Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Henry David aweka wazi mastaa anaowakubali Ligi Kuu

Muktasari:

  • Miongoni mwao ni Henry David, raia wa Nigeria anayekipiga Singida Black Stars baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita akiwa Fountain Gate kisha akatua kwa walima alizeti.

KAMA kuna kitu kinachoongeza ladha katika Ligi Kuu Bara msimu huu, basi ni uwepo wa mastaa kutoka mataifa mbalimbali waliokuja Tanzania kuonyesha uwezo.

Miongoni mwao ni Henry David, raia wa Nigeria anayekipiga Singida Black Stars baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita akiwa Fountain Gate kisha akatua kwa walima alizeti.

Henry si mgeni kabisa katika soka la Tanzania. Uzoefu alioupata msimu uliopita umemsaidia kuifahamu ligi, mazingira yake pamoja na namna ambavyo mashabiki wanavyolipenda soka.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Henry amezungumza mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake mapya Singida Black Stars, ushindani wa namba, mastaa anaowakubali kwenye ligi na chakula anachokipenda zaidi.

SINGIDA

Henry anasema kuhamia Singida Black Stars ni hatua mpya katika safari yake ya soka, hasa kutokana na ukubwa wa klabu hiyo na matarajio yaliyopo ndani yake.

Anakiri kuwa mazingira aliyoyakuta ni tofauti na yale aliyoyazoea, lakini anaona hilo kama changamoto nzuri inayoweza kumsaidia kupiga hatua nyingine katika maisha yake ya soka.

“Kuja hapa ni uzoefu mpya kwangu kwa sababu Singida ni timu kubwa, kwa hiyo ni ngazi nyingine kabisa hapa. Ni changamoto nzuri na nina furaha kubwa kuwa hapa,” anasema Henry.

Winga huyo anaongeza kuwa sehemu ya mafanikio ya timu na kuonyesha uwezo wake kila anapopata nafasi ya kucheza.


VITA YA NAMBA?

Singida Black Stars ina kikosi chenye wachezaji wengi wenye uwezo, jambo linalofanya ushindani wa kupata nafasi ya kucheza kuwa mkubwa.

Lakini, Henry hana presha na hali hiyo kwake anaiona kama fursa ya kila mchezaji kuongeza kiwango hususani yeye mwenyewe anayependelea ushindani wa namba.

“Tuna kikosi kipana na tuna wachezaji wengi wazuri sana kwenye timu. Kila mchezaji anapaswa kupandisha kiwango chake ili apate nafasi ya kucheza,” anasema.

Anaongeza :“Kwenye nafasi yangu kuna wachezaji wengi wazuri na wa ajabu, kwa hiyo njia bora ya kucheza ni kuendelea kufanya vizuri tu. Ukifanya vizuri, hakika utacheza.”

Winga huyo anasema angalau ameanza kuzoea mazingira na tayari amepata marafiki ambao ni Benjamin Tanimu na Marcel.

FEI TOTO ANAMKOSHA

Moja ya sehemu zinazovutia zaidi kwenye mahojiano hayo ni pale Henry alipoulizwa kuhusu wachezaji anaowakubali zaidi kwenye Ligi Kuu.

Jina la kwanza alilolitaja ni Feisal Salum ‘Fei Toto’, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, ambaye Henry anasema anamvutia tangu alipofika Tanzania.

“Tangu nilivyokuja nchi hii, nimekuwa nikiangalia mechi za Azam na yeye amekuwa mchezaji bora na wa kipekee zaidi uwanjani mimi ni shabiki wake mkubwa sana,” anasema.

Henry amekuwa akifuatilia kwa karibu namna Fei Toto anavyocheza, hasa uwezo wake wa kutengeneza nafasi na kuwa hatari dhidi ya wapinzani.


CHAMA LEJENDARI

Mwingine ni Clatous Chama ambaye Henry amempa heshima yake kwake Mzambia huyo si mchezaji wa kawaida kutokana na kile alichokiona baada ya kupata nafasi ya kumshuhudia akicheza.

“Chama ni kama lejendari hivi. Nilikuwa nasikia habari zake tangu nilipofika hapa, lakini nilipomshuhudia akicheza niliona wazi kabisa ni kwa nini anaitwa lejendari nchini hapa,” anasema.

Henry anaongeza kuwa Chama ni miongoni mwa wachezaji ambao anavutiwa nao kutokana na uwezo wake wa kucheza na uzoefu alioujenga katika soka.


SHEKHAN ANAMKUBALI

Kiungo Shekhan Khamis ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao msimu huu wametolewa kwa mkopo Singida na tayari ameonyesha kiwango bora.

Henry anasema Shekhan ana uwezo mkubwa wa kucheza na ana mguso mzuri wa mpira. “Ni mchezaji mwenye maajabu yake miguuni naamini yuko sehemu salama ya kuonyesha uwezo wake na anastahili tuzo ya mchezaji bora wa mwezi.”


HAWAFUATILII WAPINZANI

Henry amefichua kwamba yeye si mtu anayependa kutumia muda mwingi kufuatilia majina ya wachezaji wa timu pinzani labda wale wachezaji maarufu.

“Mimi kwa kweli sijui mengi kuhusu wachezaji wa timu zingine. Huwa ninaangazia zaidi timu yangu,” anasema.

“Hata tunapocheza dhidi ya wapinzani wetu, huwa siangalii au kufuatilia mambo yao au kujua majina yao. Ni ngumu kwangu kutaja majina ya wachezaji wa timu pinzani, najua wachache tu.”

TANZANIA AU NIGERIA?

Henry pia amefafanua kuhusu maisha yake nje ya soka, akieleza namna anavyoupenda utamaduni wa Tanzania, hasa mapenzi makubwa ambayo Watanzania wanaonyesha kwenye soka.

“Njia ambayo watu wanapenda soka hapa ni ya kushangaza sana. Ni nadra sana kupata mapenzi na uungaji mkono mkubwa namna hii katika maeneo mengine barani Afrika,” anasema.

Kuhusu chakula, Henry anasema kuwa anavipenda vyakula vya Tanzania, lakini bado vile vya Nigeria ni vizuri zaidi.

“Vyakula vya hapa ni vizuri, lakini napendelea zaidi chakula cha Nigeria. Nigeria ndio bora zaidi. Chakula cha Nigeria ni cha kiwango kingine kabisa,” anasema huku akicheka.


MALENGO YAKE

Henry anasema malengo msimu huu ni kunisaidia timu kufanya vizuri mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Henry anatamani kujitoa msimu huu kuonyesha uwezo wake zaidi, akiamini kuwa Singida Black Stars inaweza kuwa sehemu ya mafanikio makubwa kwake na kwa klabu. Lengo lake ni kusaidia timu kwa kufunga mabao, kutoa pasi za mwisho na kufanya kazi ambayo itamfanya awe mchezaji muhimu ndani ya kikosi.