Hatimaye BMT wamekata mzizi wa fitina
Muktasari:
- Kijumla hapa kijiweni tuna furaha sana baada ya BMT kusema katiba mpya ya Simba inapaswa kuanza kufuatwa badala ya jambo hilo kutofanyiwa kazi.
WANANGU pale Simba baada ya muda mrefu mambo yanaanza kwenda katika mstari mnyoofu baada ya tamko la Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Kijumla hapa kijiweni tuna furaha sana baada ya BMT kusema katiba mpya ya Simba inapaswa kuanza kufuatwa badala ya jambo hilo kutofanyiwa kazi.
Kuna mwana hapa kijiweni anasema yeye kilichomfurahisha ni sasa maneno maneno kwa mwekezaji yatapungua maana mfumo utaanza kufanya kazi na hela anayoweka itakuwa kwa mfumo rasmi.
“Mwekezaji amechanjwa sana hela na amekuwa akilalamika sasa hii katiba ikianza kufanyiwa kazi, hatotoa tu hela kiholela bali kwa utaratibu unaoeleweka.
"Ppia mwekezaji atapata wenzake wawili au watatu ambao atasaidiana nao katika kuendesha Simba tofauti na mwanzo na mzigo ulikuwa kwake peke yake,” anasema mdau wa kwanza.
Mwanakijiwe mwingine yeye anaamini jambo hilo litampa ulinzi mwenyekiti wa klabu Murtaza Mangungu.
“Yule Mzee Mangungu amekuwa akilaumiwa sana anachelewesha mchakato wa mabadiliko na kuna wakati amekuwa akipokea mashambulizi asiyostahili.
“Sasa tunaingia rasmi katika uwekezaji angalau na yeye atapumzika na lawama anafanya mabadiliko yasikamilike zitaisha,” anaongea kwa hisia mwingine.
Mjadala unaendelea hapa kijiweni lakini kijumla karibia wote tuna furaha hapa kwa hicho kinachoenda kutokea.