Giallossi kuvunja mwiko miaka 26 mbele ya Serie A?
Muktasari:
- Wakati huo kikiwa chini ya kocha Fabio Capello, kikosi hicho kilichokuwa na mastaa kama Cafu, Walter Samuel, Francesco Totti, Vincenzo Montella na Gabriel Batistuta kiliwapiku Juventus kwa tofauti ya pointi mbili.
ROMA, ITALIA: KWA ushindi wa michezo minne kati ya mitano ya Serie A, Roma wakiwa na jina la utani la Giallorossi wanaongoza katika hatua za mwanzo za msimu wakiwa na pointi 13 sawa na Inter Milan. Na wameshakutana na Inter ambayo pia ina rekodi hiyo hiyo ya ushindi, huku wakilenga kuwania ubingwa, tangu walipobeba Scudetto msimu wa 2000-01.
Wakati huo kikiwa chini ya kocha Fabio Capello, kikosi hicho kilichokuwa na mastaa kama Cafu, Walter Samuel, Francesco Totti, Vincenzo Montella na Gabriel Batistuta kiliwapiku Juventus kwa tofauti ya pointi mbili.
Na sasa zaidi ya robo karne baadaye, Roma wanataka kumaliza kusubiri kwa muda mrefu ili kutwaa ubingwa. Ni mapema sana, lakini wameanza vizuri kadiri inavyowezekana wakishinda michezo minne, sare moja na kufungwa mabao matatu pekee.
Wameshindwa kushinda michezo mitano ya kwanza ya Serie A kwa mara ya tatu katika historia yao, baada ya kushinda misimu ya 2013-14 na 2014-15. Hata hivyo, ili kupata ushindi wa tano, wangelazimika kuifunga timu nyingine pekee (inter Milan) katika Serie A ambayo ina rekodi ya asilimia 100 ya ushindi na ni mabingwa watetezi.
Inter ilitembelea Stadio Olimpico Jumamosi katika mchezo ambao tayari ulionekana kuwa muhimu katika mbio za ubingwa na kutoka sare ya bao 2-2.
MBAYA HIYOO
Roma walikuwa na rekodi mbaya katika michezo ya karibuni dhidi ya Inter, wakishinda miwili pekee kati ya 18 iliyopita, wakitoka sare saba na kupoteza 10. Pia walipoteza mchezo wao wa mwisho kwa mabao 5-2 dhidi ya Inter kwenye Uwanja wa San Siro mwezi Aprili, mwaka huu.
Hata hivyo, safari hii mambo yanaonekana kuwa tofauti. Roma walimaliza vizuri msimu uliopita. Giallorossi wameshinda michezo tisa ya mwisho ya Serie A; ni mara mbili pekee katika historia ambapo wamewahi kushinda angalau michezo 10 mfululizo katika mashindano hayo wakifanya hivyo mara 11 kati ya Desemba 2005 na Februari 2006, na mechi 11 tena kati ya Mei na Oktoba 2013.
Kocha mkuu, Gian Piero Gasperini amekuwa na safari yenye misukosuko katika kazi hiyo akifanya vipindi viwili tofauti katika kila moja ya klabu za Crotone, Genoa na Palermo, pamoja na kipindi kifupi Inter Milan kabla ya kuwa na mafanikio miaka tisa Atalanta. Hata hivyo mwanzo wa 2025 alipewa jukumu la kuifanya Roma itishe Italia.
MAKOCHA WATATU
Roma walitoka msimu wa 2024-25 uliokuwa na vurugu nyingi upande wa benchi la ufundi. Ulianza huku gwiji wa klabu hiyo Daniele De Rossi akiwa kocha, kabla ya kubadilishwa mwezi mmoja tu baada ya msimu kuanza na Ivan Juric.
Chini ya miezi miwili baadaye, Roma walikuwa tayari na kocha wa tatu, na klabu ikamteua kocha mkongwe Claudio Ranieri, ambaye huo ulikuwa muda wake wa tatu kuiongoza.
Licha ya misukosuko hiyo Roma walimaliza katika nafasi ya tano iliyokuwa nzuri, lakini baada ya Ranieri kustaafu ukocha mwishoni mwa msimu Gasperini alipewa mwaka mmoja tu baada ya kuiongoza Atalanta kwa mafanikio makubwa na kushinda UEFA Europa League.
Kipindi chake kilianza vizuri, huku Roma wakishinda michezo mitano kati ya sita ya kwanza, lakini mfululizo wa vipigo vinne katika michezo sita kati ya mwishoni mwa Novemba 2025 na mwanzoni mwa Januari 2026 uliwarudisha katika hali halisi.
Mwanzoni ilikuwa ni kama walikuwa na matokeo ya “yote au hakuna”. Roma hawakutoka sare katika mchezo wa Serie A chini ya Gasperini hadi Januari 25 walipopata sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya AC Milan katika mchezo wa 22 wa ligi msimu huo. Walikuwa nje ya nafasi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini ushindi wa michezo mitano mfululizo mwishoni mwa msimu uliwapa nafasi ya tatu.
Na kiwango hicho kimeendelea hadi msimu huu. Roma walianza kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Fiorentina na Lecce, kabla ya kufanya ‘comeback’ ya kusisimua mwishoni mwa mchezo dhidi ya klabu ya zamani ya Gasperini, Atalanta. Ushindi wa 2-0 uliokuwa mgumu dhidi ya Torino uliwafanya wafikishe ushindi wa nne katika michezo minne.
HAYA SASA
Kama ilivyokuwa katika mtindo wa uchezaji wa timu, Roma walikuwa na mchezo wa moja kwa moja zaidi msimu wa 2025-26 kuliko 2024-25. Baadhi ya mechi walizocheza kabla ya Gasperini kuwasili zilikuwa za taratibu, na ingawa hawakwenda moja kwa moja kabisa, kasi ya ziada waliyocheza nayo ilionekana kuongeza kitu katika mchezo.
Hilo limeendelea katika wiki za mwanzo za msimu huu. Wana wastani wa pasi nyingi zaidi kidogo kwa kila mchezo, lakini walikuwa bado hawajakutana na timu yoyote iliyomaliza katika nafasi sita za juu msimu uliopita, hivyo huenda hali hiyo ikabadilika kadiri msimu unavyoendelea.
Bila shaka, ni timu ya Gasperini, hivyo wanafanya kazi kwa bidii kurejesha mpira. Roma waliongoza kwa shinikizo la mashambulizi (pressing) katika Serie A msimu uliopita wakiwa na 476.
Huo ni mfululizo wa matukio unaoanzia katika theluthi ya ulinzi ya mpinzani ambapo mpinzani anakuwa amepiga pasi tatu au chache na unaishia katika nusu yake ya uwanja. Hii inaonyesha ubora wa shinikiso la Roma katika kuwanyang’anya wapinzani mpira.
WANASHAMBULIA HAO
Msimu huu wako nafasi ya pili nyuma ya Juventus kwa mfululizo wa ‘pressing’, lakini wanaongoza Serie A kwa kupora mpira katika maeneo ya juu ya uwanja mara 52, pamoja na matukio 15 ya kuupora katika maeneo ya juu ambayo yameishia kwa shuti.
Roma pia wanaongoza kwa mashambulizi ya moja kwa moja wakiwa na 13 ambao ni mfululizo wa mchezo wa wazi unaoanzia ndani ya nusu ya uwanja wa timu yenyewe na angalau asilimia 50 ya harakati kuelekea lango la mpinzani, na kuishia kwa shuti au mchezaji kugusa mpira ndani ya boksi la mpinzani.
Pia wanaongoza kwa maendeleo ya mpira, ambayo ni wastani wa umbali wanaosogea mbele kwa kila mfululizo wa mchezo, ukiwa mita 17.2. Hata hivyo, wanaidhibiti sana michezo. Unaweza kuona katika maeneo yao ya udhibiti kwamba wamekuwa na zaidi ya asilimia 55 ya miguso ya mpira katika sehemu kubwa ya uwanja katika michezo yao ya Serie A msimu huu.
Hii ina maana wapinzani lazima wawe makini kwa sababu Roma wanakuwa na mpira kwa muda mwingi, wakiwa na wastani wa asilimia 59.8 ya umiliki wa mpira, kiwango cha tatu kwa juu Serie A msimu huu, lakini pia wanaanzisha mashambulizi kwa haraka.
NAMBA ZA MOTO
Mchezaji mmoja ambaye amefanya vizuri zaidi chini ya Gasperini ni Donyell Malen. Mholanzi huyo alikuwa na mwaka wa kawaida akiwa Aston Villa 2025, akicheza michezo 46 katika mashindano yote, lakini 14 tu kati yake akiwa kwenye kikosi cha kwanza, huku akifunga mabao 10.
Hata hivyo, alijiunga na Roma kwa mkopo Januari na mara moja akaanza kuonyesha uwezo mkubwa, ambapo alifunga mabao 14 katika michezo 18 ya Serie A wakati wa kipindi chake cha mkopo; ni Harry Kane pekee aliyefunga zaidi katika ligi tano kubwa za Ulaya katika kipindi hicho (mabao 16).
Roma walifanya uhamisho wake kuwa wa kudumu katika dirisha lililopita, na ameendelea kuwalipa. Tangu mechi yake ya kwanza Serie A Januari 18, Malen amefunga mabao 20 katika mechi 22, angalau mara mbili ya mchezaji mwingine yeyote katika mashindano hayo katika kipindi hicho.
Katika ligi tano kubwa za Ulaya, amefunga angalau mara nne zaidi ya mchezaji yeyote, akiwa mbele ya Kane na Lamine Yamal ambao wana mabao 16. Jambo muhimu linaonekana kuwa amecheza kama mshambuliaji. Malen alitumia takribani theluthi mbili ya muda wake akiwa mbele Aston Villa, lakini pia alitumika mara kwa mara upande wa kulia. Roma, yeye ni mshambuliaji kamili, na ni mshambuliaji mzuri.
Pia anapata nafasi nzuri za kufunga akitengenezewa. Malen ana mabao yanayotarajiwa (xG) yasiyohusisha penalti 4.23 katika Serie A msimu huu, ikiwa angalau 1.17 zaidi ya mchezaji mwingine yeyote. Ni wachezaji watatu tu walio na zaidi ya 2.0.
Vilevile Paulo Dybala anaonekana kurejea katika kiwango chake cha zamani. Tangu alipotuaa Roma 2022 amewahi kutoa zaidi ya asisti sita za Serie A msimu mmoja mara moja tu, lakini sasa amebakiza tatu kuvuka kiwango hicho.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 amemsaidia Malen kufunga mara tatu kati ya sita alizofunga, huku akiwa na asisti nne kwa jumla, idadi inayomfanya kuwa miongoni mwa vinara kwenye ligi tano bora za Ulaya pamoja na Anthony Gordon wa Barcelona na Javi Hernandez wa Espanyol.
Dybala ametengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga katika ligi, akiwa na 17 kwa ujumla na 14 kutokana na mchezo wa wazi, huku pia akionyesha umuhimu upande wa ulinzi kwa kupora mpira katika theluthi ya mwisho ya uwanja mara nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote, mara saba. Roma wamefungwa mabao matatu katika michezo mitano ya Serie A msimu huu, huku wakikabiliwa na mashuti 32 pekee, ambayo ni idadi ya pili kwa uchache.
Lakini, kuna bidii inaonekana katika timu nzima. Ni wachezaji watatu pekee ambao wameupora mpira mara nyingi zaidi ya mabeki wa Roma Emanuele Lulli na Mario Hermoso, ambao wote wamefanya hivyo mara 22, huku Hermoso pia akiongoza ligi kwa kukatiza na mipira mara 15.