09:48 na mwanariadha wa Italia, Illias Aouani akitumia saa 2:09:53. Ingawa muda wa Simbu na Amana unaonekana unalingana lakini Mtanzania huyo alimzidi mpinzani wake kwa tofauti ya nukta tatu.
Ilibidi kutumia teknolojia ya picha (photo finish) kumpata mshindi na hivyo matokeo hayo kuweka historia ya washindi kutofautiana na muda mfupi kuliko mengine yote ya ubingwa wa dunia wa riadha.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya jitihada za muda mrefu za Simbu katika mbio duniani. Alitwaa medali ya shaba katika mashindano hayo mwaka 2017, akatwaa medali ya shaba katika mashindano ya World Marathon Majors jijini Boston mwaka huu na ameshatwaa medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022 jijini Birmingham.
Katika Michezo ya Olimpiki iliyopita ndiye mwanariadha pekee wa kiume wa Tanzania aliyemaliza mbio za marathon baada ya wengine kuishia njiani. Katika nchi ambayo mchezo wa riadha umepoteza umaarufu wake uliotokana na mafanikio ya wanariadha magwiji kama Filbeth Bayi, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga, Clever Kamanya, Nzael Kyomo, Mwinga Mwanjala, Suleiman Nyambui, haikuwa rahisi kutegemea medali katika mashindano hayo.
Licha ya taasisi nyingi kuandaa mbio za marathon kila mwaka na katika mikoa tofauti, bado nchi haijaweza kuzalisha wanariadha wazuri wa mbio ndefu zaidi ya hawa kina Simbu na wenzake ambao huinuka kutokana na jitihada binafsi.
Chama cha Riadha (RT) bado hakijaweza kutoka na mkakati mzuri wa kuzalisha wanariadha wa mbio fupi, masafa ya kati na mbio ndefu na inaonekana jitihada binafsi ndio huzalisha wanariadha wa mbio ndefu, wengi wakitoka mikoa kama Arusha, Manyara na Singida ambako kuna vipaji vya mchezo huo.
Kwa hiyo, kwa Simbu kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano hayo makubwa, ni kengele inayopigwa kwa Chama cha Riadha kuwa kuna Watanzania wenye uwezo wa kufanya makubwa katika jukwaa kubwa, lakini bado hawajatengenezwa ipasavyo.
Mikoa hiyo mitatu imekuwa ikizalisha wanariadha wengi wa mbio ndefu na masafa ya kati, lakini hatuoni kama AT ina mkakati wowote katika maeneo hayo ili kuwavuna kirahisi wenye vipaji, kuwapa mafunzo sahihi ili kuwaandaa kwa mashindano makubwa.
Zamani mikoa kama Mara, Mbeya na ya Zanzibar ilisifika kutoa wanariadha wa mbio fupi kama kina Morris Okinda, Norman Chihota, Ali Hamis, Makame Ally na wengine lakini kutokana na kutokuwa na mradi wa kuzalisha na kukuza wanariadha, haikuwezekana kuendelea kupata nyota wengine.
RT imekuwa ikitegemea taasisi za serikali kama Jeshi la Wananchi na Polisi kuzalisha wanariadha, badala ya kujikita katika mashindano ya shule za msingi na sekondari kupata wanariadha wachanga.
Hata michezo ya taifa ya riadha sasa ni kama haipo. Mchezo wa riadha haukusanyi mashabiki wengi wa kwenda kushuhudia nyota wao wakipambana kama ilivyokuwa miaka ya sabini. Hivi sasa ni marathoni tu ndio hujaza watu ambao ni washiriki wa mbio za kujifurahisha za kilomita tano.
Kwa hiyo ni wakati sasa kwa Chama cha Riadha kuzinduka na kuanza kutengeneza nyota wapya, kabla ya hawa kina Simbu na wenzake hawajastaafu. Medali ya dhahabu ya Simbu yafaa iwe kengele ya kuwaamsha na kutafuta mikakati mipya ya kuzalisha wanariadha hodari.