Prime
Haji Manara zilongwa mbali, zitendwa mbali
ZILONGWA mbali zitendwa mbali ni msemo wa Kizaramo, ‘lugha ya kufikia’ ya Diwani wa Kariakoo na msemaji wa zamani wa Simba na Yanga, Haji Sunday Manara ‘Bugatti’.
Nimetumia ‘lugha ya kufikia’ kwa sababu hii ni lugha ya kabila la upande wa mama yake, ilhali upande wa baba yake ni watu wa kutoka Kigoma; kama si Waha basi ni Wamanyema.
Lakini mwenyewe hujivunia zaidi uzaramo kuliko ukigoma, yawezekana ni kwa sababu hajawahi kuishi Kigoma. Familia ya baba yake ilihamia Dar es Salaam wakati baba yake akiwa kijana mdogo sana. Yeye kazaliwa Dar es Salaam, kakulia Dar es Salaam.
Na kwa sababu muda mwingi wa maisha yake alikuwa na mama yake pale Kariakoo, basi uzaramo ukamvaa hasa.
Juma lililopita ‘Mzaramo’ Haji Manara aliuzua ugomvi mkubwa na mashabiki wa Yanga ‘alipoichokonoa’ klabu hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo kimoja cha redio, Haji aliushutumu uongozi wa Yanga kwa kuwekeza kwenye mipango holela ya muda mfupi.
“Yanga kufuzu mara moja robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa miaka minne ni anguko. Na anguko letu la kwanza ni kusajili kila baada ya miezi sita. Kila dirisha, liwe kubwa au dogo, Yanga inasajili... huwezi kufanikiwa.
“Hata Rais nimemwambia, kila baada ya miezi sita unaleta wachezaji saba... unaleta wachezaji sita.”
Maneno haya yanayokaribia ukweli yalipenya hasa katika masikio ya wanayanga na kukita kwenye mioyo yao.
Wakaanza kumsakama kwa maneno anaishambulia Yanga kwa sasa kwa sababu yeye si mwanayanga.
Kelele zilipozidi, akaitisha mkutano na waandishi wa habari, ndipo akamwaga na ugali kabisa, baada ya awali kumwaga mboga tu.
Akaongea maneno mengi kuhusu Yanga na Simba, kisha akamwagia maua mengi sana beki wa Simba, Rushine De Reuck, raia wa Afrika Kusini. Halafu akamalizia kwa kusema yeye, kama mwana Yanga hakuna tatizo kumsifia mchezaji mzuri wa Simba.
Akatania kwa kusema mchezaji mwenyewe jina lake linafanana na mkewe wa zamani, Rushaina, pia ni mzuri hata kwa mwonekano. Hapa sasa ndipo kwenye msingi wa Pumzi ya Moto kwa andiko letu la leo katika kolamu hii.
Haji amemsifia mchezaji wa Simba, kisha kutetea uamuzi wake kana kwamba hakuna tatizo kabisa. Mwaka 2021, Haji akiwa msemaji wa Simba, alimjia juu kipa wao Aishi Manula kwa kumsifia Bernard Morrison ‘BM3’.
Ni baada ya Morrison kufunga bao la dakika ya 44 kwa mkwaju wa adhabu ndogo (friikiki) na kuipatia Yanga ushindi wa 1-0 katika mechi ya Ligi ya Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Machi 8, 2020. Bao hilo liliingia hadi bungeni na Makamu wa Rais wa wakati huo, Philip Mpango, akalibatiza jina la ‘Mkuki wa Sumu’.
Aishi alialikwa katika moja ya vituo vya redio na akaulizwa kuhusu bao lile. Akasema hakuna cha zaidi ya kumsifia mpigaji badala ya kujilaumu; akamsifia sana Bernard Morrison.
Hapo Haji alichafukwa sana... kwa nini Aishi, kama mchezaji wa Simba, amsifie mchezaji wa Yanga?
Haji alimbwatukia Aishi na kumtamkia maneno makali yasiyofaa kuandikwa hapa. Aishi alishambuliwa kana kwamba amefanya kosa la kuua. Sasa Haji huyu ndiye anayetuambia leo kumsifia mchezaji wa timu pinzani si tatizo. Ndiyo maana nasema ZILONGWA MBALI ZITENDWA MBALI.
Na hii si moja tu. Manara amekuwa na matukio mengi ya kufanya kinyume na anachokisema. Alipokuwa Simba, aliwahi kuulizwa endapo anaweza kufanya kazi Yanga. Akasema “over my dead body”, akiwa na maana hata maiti yake haiwezi. Akasema yeye, licha ya kwamba ni mtoto wa gwiji wa Yanga, lakini ni Simba damu na alipokuwa mtoto alikuwa akipita pale Jangwani na kuwatupia mawe Yanga.
Akasema babu yake alikuwa akimpeleka uwanjani kwenye mechi za Simba. Babu anayemzungumzia hapa ni Hassan Haji (marehemu), baba mzazi wa mamake Haji. Mwanzoni mwa miaka ya 1970, mzee huyo alikuwa mwenyekiti wa Simba na mwaka 1975 ukatokea mpasuko uliomfanya afukuzwe Simba. Ndipo yeye na wenzake wakaenda kuanzisha timu mpya ya Red Star (Nyota Nyekundu); maskani yao yalikuwa Mtaa wa Kongo, jirani kabisa na Msimbazi.
Huyu ndiye babu aliyemlea Haji kwa sehemu kubwa ya maisha yake ya utotoni. Kwa hadithi hii mtu anaweza kuamini kweli Haji ni Simba tangu utotoni. Fumba na kufumbua, Haji akahamia Yanga na kusema yeye ni Yanga damu tangu utotoni. Anasema alichezea hadi timu ya watoto iliyoitwa DIGIDIGI.
Anasema akiwa mtoto alikuwa anacheza pale Jangwani na vyumba vyote anavijua, hadi wachezaji waliokuwa wakilala.
Huyu ndiye Haji Manara halisi... ZILONGWA MBALI ZITENDWA MBALI.