Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vidokezo 10 vya kujenga heshima na mvuto unapokuwa na watu

Muktasari:

  • Wapo ambao mkionana kwa dakika chache tu, bado unawakumbuka kwa muda mrefu kutokana na tabia zao, namna walivyoongea au walivyojitokeza.

WIKIENDI ni muda ambao watu wengi hutumia kupumzika na kujiburudisha baada ya shughuli nyingi za kazi au masomo. Wengine huenda ufukweni, migahawani, kwenye bustani, sehemu za muziki au kutembelea marafiki na familia.

Katika maeneo hayo hukutana na watu mbalimbali, lakini si kila mtu huacha kumbukumbu nzuri.

Wapo ambao mkionana kwa dakika chache tu, bado unawakumbuka kwa muda mrefu kutokana na tabia zao, namna walivyoongea au walivyojitokeza.

Kama unataka kuwa mmoja wa watu wanaoacha taswira nzuri kila wanapokwenda mtokoni, basi zingatia mambo haya muhimu.

                                         

1. TABASAMU ZURI

Tabasamu ni kitu kidogo lakini kina nguvu kubwa sana katika kujenga mahusiano. Unapotabasamu kutoka moyoni unaonyesha kuwa ni mtu mwenye amani, anayependa watu. Hakuna anayependa kuanza mazungumzo na mtu mwenye uso wa hasira au anayekaa muda wote bila kuonyesha furaha.

Wataalamu wa mawasiliano wanaeleza kuwa tabasamu humfanya mtu aonekane mwenye kuaminika na mkarimu. Hata kama hukufanya mazungumzo marefu, tabasamu lako linaweza kuwa sababu ya mtu kukukumbuka baada ya kuondoka.


2. MUONEKANO UNAONGEA

Siyo lazima kuvaa nguo za gharama kubwa ili uvutie. Kitu muhimu ni kuhakikisha mavazi yako ni safi, yamepigwa pasi na yanaendana na sehemu unayokwenda. Mtu anayejua kuvaa vizuri huonyesha kwamba anajiheshimu na anawathamini watu anaokwenda kukutana nao. Pia hakikisha viatu, mkoba, saa na vifaa vingine vinaendana na mavazi yako. Mwonekano mzuri humfanya mtu akukumbuke kwa sababu uliwasilisha picha ya mtu makini na mwenye mpangilio.


3. HESHIMA NA BUSARA

Namna unavyoongea ndiyo inayoweza kuwafanya watu wakutafute tena au wakukwepe. Tumia maneno ya heshima, sikiliza wengine wanapozungumza na usiwe mtu wa kukatiza mazungumzo kila wakati.

Epuka kejeli, matusi au maneno ya kuwashusha wengine. Watu hupenda kukaa karibu na mtu anayewafanya wajisikie vizuri na kuthaminiwa. Mazungumzo yenye busara huacha kumbukumbu nzuri kuliko maneno ya kujisifu.


4. NUKIA VIZURI

Harufu nzuri ni moja ya vitu ambavyo watu huvihifadhi akilini kwa urahisi. Ukitumia manukato mazuri yasiyo muumiza mtu, utaongeza mvuto wako bila kuwasumbua waliopo karibu nawe.

Usafi wa mwili, nguo safi na matumizi sahihi ya deodorant (kipako cha kwapani) ni mambo yanayokamilisha muonekano wako pekee. Hakikisha manukato mazuri yanahusika, kwani harufu kali kupita kiasi inaweza kuwafanya watu wajisikie vibaya.


5. KUJIAMINI

Kujiamini ni sifa inayovutia sana. Unapotembea, kuzungumza na kushirikiana na watu kwa kujiamini unaonyesha unaamini uwezo wako. Hata hivyo, kujiamini hakumaanishi kujisifu au kuwadharau wengine.

Mtu anayejivuna mara nyingi huwafanya watu wapoteze hamu ya kuendelea kuzungumza naye. Kuwa mnyenyekevu huku ukiamini uwezo wako ndiko kunakokuvutia zaidi.


6. SIKILIZA SANA KULIKO KUONGEA

Watu wengi hupenda kusikilizwa kuliko kuzungumziwa. Ukimpa mtu nafasi ya kueleza mawazo yake bila kumkatiza, atajisikia kuthaminiwa. Kuuliza maswali yenye kujenga mazungumzo na kuonyesha unafuatilia anachokisema mwenzako ni ishara ya heshima. Mara nyingi watu hukumbuka wale waliowasikiliza kwa makini kuliko wale waliotaka wao pekee waonekane.


7. LUGHA NZURI YA MWILI

Mbali na maneno, mwili wako nao huwasiliana. Kusimama vizuri, kutembea kwa kujiamini, kuwasalimia kwa heshima na kutazamana machoni wakati wa mazungumzo huonyesha una heshima na unaamini unachokizungumza.

Epuka tabia ya kukunja uso, kukaa ukiwa umeinama muda wote au kuonyesha kukosa hamu ya kushiriki mazungumzo. Lugha nzuri ya mwili huwafanya watu wajisikie huru kuwa karibu nawe.


8. ONYESHA KUJALI WENGINE

Watu hukumbuka matendo mema kuliko maneno. Kumfungulia mtu mlango, kumpisha, kumsaidia pale anapohitaji au kumuuliza hali ni mambo madogo yanayoweza kukuongezea heshima kubwa.

Usiwajali watu wenye nafasi au fedha pekee. Mtu anayewaheshimu wote bila ubaguzi huonekana mwenye utu na hupendwa na wengi.


9. TUMIA SIMU KWA KIASI UNAPOKUWA NA WATU

Ni jambo la kawaida kuona watu wameketi pamoja lakini kila mmoja anatazama simu yake. Tabia hiyo hupunguza mawasiliano na kuwafanya watu wajisikie hawana umuhimu.

Unapokuwa mtokoni, weka simu pembeni kwa muda na toa nafasi ya kuzungumza na watu uliopo nao. Hilo linaonyesha unawapa thamani na unafurahia uwepo wao.


10. ONDOKA VIZURI

Namna unavyoondoka ni muhimu kama ulivyowasili. Kabla ya kuondoka, washukuru uliokuwa nao, waage kwa heshima na waonyeshe umefurahia muda uliotumia nao.

Tabia hii huwafanya watu wakutamani tena na kukukaribisha katika mikusanyiko mingine. Kumbukumbu nzuri hujengwa kuanzia mwanzo wa kukutana hadi mwisho wa mazungumzo.