Historia yabakisha timu tano tu Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Takwimu hizo zinaonyesha kuwa ushindi wa Kombe la Dunia haujawahi kuwa jambo la bahati, bali matokeo ya mchanganyiko wa historia, ubora wa kikosi, uzoefu wa mashindano makubwa na mazingira yanayozunguka timu husika.
CHICAGO, MAREKANI: KOMBE la Dunia 2026 linakaribia kuanza huku mataifa 48 yakijiandaa kushindania taji kubwa zaidi katika soka. Lakini pamoja na ongezeko la timu, mechi na ushindani mkubwa kuliko wakati mwingine wowote, historia ya mashindano hayo inaonyesha kuwa idadi ya mataifa yenye nafasi kutwaa ya kutwaa ubingwa huo bado ni ndogo.
Katika kipindi cha miaka 96 tangu kuanzishwa kwa Kombe la Dunia mwaka 1930, ni mataifa manane pekee yaliyowahi kulibeba taji hilo.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa ushindi wa Kombe la Dunia haujawahi kuwa jambo la bahati, bali matokeo ya mchanganyiko wa historia, ubora wa kikosi, uzoefu wa mashindano makubwa na mazingira yanayozunguka timu husika.
Uchambuzi wa mwenendo wa mabingwa wa zamani unaonyesha kuwa kuna sifa kadhaa zinazofanana kwa karibu katika timu zote zilizowahi kutwaa ubingwa.
Kutokana na vigezo hivyo, mataifa mengi yameondolewa mapema kwenye orodha ya wanaowania taji na kubakisha timu tano tu ambazo historia inaonekana kuzipa nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa mwaka huu.
MABINGWA HUTOKA ULAYA AU AMERIKA KUSINI
Kigezo cha kwanza kinachotumiwa na historia ni eneo la kijiografia. Katika mashindano yote 22 yaliyopita ya Kombe la Dunia, hakuna taifa kutoka nje ya Ulaya au Amerika Kusini lililowahi kutwaa ubingwa.
Zaidi ya hilo, ni mataifa 13 pekee yaliyowahi kufika fainali ya Kombe la Dunia. Kati ya hayo, 10 yanatoka Ulaya huku matatu yakitoka Amerika Kusini.
Hii inaonyesha jinsi mabara hayo mawili yalivyoendelea kutawala soka la dunia kwa miongo mingi. Kutokana na rekodi hiyo, mataifa yote kutoka Afrika, Asia, Amerika Kaskazini na Oceania yanaonekana kuwa na mlima mkubwa wa kupanda ili kuvunja historia hiyo.
Hata wenyeji wa mashindano ya mwaka huu Marekani, Canada na Mexico wamejikuta wakiondolewa katika kundi la wagombea wakuu kwa kuzingatia mwenendo wa kihistoria.
Morocco ambayo ilivutia dunia kwa kufika nusu fainali mwaka 2022, inaonekana kuwa taifa lenye nafasi kubwa zaidi kuvunja utawala huo.
Mafanikio yao katika mashindano ya vijana na Olimpiki yanaonyesha maendeleo makubwa lakini bado wengi wanaamini safari ya kutwaa Kombe la Dunia inaweza kuwa mapema mno kwa kizazi hiki.
MTIANI WA VIWANGO NA UBORA
Kigezo kingine muhimu ni kiwango cha ubora wa taifa husika kabla ya mashindano kuanza. Takwimu za Elo Ratings, ambazo hutumiwa kupima nguvu za timu za taifa duniani, zinaonyesha kuwa hakuna nchi iliyowahi kutwaa Kombe la Dunia ikiwa nje ya nafasi 17 bora duniani wakati mashindano yanaanza.
Mfano pekee wa karibu na hilo ni Uruguay mwaka 1950 iliposhangaza dunia kwa kutwaa ubingwa nchini Brazil ikiwa katika nafasi ya 17.
Hadi leo ushindi huo unaendelea kutajwa kama moja ya maajabu makubwa zaidi katika historia ya soka. Kwa kawaida mabingwa wengi wamekuwa wakitoka ndani ya nafasi nne bora duniani kabla ya mashindano kuanza. Hilo linaonyesha kuwa Kombe la Dunia si sehemu ambayo timu za kawaida huibuka ghafla na kushinda kila kitu.
Kutokana na kigezo hicho, mataifa kama Paraguay, Austria, Scotland, Sweden, Czech na Bosnia-Herzegovina yanaondolewa kwenye hesabu za ubingwa licha ya kuwa na vikosi vyenye uwezo wa kufanya vizuri katika hatua za awali.
WACHEZAJI WALIOSHINDA BALLON D’OR
Kwa mataifa ya Ulaya, historia imeonyesha jambo lingine la kuvutia. Hakuna taifa la Ulaya lililowahi kushinda Kombe la Dunia bila kuwa na zaidi ya mchezaji mmoja aliyewahi kushinda tuzo ya Ballon d’Or katika historia yake.
Mantiki ya takwimu hiyo ni rahisi. Mataifa yanayozalisha wachezaji bora zaidi duniani mara nyingi ndiyo yanayokuwa na uwezo mkubwa wa kutwaa mataji makubwa ya kimataifa.Ufaransa ndiyo inaongoza kwa kuwa na wachezaji sita tofauti waliowahi kushinda Ballon d’Or.
Ujerumani na Italia zina watano kila moja, huku England ikiwa na wanne. Hispania, Uholanzi na Ureno zina washindi watatu kila moja.Kutokana na historia hiyo, baadhi ya mataifa yenye vipaji vikubwa lakini bila urithi mkubwa wa washindi wa Ballon d’Or yanaonekana kupoteza nguvu katika mbio za ubingwa.
KOCHA MZAWA NI FAIDA
Takwimu nyingine ya kuvutia ni kuhusu makocha. Hakuna taifa lililowahi kushinda Kombe la Dunia likiwa linaongozwa na kocha wa kigeni.
Ingawa baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa rekodi hiyo ni matokeo ya mataifa makubwa kuamini makocha wao wenyewe, bado imeendelea kudumu kwa karibu karne nzima. Mwaka huu Brazil inaongozwa na kocha raia wa Italia, Carlo Ancelotti, huku England ikiwa chini ya Mjerumani Thomas Tuchel.
Ureno inaongozwa na Mhispania Roberto Martínez, wakati Uruguay, Colombia na Ecuador nazo zina makocha wa kigeni. Kwa mujibu wa mwenendo wa kihistoria, hali hiyo inaonekana kuyapunguzia nafasi mataifa hayo licha ya kuwa na vikosi vyenye ubora mkubwa.
ZENYE NAFASI MBIO ZA UBINGWA
Baada ya kutumia vigezo vyote vya kihistoria, timu tano pekee ndizo zinazobaki katika orodha ya wagombea wakuu wa ubingwa wa Kombe la Dunia 2026.
Bingwa mtetezi Argentina anaendelea kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa kutokana na uzoefu, utamaduni wa ushindi na ubora wa kizazi chake cha sasa.
Ufaransa inaonekana kuwa moja ya timu kamili zaidi katika mashindano haya. Ikiwa na nyota kama Kylian Mbappé na kikosi kipana, wengi wanaiona kama mgombea namba moja wa ubingwa.
Ujerumani nayo haipaswi kubezwa. Taifa hilo limeonyesha uwezo wa kushinda katika nyakati tofauti za historia na limejijengea sifa ya kufanya vizuri katika mashindano makubwa.
Hispania inaingia ikiwa moja ya timu zinazocheza soka la kuvutia zaidi duniani kwa sasa. Mchanganyiko wa vijana wenye vipaji na uzoefu wa kimataifa unaifanya kuwa miongoni mwa vinara wa ubingwa.
Timu ya mwisho ni Uholanzi. Ingawa haijawahi kutwaa Kombe la Dunia, imefika fainali mara tatu na mara zote imekuwa karibu sana na ushindi. Kizazi cha sasa kinaonekana kuwa na uwezo wa kuandika historia mpya kwa taifa hilo.
JE, HISTORIA ITAENDELEA AU ITAVUNJWA?
Swali kubwa linalobaki ni kama Kombe la Dunia 2026 litaendelea kufuata mkondo wa historia au litashuhudia mapinduzi mapya.
Kwa miaka karibu 100, Kombe la Dunia limekuwa likithibitisha kuwa historia na takwimu zina uzito mkubwa kuliko matumaini ya mashabiki. Hata hivyo, kila kizazi huja na nafasi ya kuandika simulizi jipya.
Iwapo historia itaendelea kujirudia, basi bingwa wa Kombe la Dunia 2026 atatoka kati ya Argentina, Ufaransa, Ujerumani, Hispania au Uholanzi.
Lakini kama kutakuwa na mshangao mkubwa zaidi katika historia ya soka, basi dunia inaweza kushuhudia taifa jipya likiandika ukurasa mpya ambao haujawahi kuandikwa tangu mwaka 1930.