Geita Gold, Polisi Tanzania zilivyoanza na moto Ligi Kuu
Muktasari:
- Rekodi zinaonyesha tangu msimu wa 2021-2022 hadi sasa ni timu 12 zilizopanda daraja kutoka Championship, ambapo kati ya hizo zilizoshinda ni tano, sambamba na zilizopoteza pia, huku mbili zikitoka sare kama Mwanaspoti linavyozielezea.
MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027 unaendelea kushika kasi kwa sasa, huku tukishuhudia wageni wapya Geita Gold, maafande wa Polisi Tanzania na Kagera Sugar zikianza kupata matokeo mchanganyiko kutokana ushindani uliopo.
Rekodi zinaonyesha tangu msimu wa 2021-2022 hadi sasa ni timu 12 zilizopanda daraja kutoka Championship, ambapo kati ya hizo zilizoshinda ni tano, sambamba na zilizopoteza pia, huku mbili zikitoka sare kama Mwanaspoti linavyozielezea.
MSIMU WA 2021-2022
Msimu huo ulishuhudiwa Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars ikipanda Ligi Kuu Bara baada ya kuongoza kwa pointi 66, ambazo ni sawa na DTB iliyokuja kubadilishwa jina baadae na kuitwa Singida Big Stars, zikitofautiana kwa mabao tu.
Zikiwa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2022-2023, Ihefu ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Ally Bilaly, dakika ya 19, katika pambano lililopigwa Agosti 15, 2022.
Kwa upande wa DTB iliyotambulika baadaye kwa jina la Singida Big Stars, ilianza vizuri kwa ushindi wa bao 1-0 la nyota wa zamani wa kikosi hicho raia wa Brazil, Peterson Da Cruz 'Peu', dakika ya 36, katika mechi iliyopigwa Agosti 16, 2022.
MSIMU WA 2022-2023
Huu ndio msimu uliopandisha timu tatu kwenda Ligi Kuu Bara zikitoka Championship, ambapo mbili zilizomaliza ya kwanza na ya pili zilipanda moja kwa moja kwa mujibu wa kanuni, huku nyingine ikipanda kupitia mechi za mtoano yaani ('Play-Off').
Mabingwa msimu huo walikuwa ni maafande wa JKT Tanzania iliyomaliza na pointi 63, ikiungana na Kitayosce kupanda daraja ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, iliyokuwa ya pili kwa kukusanya pointi 60.
Mbali na JKT na Kitayosce ambayo kwa sasa ni TRA United zilizopanda moja kwa moja, timu nyingine ni maafande wa Mashujaa ambao ilipanda kwa kuishusha Mbeya City kwa jumla ya mabao 4-1, ambayo hata hivyo, ilirejea tena kwa msimu wa 2025-2026.
Baada ya kupanda Ligi Kuu, JKT ilianza vizuri na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Namungo FC, lililofungwa na Martin Kigi dakika ya 43, katika mechi iliyopigwa Agosti 15, 2023, huku kwa upande wa TRA United ikianza kwa kuchapwa mabao 4-0.
Tabora ambayo ni TRA United kwa sasa, ilichapwa mabao hayo na Azam, yaliyofungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' aliyefunga matatu 'Hat-Trick' ya dakika ya 3, 9 na 13, huku lingine moja likifungwa na mshambuliaji nyota, Prince Dube, dakika ya 5.
Hata hivyo, TRA ilikuwa na wachezaji wanane uwanjani baada ya wengine kutokamilisha usajili, ambapo mechi ilichezwa kwa dakika 18 badala ya 90, kutokana na wawili kuumia na kubakia sita ambao kikanuni hairuhusu pambano hilo kuendelea tena.
Kwa upande wa maafande wa Mashujaa ambao ilipanda kupitia 'Play-Off', ilianza vizuri Ligi Kuu mechi ya kwanza, baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-0, Agosti 16, 2023, yaliyofungwa na Adam Adam dakika ya 15 na Othman Dunia dakika ya 73.
MSIMU WA 2023-2024
Msimu huu ilipanda KenGold iliyokuwa mabingwa wa Championship kwa kuongoza na pointi zake 70, ikiungana na Pamba Jiji iliyomaliza ya pili na pointi 67, ambayo ilirejea Ligi Kuu Bara baada ya miaka 23, tangu iliposhuka daraja mwaka 2001.
Katika Ligi Kuu Bara, Pamba Jiji ikiwa nyumbani ilianza kwa suluhu (0-0) dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, katika pambano lililoshuhudia ushindani wa hali ya juu, lililopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Agosti 16, 2024.
Kwa KenGold iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025, ikitokea Ligi Kuu Bara hadi Championship, ilianza vibaya kwa kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Agosti 18, 2024.
Mechi hiyo iliyopigwa Agosti 18, 2024, ilishuhudia mabao ya Singida yakifungwa na Emmanuel Keyekeh dakika ya 41, Elvis Rupia ya 61 na Mohamed Damaro ile ya 81, huku bao la upande wa KenGold lilifungwa na Joshua Ibrahim katika dakika ya 68.
MSIMU WA 2024-2025
Katika msimu huu, ulishuhudiwa Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024 kwa kuburuza mkiani na pointi zake 21, ikirejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kumaliza mabingwa wa Ligi ya Championship, kufuatia kukusanya jumla ya pointi 71.
Mtibwa iliungana na Mbeya City kupanda baada ya timu hiyo ya Mbeya kumaliza nafasi ya pili na pointi 68, ikirejea tena Ligi Kuu, kufuatia kushuka msimu wa 2022-2023, ilipotolewa na Mashujaa kwa jumla ya mabao 4-1 katika mechi ya mtoano.
Mbeya City ndio pekee iliyoanza vizuri Ligi Kuu kwa msimu wa 2025-2026 kwa kuifunga Fountain Gate bao 1-0, lililofungwa kwa penalti na Habib Kyombo dakika ya 56, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Septemba 18, 2025.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar, ilianza Ligi Kuu msimu huo kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya maafande wa Mashujaa, lililofungwa na Idrisa Stambuli dakika ya 32, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Septemba 21, 2025.
Mara ya mwisho kwa Mashujaa na Mtibwa kukutana katika Ligi Kuu kabla ya pambano la Septemba 21, 2025, ilikuwa pia kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, ambapo kikosi cha maafande kiliibuka na ushindi wa mabao 3-2, mechi iliyopigwa Mei 25, 2024.
Mabao ya Mashujaa yalifungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Reliants Lusajo aliyefunga mawili, na lingine lilifungwa na Mundhir Vuai, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Seif Karihe, huku lingine ni la kujifunga mwenyewe kwa Samson Madeleke.
MSIMU WA 2025-2026
Msimu wa 2025-2026 ulishuhudiwa jumla ya timu tatu zikipanda daraja kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara na kati ya hizo mbili ambazo ni Geita Gold na Kagera Sugar zilipanda moja kwa moja, huku Polisi Tanzania ikipanda kupitia mtoano.
Geita Gold ndio mabingwa wa Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kumaliza kinara na pointi 77, kufuatia kushinda mechi 24, sare tano na kupoteza moja tu kati ya 30 iliyocheza, huku ikifunga jumla ya mabao 68 na kuruhusu 17.
Timu hiyo iliyopanda daraja kufuatia kushuka msimu wa 2023-2024, imeanza vizuri msimu wa 2026-2027 wa Ligi Kuu, baada ya kuifunga Mbeya City bao 1-0 la Obrey Chirwa dakika ya 15, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Agosti 14, 2026.
Kwa Kagera Sugar 'Wanankurukumbi' iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 72, iliyorejea Ligi Kuu msimu wa 2025-2026 baada ya kushuka 2024-2025, ilianza vibaya msimu huu wa 2026-2027 kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Simba, Agosti 16, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, ilishuhudiwa kikosi hicho cha Kagera Sugar kikishindwa kutamba na kuchapwa mabao hayo mawili yaliyofungwa na Ismael Olivier Toure dakika ya 45+1 na Elie Mpanzu dakika ya 69.
Kwa upande wa kikosi cha maafande wa Polisi Tanzania, kilichorejea tena katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilimaliza nafasi ya tatu katika Ligi ya Championship kikiwa na pointi zake 66.
Baada ya kumaliza nafasi ya tatu, Polisi ikacheza mechi za mtoano ili kusaka tiketi ya kurejea Ligi Kuu Bara, ikianza na kuitoa Mbeya Kwanza iliyomaliza nafasi ya nne na pointi 61 katika Ligi ya Championship na kuichapa kwa jumla ya mabao 7-1.
Ushindi huo ukaipeleka Polisi mechi ya mwisho ya hatua ya mtoano na ilicheza na Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi 32, iliyocheza na Mbeya City iliyomaliza nafasi ya 14 na pointi zake 30 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Baada ya Prisons kuchapwa jumla ya mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City zilizocheza mechi hiyo ya mtoano zikiwa Ligi Kuu Bara, kikosi hicho kikachapwa na Polisi Tanzania jumla ya mabao 4-1, kisha kurejea tena kufuatia kushuka msimu wa 2022-2023.
Mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Polisi Tanzania ikaanza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC, Agosti 15, 2026, katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na kushuhudia mabao yote yakifungwa kwa penalti.
Matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, ilikuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya 75, lililofungwa kwa penalti na nyota wa kikosi hicho, Abdul Suleiman 'Sopu', kisha Anuary Jabir akaisawazishia Polisi kwa penalti pia ya dakika ya 89.