Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatua 5 zingezuia utata dili la Kagoma

Muktasari:

  • Je, kwanini vitu kama hivi vinajitokeza kwa wingi kwenye madirisha ya usajili hapa nchini? Makala haya yanahusu hatua tano muhimu kwa klabu kuzifuata kwenye usajili wa mchezaji mpya ili kuepuka sintofahamu za aina hiyo ambazo si tu zinaharibu taswira ya soka nchini kwa ujumla.

KIUNGO mkabaji, mzawa Yusuf Kagoma amekuwa maarufu kwa siku za hivi karibuni baada ya jina lake kuhusishwa kwenye utata wa usajili akitokea klabu ya Fountain Gate.

Simba ilinasa huduma ya mchezaji huyo kabla ya mahasimu wao Yanga kuibuka na kudai kuwa na dili naye. Hata hivyo, baada ya shauri hilo kusikilizwa na mamlaka husika, Shirikisho la Soka Tanzania kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, kiungo huyo ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa kazi anayopiga uwanjani, amethibitishwa kuichezea Simba kwa msimu huu wa 2024/2025.

Katika dirisha kubwa la uhamisho wa wachezaji hapa nchini, sakata jingine kama hilo limetokea kwa beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi, ambaye pia alidaiwa kusainiwa na Simba, ukiweka kando sekeseke la kumhusu kiungo Awesu Awesu kutoka KMC kwenda Simba pia.

Mbali na sakata la wachezaji hao, lakini misimu miwili iliyopita ilitokea mzozo kama huo kwa Habib Kyombo aliyekuwa amesajiliwa Singida Fountain Gate na Simba kwa pamoja kutoka Mbeya Kwanza, kabla ya klabu hizo mbili kumalizana kiungwana kwa Singida kuwaachia Wekundu mchezaji huyo.

Je, kwanini vitu kama hivi vinajitokeza kwa wingi kwenye madirisha ya usajili hapa nchini? Makala haya yanahusu hatua tano muhimu kwa klabu kuzifuata kwenye usajili wa mchezaji mpya ili kuepuka sintofahamu za aina hiyo ambazo si tu zinaharibu taswira ya soka nchini kwa ujumla.

1. Kumfanyia uskauti mchezaji

Hii mara zote inaanza kabla ya dirisha halijafunguliwa, ambapo mchezaji anafuatiliwa kutambua ubora wake wa uwanjani, lakini pia skauti hao wanajaribu kutafuta uhusiano mzuri na timu yenye mchezaji ambaye wanamtaka ili kuwepo na urahisi wa michakato inayofuata.

Kipindi hicho cha awali cha kutambua uwezo wa mchezaji ni muhimu kwelikweli, ambapo kwa sasa klabu mbalimbali zimekuwa zikitumia programu maalumu kwenye kompyuta kutafuta takwimu halisi za mchezaji husika na uchambuzi wake.

Na kwa kipindi hiki za kizazi cha intaneti, makocha na wakurugenzi wa soka wanapata fursa ya kutazama video za mchezaji husika kwenye mechi alizocheza ili kutambua uwezo wake.

Klabu nyingi kubwa zinatumia takwimu za mtandaoni kwa wachezaji inaowasaka kwa muda mrefu na inafanya haraka kwenda kupeleka ofa ikichambua kwamba anaweza kupatikana. Mchezaji akichambuliwa na uongozi wa klabu ukavutiwa naye, dili hilo linaingia hatua nyingine.

2. Kutuma ofa kwa klabu yake

Wakati hatua ya kutambua mchezaji wa kumsajili ikikamilika, klabu inaanza utaratibu wa kutuma ofa kwa mchezaji inayemtaka.

Licha ya kwamba kuwasilisha ofa ni kitu rahisi, kazi kubwa zaidi inahitajika kabla ya kutuma ofa rasmi.

Kifungu 18(3) cha kanuni za Fifa juu ya hadhi na uhamisho wa wachezaji, inasema: "Klabu inayohitaji kumsajili mchezaji mwingine inapaswa kuwasiliana na klabu yake ya sasa kwa maandishi kabla ya kuingia kwenye mazungumzo naye."

Hii inazuia klabu 'kuteka' wachezaji, lakini klabu zinakwepa hilo kwa kuwatumia mawakala au chombo binafsi kwenda kuzungumza na mchezaji kuona kama yupo tayari kuhama.

Licha ya kwamba hiyo ni kosa kisheria, hatua hii ni muhimu kwa klabu katika kuepuka aibu ya kukataliwa na mchezaji - kama ilivyotokea kwa Liverpool wakati ofa yao ilipokataliwa na Alexis Sanchez mwaka 2014.

Baada ya ofa kukubaliwa na klabu inayomuuza mchezaji, hatua zinazofuata ndizo zinafuata.

3. Kuanzisha mazungumzo

Hatua ya mazungumzo kwenye usajili hufanywa kwenye ngazi tatu. Kwanza mazungumzo baina ya klabu mbili kuhusu ada ya mchezaji husika. Pili, mazungumzo baina ya klabu inayotaka kumnunua na kambi ya mchezaji juu ya mahitaji yake binafsi.

Tatu, mazungumzo baina ya klabu inayomtaka mchezaji na wakala wake kuhusu ada ya uwakala. Mazungumzo yanaweza kuwa mafupi au marefu, inategemea na mahitaji ya pande zote. Uhamisho unapokwama kwenye hatua hii, mara nyingi inakuwa mahitaji ya mshahara au mahitaji binafsi.

4. Kumfanyia vipimo afya na kuomba vibali

Baada ya makubaliano kufikiwa, mchezaji atachukuliwa kupelekwa kwenda kupimwa afya. Hatua hiyo inawaaminisha mashabiki kwamba dili hilo linaelekea patamu, licha ya kwamba linaweza kuvunjika pia kama vipimo vitafeli. Mfano Loic Remy alifeli vipimo Liverpool mwaka 2014 na Demba Ba alifeli kwenye hatua kama hiyo huko Stoke City mwaka 2011. Hata hivyo, wakati mwingine vipimo vya afya si kila kitu, Arsenal iliamua kumsajili Andrey Arshavin kutoka Zenit St Petersburg licha ya kwamba alifeli vipimo vya kwanza na kufaulu vya pili.

5. Kumsainisha mkataba

Baada ya vipimo vya afya na maombi ya kibali cha kazi yakishawasilishwa, mchezaji sasa anasaini mkataba. Baada ya hapo, mkataba huo unatumwa kwa 'faksi' bodi ya ligi na baada ya hapo anakabidhiwa jezi yake na kupiga picha. Hatua ya kumsainisha mkataba ni ya mwisho kabisa ili kujihakikishia mchezaji hajafungamana na upande wowote ambao unaweza kuleta shida siku za mbele kinapokuja kipindi cha kuanza kumtumia.