Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DADDY FRANCIS: Kutoka kukata tamaa Bara hadi kuwaka Zenji

Muktasari:

  • Watu wa namna hiyo hupata nguvu mahali ambapo walidhani wamebaki dhaifu na kugundua kwamba yale yaliyowaumiza yalikuwa yakiwatengeneza kuwa wenye uwezo wa kubeba ndoto zao.

WAKATI mwingine watu hufikiria kila kitu kimekwisha, na hapo ndipo maisha yanapotoa nafasi nyingine ya kuanza upya kwa kufungua milango ambayo waliamini ilikuwa imefungwa.

Watu wa namna hiyo hupata nguvu mahali ambapo walidhani wamebaki dhaifu na kugundua kwamba yale yaliyowaumiza yalikuwa yakiwatengeneza kuwa wenye uwezo wa kubeba ndoto zao.

Cha kushangaza ni kwamba, hata katika nyakati ngumu, maisha hutoa fursa nyingine ya kujifunza kutokana na makosa na kuendelea na safari, kwa sababu kushindwa si mwisho wa ndoto, bali ni sehemu ya safari.

Hilo linathibitishwa na kiungo mshambuliaji wa Chipukizi, Daddy Francis ambaye katika mechi tatu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) dhidi ya Black Sailors, Uhamiaji na JKU ameonekana kufanya vizuri licha ya kikosi hicho kutopata matokeo mazuri huku akiwa tayari amefunga bao moja.

Mwanaspoti ambalo limekuwa likishuhudia mechi za Ligi Kuu Zanzibar na kufika viwanja vya mazoezi, limemshuhudia nyota huyo akiwa na kikosi cha Chipukizi kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Sumait wakiendelea kujiandaa na mechi za ligi hiyo.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, mbali na mambo mengine, Daddy anaelezea namna alivyokata tamaa na soka hadi kufanikiwa kurejea uwanjani kupambana kuisaidia Chipukizi, licha ya timu hiyo kutoanza vizuri Ligi Kuu Zanzibar ambapo mechi tatu za kwanza, imetoka sare moja na kupoteza mbili.

KILICHOMKATISHA TAMAA

Daddy ni mzaliwa wa Kilombero mkoani Morogoro. Anasema mwaka 2025 alipata jeraha la mshipa wa ndani ya nyonga na kukaa nje ya uwanja kwa miezi tisa, hadi rafiki yake, Rahimu Shomari, alipoamua kumtibia ili aweze kurejea uwanjani.

Anasema baada ya kupata jeraha hilo alifikiria kuacha soka, lakini Rahimu alimsihi ajipumzishe na kurejea tena kwa sababu bado alikuwa na uwezo wa kucheza soka la kulipwa.

Daddy anaeleza kuwa, si jeraha pekee lililotaka kuzima ndoto zake, bali hata kukosa watu sahihi wa kumsimamia katika safari yake kuliyumbisha ndoto hizo.

Anasema wengi waliishia kumpa pongezi kwa kuwa na kipaji na kumsifia kwa namna yake ya uchezaji, badala ya kumsaidia kumshika mkono ili kutimiza ndoto zake.


GAMERA AMUIBUA UPYA

Kiungo huyo anasema awali hakupata kocha mwenye taaluma ya ukocha, kwani wengi aliokutana nao walikuwa makocha wa mitaani. Hata hivyo, kwa sasa amempata Suleiman Mohammed ‘Mani Gamera’, ambaye anamuongoza vizuri na tayari anaona mabadiliko katika kiwango chake.

Anasema Gamera ndiye aliyefanikiwa kumrudisha kwenye soka baada ya kumfuata nyumbani kwao Morogoro, aliposikia kuhusu uwezo wake, kisha kumleta Pemba kujiunga na Chipukizi, timu anayochezea kwa sasa.

“Kocha Gamera amekuwa na mchango mkubwa sana kwangu. Ameniamini hadi kunifuata nyumbani baada ya kusikia uwezo wangu na kunipa fursa ya kuendeleza kipaji changu,” anasema.

MKAMBA RANGERS TIMU ILIYOMTOA

“Nilianza kucheza soka nikiwa na umri wa miaka 13 katika Akademi ya Serengeti Boys iliyopo Kilombero mkoani Morogoro. Nilivutiwa na uchezaji wa mshambuliaji Aritz Aduriz (mshambuliaji wa zamani wa Hispania na Athletic Club), ingawa kwa sasa amestaafu, pamoja na Salumu Kihimbwa wa Mashujaa,” anasema Daddy.

Daddy ambaye ana uwezo wa kucheza winga, mshambuliaji wa mwisho na namba 10, anasema alilelewa katika mazingira ambayo wazazi wake walihitaji asome. Hata hivyo, baba yake pia alimpa ushauri na kumuhimiza kusimamia kipaji chake.

Baada ya kutoka Akademi ya Serengeti Boys, timu ya Mkamba Rangers, iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Pili, ndiyo iliyotambulisha kipaji chake.

Kocha wa timu hiyo alimuona mtaani na kumpa nafasi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Toto African, ambako alifanikiwa kufanya vizuri.

Wakati akiwa Mkamba Rangers, Daddy anasema alifungua ukurasa wa matumaini katika soka baada ya kufunga mabao mawili kwenye mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Cosmopolitan.

Anasema mabao hayo yalimpa imani kwamba anaweza kupata mafanikio kupitia soka.


MECHI ZA KUMBUKUMBU

Anasema akiwa anaichezea Yosso Boys mwaka 2021 katika Kombe la Mapinduzi, walifungwa mabao 5-1, lakini bao pekee la timu yao yeye ndiye alifunga, jambo analoliona kuwa sehemu ya fahari katika historia yake ya soka.

Pia anasema katika mechi ya kirafiki baina ya Mkamba Rangers na Yanga mwaka 2018, iliyokuwa chini ya Kocha Mwinyi Zahera, alionesha kiwango kizuri kilichomvutia kocha huyo hadi kutaka kumsajili katika timu ya vijana ya Yanga.

Hata hivyo, viongozi wa Mkamba Rangers walimzuia ili aisaidie timu hiyo kupanda daraja.

Anasema katika mechi hiyo alicheza dhidi ya mabeki kama Kelvin Yondan na Andrew Vicent Chikupe.

CHANGAMOTO

Anasema kipindi alipojiunga na timu ya Mbuni ya Arusha ikiwa inashiriki Ligi Daraja la Pili hakudumu hata mwezi mmoja kutokana na changamoto za mfumo wa kocha na mazingira ya klabu, hali iliyomfanya aamue kuondoka ili kulinda kiwango chake.

Daddy anasema baada ya kupitia misukosuko hiyo alijikuta akiwa muumini wa kucheza mashindano ya mtaani maarufu kama ndondo kwa sababu ya kupata fedha za haraka na ndani ya muda mfupi.

Lakini baada ya kukutana na Gamera, kiungo huyo mshambuliaji ametambua kuwa nidhamu ya soka la ligi ndiyo njia pekee ya kumjenga kuwa mchezaji wa kiwango cha juu, na si mashindano ya Ndondo.

“Hapo awali nilikuwa napenda kucheza ndondo kwa sababu ya pesa za haraka, lakini sasa nimetambua kuwa ligi rasmi ndiyo fursa pekee ya kunifikisha kwenye soka la kulipwa na kupata mafanikio ya muda mrefu,” anasema Daddy.


NDOTO YA KUCHEZA LIGI KUU BARA

Anasema kwa sasa anapambana ili katika dirisha dogo aweze kupata timu Tanzania Bara. Hilo ni miongoni mwa malengo na ndoto zake, hivyo anajipanga kufunga mabao na kuonesha kiwango kizuri.

Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, Daddy anasema anafanya mazoezi binafsi, ikiwemo kukimbia ufukweni, kwa lengo la kuongeza stamina na utulivu kabla ya mechi.


TIMU ALIZOCHEZA

Daddy amefanikiwa kucheza katika timu za Mkamba Rangers, Area C, Simba B, African Lyon, Mbuni, Yosso Boys na sasa Chipukizi.