Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi ya familia 27, kuvunjwa Kombe la Dunia

FAMILIA Pict

Muktasari:

  • Jumla ya familia 27 za baba na mwana zimewahi kushiriki Kombe la Dunia kama wachezaji. Baadhi ya familia maarufu ni akina:Cesare Maldini na Paolo Maldini (Italia), Jean Djorkaeff na Youri Djorkaeff (Ufaransa), Pablo Forlán na Diego Forlan (Uruguay),Miguel Ángel Alonso na Xabi Alonso (Hispania) Pia wapo Mazinho na Thiago Alcantara (Brazil)

MIAMI, MAREKANI: Katika historia ya Kombe la Dunia ni familia 27 tu za baba na mwana ambazo zimewahi kuwakilishwa kucheza mashindano hayo, zikihusisha familia maarufu za soka kama akina Maldini, Thuram, Schmeichel, Forlan,a Alonso pamoja na Hernandez.

Kama ilivyokuwa kawaida rekodi zinawekwa ili kuvunjwa, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka nchini Marekani, Canada na Mexico mwaka huu, huku wachezaji kadhaa wakitarajia kuiga mafanikio ya baba zao kwa kuwakilisha mataifa yao kwenye Kombe la Dunia.

Jumla ya familia 27 za baba na mwana zimewahi kushiriki Kombe la Dunia kama wachezaji. Baadhi ya familia maarufu ni akina:Cesare Maldini na Paolo Maldini (Italia), Jean Djorkaeff na Youri Djorkaeff (Ufaransa), Pablo Forlán na Diego Forlan (Uruguay),Miguel Ángel Alonso na Xabi Alonso (Hispania) Pia wapo Mazinho na Thiago Alcantara (Brazil)

Peter Schmeichel na Kasper Schmeichel (Denmark), Claudio Reyna na Giovanni Reyna (Marekani), Lilian Thuram na Marcus Thuram (Ufaransa).


Familia kubwa zaidi kucheza Kombe la Dunia kwa vizazi tofauti inatoka Mexico ya akina Chicharito alianza babu Tomas Balcazar (1954), baba  Javier Nicolas Hernandez Gutierrez (1986) na mjukuu Javier Hernandez 'Chicharito' (2010).

Baba na mwana wa kwanza kushiriki Kombe la Dunia walikuwa Luis Pérez na Mario Pérez. Luis aliichezea Mexico katika Kombe la Dunia la 1930 nchini Uruguay, huku mwanawe Mario akiichezea Mexico katika Kombe la Dunia la 1950 nchini Brazil.

Pia, Jose Vantolrá, ambaye baba yake Martí Ventolrà aliichezea Hispania mwaka 1930, aliichezea Mexico katika Kombe la Dunia la 1970.

Familia ya Thuram imefanikiwa zaidi kwa upande wa medali. Lilian Thuram alitwaa medali ya dhahabu baada ya Ufaransa kushinda Kombe la Dunia la 1998, huku mwanawe Marcus Thuram akishinda medali ya fedha baada ya Ufaransa kumaliza nafasi ya pili katika Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.

Historia hii inaonyesha namna urithi wa soka unavyopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, huku watoto wengi wakifuata nyayo za baba zao na kufikia hatua ya juu kabisa ya mchezo huo duniani.

Katika fainali za mwaka huu tutashuhudia mwendelezo wa utamaduni maalum wa kifamilia katika jukwaa kubwa zaidi la soka duniani, huku wachezaji kama Giuliano Simeone, Justin Kluivert, Francisco Conceicao na Sebastian Berhalter wakifuata nyayo za baba zao ambao pia waliwahi kushiriki Kombe la Dunia.Hawa hapa wachezaji wanaoweza kuendeleza urithi wa familia zao katika Kombe la Dunia la FIFA 2026.

FAMIL 01

1. SEBASTIAN BERHALTER (MAREKANI)

BABA: GREGG BERHALTER

Sebastian Berhalter ameibuka kama mmoja wa vipaji vinavyokua kwa kasi katika soka la Marekani. Kiungo huyo aliingia katika kikosi cha timu ya taifa ya Marekani mwaka 2025 na kuimarisha nafasi yake ya kuitwa Kombe la Dunia baada ya kuwa na msimu bora akiwa na Vancouver Whitecaps.

Baba yake, Gregg Berhalter, aliichezea Marekani katika Kombe la Dunia la 2002 na 2006. Baadaye alirejea kama kocha wa timu ya taifa na kuiongoza Marekani kwenye Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.

Jambo la kuvutia: Gregg Berhalter ni mtoto wa ubatizo wa gwiji wa mchezo wa baseball, Carl Yastrzemski.

FAMIL 02

2. FRANCISCO CONCEICAO (URENO)

BABA: SERGIO CONCEIÇAO

Mmoja wa vipaji bora vya ushambuliaji nchini Ureno, Francisco Conceicao amejijengea sifa kwa kasi yake kubwa na uwezo wa kupiga chenga.

Winga huyo alijitangaza kimataifa kwa kufunga bao la ushindi dhidi ya Czech katika mashindano ya Kombe la Euro 2024 na akaendelea kung'ara kwa kufunga tena dhidi ya Ujerumani katika UEFA Nations Ligi.

Baba yake Sergio aliwakilisha Ureno katika Kombe la Dunia la 2002.

Jambo la kuvutia: Watoto watatu kati ya watano wa Sergio Conceicao wamekuwa wachezaji wa kulipwa.

FAMIL 03

3. LEE TAE-SEOK (KOREA KUSINI)

BABA: LEE EUL-YONG

Lee Tae-seok anaendelea kujijenga kama mmoja wa mabeki wenye matumaini makubwa nchini Korea Kusini.

Beki huyo wa pembeni wa Austria Vienna ameonyesha uwezo mkubwa wa kusaidia mashambulizi na hivi karibuni alifunga bao la ushindi katika mechi dhidi ya Ghana.

Baba yake, Lee Eul-yong, alikuwa sehemu kikosi cha timu ya Korea Kusini iliyoshiriki Kombe la Dunia la 2002 na 2006.

Jambo la kuvutia: Lee Eul-yong aliwahi kufanya kazi kwenye klabu ya usiku akiwa kijana kabla ya kuwa mchezaji wa kulipwa akiwa na miaka 23.

FAMIL 04

4. ANGUS GUNN (SCOTLAND)

BABA: BRYAN GUNN

Kipa namba moja wa Scotland, Angus Gunn, anaelekea kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia baada ya kubadili uraia wa kisoka kutoka England kwenda Scotland.

Baba yake Bryan Gunn alikuwa sehemu ya kikosi cha Scotland katika Kombe la Dunia la Italia 1990, ingawa hakupata nafasi ya kucheza.

Jambo la kuvutia: Bryan Gunn anaripotiwa kumvisha pete ya uchumba wake ambaye ni mama wa Angus saa 48 tu baada ya kukutana naye wakati wa likizo nchini Hispania.

FAMIL 05

5. ERLING HAALAND (NORWAY)

BABA: ALF-INGE HAALAND

Ni wachezaji wachache wanaokwenda Kombe la Dunia wakiwa na matarajio makubwa kama Erling Haaland.

Akiwa tayari ni mmoja wa wafungaji bora zaidi duniani, Haaland ameisaidia Norway kurejea Kombe la Dunia baada ya miaka 28 ya kusubiri. Baba yake, Alf-Inge Haaland, aliwakilisha Norway katika Kombe la Dunia la 1994 nchini Marekani.

Jambo la kuvutia: Erling alikua mchezaji wa sita katika historia ya soka kufikisha mabao 50 ya kimataifa akiwa amecheza chini ya mechi 50.

FAMIL 06

6. JUSTIN KLUIVERT (UHOLANZI)

BABA: PATRICK KLUIVERT

Justin Kluivert alikuwa na msimu bora akiwa na AFC Bournemouth, jambo lililomsaidia kujihakikishia nafasi katika timu ya taifa ya Uholanzi.

Baba yake Patrick Kluivert aliing'ara katika Kombe la Dunia la 1998, akifunga mabao muhimu dhidi ya Argentina na Brazil huku Uholanzi ikifika hatua ya nusu fainali.

Jambo la kuvutia: Patrick ana urefu wa mita 1.91, wakati Justin ana urefu wa mita 1.72.

FAMIL 06 (1)

7. GIULIANO SIMEONE (ARGENTINA)

BABA: DIEGO SIMEONE

Giuliano Simeone amekuwa mmoja wa vijana wanaovutia zaidi katika kikosi cha Argentina.

Winga huyo wa Atletico Madrid amepewa nafasi za mara kwa mara na kocha Lionel Scaloni na aliwahi kufunga katika ushindi mkubwa wa Argentina dhidi ya Brazil kwenye mechi za kufuzu.

Baba yake Diego Simeone alicheza Kombe la Dunia mara tatu akiwa na Argentina na alikuwa nahodha wa timu hiyo mwaka 1998.

Jambo la kuvutia: Diego Simeone alikuwa akiandaa milo ya kifamilia kwa njia ya mtandao akiwa nje ya nchi huku wanawe wakifuatilia ndoto zao za soka.

FAMIL 08

8. KRISTIAN THORSTVEDT (NORWAY)

BABA: ERIK THORSTVEDT

Kristian Thorstvedt amekuwa mhimili muhimu wa safu ya kiungo ya Norway baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa na US Sassuolo.

Baba yake Erik Thorstvedt alikuwa kipa wa Norway katika Kombe la Dunia la 1994 na aliisaidia timu hiyo kuruhusu bao moja tu katika hatua ya makundi. Jambo la kuvutia: Kristian na Erling Haaland wanaweza kuwa watoto wa kwanza wa wachezaji waliowahi kucheza pamoja Kombe la Dunia ambao nao watacheza pamoja kwenye Kombe la Dunia.

FAMIL 09

9. LUCA ZIDANE (ALGERIA)

BABA: ZINEDINE ZIDANE

Mwana wa mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya soka anaweza kuandika simulizi yake mwenyewe kwenye Kombe la Dunia.

Luca Zidane aliwakilisha Ufaransa katika ngazi za vijana kabla ya kubadili uraia na kujiunga na Algeria. Kipa huyo wa Granada CF alicheza mechi yake ya kwanza ya timu ya taifa mwaka 2025 na sasa analenga kuisaidia Algeria kung'ara duniani.

Baba yake, Zinedine Zidane, aliiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 na kuifikisha fainali nyingine mwaka 2006.

Jambo la kuvutia: Zinedine Zidane alifanikiwa kupita kwa chenga mara zote 11 alizojaribu dhidi ya Brazil katika robo fainali maarufu zaidi ya Kombe la Dunia 2006.