Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki ndicho kimechangia Simba na Azam kuanza vibaya makundi CAF


WAKATI Yanga ikiendelea kuiwakilisha nchi vyema kwenye michuano ya CAF msimu huu kwa kutoruhusu bao kwa dakika 180, wawakilishi wengine kutoka Simba, Azam na Singida Black Stars zimeruhusu nyavu zao kutikiswa. Timu zote zimecheza mechi mbili za makundi.


Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi nne na bao moja kundi B, watani zao wa jadi Simba inayoshiriki pia michuano hiyo ikipangwa kundi D, inaburuza mkia kutokana na kupoteza mechi zote mbili, imefunga bao moja na kuruhusu matatu.


Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC iliyopo kundi B haijavuna pointi wala bao ikiruhusu matatu, huku Singida iliyopo kundi C ikivuna pointi moja ikifunga bao moja na kuruhusu matatu.

Katika michuano hiyo, kila timu imekuwa na udhaifu wake kwenye baadhi ya maeneo na kusababisha kushindwa kupata ushindi mnono au kukosa kabisa, jambo linalotakiwa kufanyiwa marekebisho wakati huu kabla ya kuendelea Januari 2026.

CA 01

CHANGAMOTO

Tangu Simba inaanza mechi ya kwanza ya kundi dhidi ya Petro De Luanda, iliitawala mechi hiyo, ilitengeneza mashambulizi vizuri lakini changamoto ilikuwa kwenye kuzigeuza kuwa mabao.

Kwenye mechi hiyo ya kwanza, Simba ilipiga mashuti saba karibu na lango la wapinzani, kama wachezaji wangekuwa na utulivu, ingepata ushindi, lakini haikuwa hivyo. Pia ilipata nafasi mbili kubwa ikashindwa kuzitumia.

Simba ilipiga pasi 324 sahihi kutoka kwa mchezaji mmoja kwenda kwa mwingine, lakini hakukuwa na umaliziaji mzuri kwenye eneo la mwisho.

Benchi la ufundi la Simba ni kama halikufanya uchambuzi mzuri wa wapinzani wao, kuingia uwanjani na viungo wengi bila ya mshambulaji halisi, iliwagharimu pakubwa. Viungo hao ni Naby Camara, Alassane Kante, Morice Abraham, Neo Maema, Joshua Mutale na Elie Mpanzu aliyetumika kama namba tisa wa uongo.

Mechi dhidi ya Stade Malien, Simba pia ilicheza vizuri lakini haikuwa bora kwenye maeneo mawili ya ulinzi na eneo la ushambuliaji.

Stade Malien ilikuwa inafika zaidi eneo la ulinzi la Simba ilionekana lilikuwa eneo rahisi kufikika, wapinzani walitengeneza nafasi 15 na kupiga mashuti 12 ndani ya boksi la wekundu hao wa Msimbazi.

CA 06

Stade Malien ilitumia mashambulizi ambayo timu inasogea moja kwa moja kuelekea lango la mpinzani kwa kasi wakipiga mipira ya haraka nyuma ya mabeki wa kati, Wilson Nangu na De Reuck. Pia ilitumia mipira ya juu kutokana na vimo virefu vya nyota wao.

Simba ilikuwa bora eneo la kati hasa Naby Camara anapokuwa na mpira lakini zile pasi ndefu alizokuwa anapiga hazikutendewa haki na waliokuwa mbele, Seleman Mwalimu aliyesimama kama mshambuliaji wa mwisho, Elie Mpanzu, Joshua Mutale na Jean Charles Ahoua.

Mnyama alipiga mashuti 14, lakini manne pekee yalilenga lango la mpinzani. Joshua Mutale hakuwa mtulivu kufanya maamuzi anapokuwa ndani ya boksi.

Kijumla mechi zote mbili Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 62, ilipiga mashuti 25, kati ya hayo 14 yalipigwa ndani ya boksi na matano yakilenga lango la wapinzani. Simba imekosa nafasi tano kubwa za wazi na jumla ilitengeneza nafasi 21 za wazi za kufunga.

CA 02

Kwa upande wa Yanga, kwenye mechi mbili imeibuka kama shujaa wa Tanzania, haijapoteza baada ya kuitandika AS FAR Rabat bao 1-0 nyumbani na kuambulia pointi moja ugenini dhidi ya JS Kablyie ya Algeria zilipotoka 0-0.

Mechi ya kwanza dhidi ya AS FAR Rabat iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga ilipiga mashuti 15 dhidi ya matano, ilifika ndani ya boksi mara 11 kwa nne za wapinzani.

Kwenye kutengeneza nafasi, Yanga ilifanya mara 13 kwa tano, hata hivyo ilikosa nafasi mbili kubwa za wazi. Kwa ufupi ilikuwa na uwezo wa kushinda kwa mabao mengi.

Kipa wa Yanga, Djigui Diarra alifanya sevu moja huku kipa wa AS FAR Rabat, Ahmed Reda akiokoa mara nane. Umakini mdogo katika kumalizia, uliifanya Yanga kupata ushindi huo wa bao 1-0.

Mechi ya pili ikiwa ugenini, Yanga ilipiga mashuti 11, matatu yakiwa ndani ya boksi huku pia matatu yakilenga lango, ilikosa nafasi moja kubwa ya wazi kutoka kwa Celestin Ecua, Diarra aliokoa mipira sita ya hatari.

CA 05

Pamoja na mwanzo mzuri, lakini Yanga bado ina changamoto ya kumalizia nafasi inazotengeneza, pia bado kuna changamoto kwenye kutumia vizuri mipira ya kona na faulo.

Azam imeanza kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa AS Maniema ya DR Congo. Kwenye mechi hiyo, Azam ilipiga mashuti 15 karibu na lango la wapinzani dhidi ya matano ya AS Maniema ambayo yalilenga lango.

Kikosi hicho cha Azam kinachonolewa na Florent Ibenge, kilipiga mashuti mengi lakini kilishindwa kulenga sahihi, changamoto ya kumalizia nafasi na utulivu inaonyesha kuwatesa.

Azam ilipiga mashuti matatu tu yaliyolenga lango, huku Maniema ikipiga matano na mawili yakitikisa nyavu, changamoto inaonekana kwa mchezaji wa mbele na viungo wanapaswa kuwa makini zaidi katika kumalizia nafasi.

CA 03

Kwenye mechi ya pili dhidi ya Wydad AC, Azam ilirudia makosa yaleyale, ilipiga mashuti 20 na manne pekee yalilenga lango.

Hii inaonyesha kuwa Azam ilikuwa bora katika kudhibiti mpira na kushambulia, lakini inahitaji kuboresha sehemu ya mwisho kutumia nafasi kwani ina uwezo wa kuzitengeneza.

Kwa Singida, mechi ya kwanza ilifungwa 2-0 dhidi ya CR Belouizdad ugenini, mabao ya mapema dakika ya tano na 14 yaliwavuruga.

Belouizdad ilianza kwa nguvu na mabao ya mapema yaliibeba timu hiyo, Singida ilihitaji utulivu kujibu mashambulizi, lakini ilikutana na timu inayocheza kwa mipango na uzoefu mkubwa.

Kwenye mechi ya pili dhidi ya Stellenbosch iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Singida ilipiga mashuti 21 dhidi ya manne ya Stellenbosch. Mashuti yaliyolenga goli Singida yalikuwa saba, wakati Stellenbosch yalikuwa matatu. Takwimu zinaonyesha Singida ilipiga pasi 576, ikionyesha ilidhibiti mpira vizuri.


MTIHANI ULIOBAKI

Kushindwa kukusanya pointi kwa Azam katika kundi C huku kinara Wydad na Maniema zikiwa na pointi sita, inalifanya kundi hili kuwa gumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania. Pia Nairobi United ya Kenya haina pointi.

CA 04

Mechi nne zilizobaki, Azam ina mtihani mkubwa kuhakikisha inakusanya pointi nyingi kwa kuanza na Nairobi United itakayocheza nayo mechi mbili mfululizo. Januari 25, 2026 ugenini na Februari 1, 2026 nyumbani. Baada ya hapo, itaikaribisha Maniema, na kumalizia ugenini kwa Wydad.

Azam haitakiwi kupoteza mechi yoyote kati ya mbili zijazo, ikipoteza hata moja, itakuwa imepotea njia.

Singida pointi moja ya juzi ni kama imewabeba kwani tofauti yake na kinara wa kundi C, Stellenbosch ni pointi tatu kwani inazo nne.

Mechi nne zilizobaki, itacheza mbili mfululizo na AS Otohô ikianzia nyumbani kisha ugenini nchini Congo. Hizo ndiyo mechi za kujiweka pazuri kwa kushinda kwani baada ya hapo itaikaribisha CR Belouizdad na kuifuata Stellenbosch mechi ya mwisho.

Mtihani wa Singida unakuja kutokana na wapinzani wake wote wameshinda nyumbani mechi walizocheza, yenyewe tu imeshindwa kufanya hivyo, jambo ambalo linazidi kuifanya kuumiza kichwa inapokwenda kukabiliana na AS Otohô na Stellenbosch huko kwao.

Simba ili kufufua matumaini, ina mtihani mzito mbele ya Espérance ya Tunisia katika mechi mbili zijazo, ikianzia ugenini kisha nyumbani.

Mbaya zaidi ni kwamba, Esperance imekuwa na matokeo mazuri inapokuwa nyumbani, msimu huu pekee katika mechi tatu za nyumbani kuanzia hatua za awali, imeshinda mbili na sare moja, imefunga mabao saba na kuruhusu moja pekee.

Baada ya hapo, itaifuata Petro de Luanda, timu ambayo msimu huu imeshinda mechi tano na sare moja kati ya sita ilizocheza, ikifunga mabao 12 na kuruhusu moja. Itamaliza makundi nyumbani dhidi ya Stade Malien.

Kocha wa Simba, Dimitar Pantev, muda mfupi baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Stade Malien na kupoteza kwa mabao 2-1, alisema: “Sio rahisi kuzungumza baada ya mechi kama hii. Sitafuti kujitetea. Najua kila mchezaji amejitahidi. Labda haukuwa mchezo wetu. Haikuwa siku yetu.

Pantev raia wa Bulgaria aliyetua Simba Oktoba 6, 2025, siku chache baada ya klabu hiyo kuachana na Msauzi, Fadlu Davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco, ameendelea kwa kusema: “Hata hivyo tangu nimefika hapa nimekuwa nikieleza kuwa kuna mchakato.

“Naamini katika mchakato huu, naamini hata watu wengine wanaoiendesha hii klabu wanaamini kwenye mchakato huu kwa sababu walinileta hapa kujaribu kubadilisha kitu kwenye timu. Miezi miwili haitoshi, lakini timu kama Simba hakuna muda siku sita, kumi au karibia 15.”

Pantev alibainisha, katika maandalizi kuelekea mechi hizo mbili za kwanza hatua ya makundi, kikosi kilifanya mazoezi muda mwingi kikiwa na wachezaji wachache kutokana na uwepo wa Kalenda ya FIFA, hivyo hilo kwa kiasi fulani limechangia matokeo mabaya lakini anaamini watarudi wakiwa imara zaidi.

“Tumefanya mazoezi bila wachezaji waliokuwepo timu ya taifa. Wamekuja muda mfupi. Najua kila mtu amechukia hususani mashabiki. Nawaelewa kwa sababu wana matarajio makubwa. Natumaini kila mchezaji na viongozi tutafanya bidii na kuja na kiwango bora kwa siku zijazo.

“Unajua tatizo hili si la sasa. Ni la muda mrefu. Hata kwenye mechi zilizopita za CAF hatukufunga. Na nilipofika haijawa rahisi kufunga. Kama hufungi huwezi kukusanya alama.”

Mwisho Pantev amewaangushia zigo wachezaji akisema kikosi cha Simba kina ubora kushinda wapinzani wao, lakini walicheza chini ya kiwango.

“Tatizo kubwa wachezaji wetu wengi wamecheza chini ya kiwango chao. Timu yetu ina ubora mkubwa kuliko timu ya wenzetu. Nimechukia kwa sababu tumeshindwa kufunga. Lakini ndio mpira,” alisema Pantev.

Yanga inahitaji kushinda mechi mbili za nyumbani zilizobaki kati ya nne itakazocheza ili kufikisha pointi 10 ambazo zitaiweka sehemu nzuri ya kucheza robo fainali. Kumbuka michuano ikiendelea, itakutana na Al Ahly ikianzia ugenini kisha nyumbani. Timu hizo ndizo zipo pale juu kwenye msimamo.