Foden anavyoweza kurejea upya Man City
Muktasari:
- Kocha wa City, Enzo Maresca alikuwa ametabiri kuwa Foden angefunga, na kweli alifunga. Katika sehemu kubwa ya maisha yake ya soka, utabiri huo usingeonekana kuwa wa ajabu hata kidogo. Lakini mambo yamebadilika sasa.
MANCHESTER, ENGLAND: PHIL Foden alivunja mfululizo wa mechi 35 bila kufunga alipocheza dhidi ya Ipswich katika Uwanja wa Etihad, lakini anakabiliwa na ushindani katika nafasi kadhaa anapojaribu kurejesha kiwango chake cha kawaida.
Kocha wa City, Enzo Maresca alikuwa ametabiri kuwa Foden angefunga, na kweli alifunga. Katika sehemu kubwa ya maisha yake ya soka, utabiri huo usingeonekana kuwa wa ajabu hata kidogo. Lakini mambo yamebadilika sasa.
Foden alikuwa amefunga mabao 27 pekee akiwa na Man City msimu wa 2023-24. Hata hivyo, Ipswich ilipowasili Etihad, Jumamosi alikuwa amefikisha mechi 35 bila kufunga, pamoja na mechi mbili akiwa na timu ya taifa ya England, ambazo huenda zilimgharimu nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia 2026.
Majuzi, Foden alifunga bao la kwanza kwa City dhidi ya Ipswich kabla ya Halaand kufutupia mawili na kulipa chama lake ushindi wa mabao 3-2.
Lakini, kuna Foden wawili. Maresca anakumbuka kipaji kile cha dogo aliyekuwa akichipukia, mchezaji aliyekuwa akishinda tuzo binafsi na aliyeonekana kuwa na uwezo wa kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa kizazi chake kabla ya kugeuka kuwa mchezaji wa akiba wa City aliyekuwa na wakati mgumu kufunga mabao.
“Kwa upande wa Phil, nimesema mara nyingi kwamba namfahamu tangu miaka iliyopita. Kwangu, yeye ni mmoja wa wachezaji bora katika Ligi Kuu England,” anasema kocha huyo wa City, ambaye aliwahi kufanya kazi na Foden katika vipindi vyake vya awali Etihad.
“Na tangu siku ya kwanza, ni wajibu wangu kumsaidia ili aweze kurejea tena kuwa mmoja wa wachezaji bora.”
Hata hivyo, mchakato huo haukuanza vizuri. Kufikia wakati City ilipoanza mchezo dhidi ya Ipswich, kwa maana fulani Foden alikuwa amekosa kushiriki mechi nne na robo. Kadi nyekundu aliyopata kipindi cha kwanza katika Dabi ya Manchester ilifuatiwa na adhabu ya kufungiwa mechi tatu za mashindano ya ndani. Pia alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumika katika kipigo cha Ligi ya Mabingwa dhidi ya PSG.
Hata kabla ya kufungiwa, tayari alikuwa amepoteza nafasi yake ya kucheza mara kwa mara, chini ya makocha waliomfuata mmoja baada ya mwingine. Kwanza katika msimu wa mwisho wa kocha Pep Guardiola na baadaye ule wa kwanza wa Maresca, ambapo Rayan Cherki ndiye aliyekuwa akicheza kiungo mshambuliaji namba 10 na kung'ara kwa kiwango cha kuvutia. Foden hakuwa akionyesha ubunifu wala ubora.
Huenda hali hiyo inaonyesha jinsi Maresca alivyo na wachezaji wengi wenye uwezo kiasi kwamba Foden ameonekana kuwa mchezaji wa kawaida zaidi katika nafasi hiyo. Pia huenda changamoto nyingine ni ushindani unaoanza kujitokeza kutoka kwa Enzo Fernandez, ambaye alisajiliwa kwa ada kubwa ya Pauni 125 milioni aliyecheza kipindi cha pili dhidi ya PSG akiwa kiungo aliyepanda zaidi katika watatu wa eneo hilo.
Somo moja lililotokana na kipigo cha 4-2 ilichopata Man City katika mechi hiyo huenda ni kwamba Maresca anahitaji Ayyoub Bouaddi na Elliot Anderson wote wakabaki nyuma kuimarisha eneo la kiungo.
Hali hiyo inaweza kumaanisha kuwa Fernandez ndiye atakayekuwa kiungo anayepanda zaidi katika watatu hao. Pia kuna ushahidi unaoonyesha kuwa Maresca ana shaka fulani kuhusu Cherki.
Kocha huyo tayari amemtoa mchezaji huyo mara tatu wakati wa mapumziko katika msimu huu, na alifikiria kupunguza muda wake wa kucheza katika mechi nyingine ya nne, lakini Mfaransa huyo aliendelea na mchezo na kufanya vizuri dhidi ya Crystal Palace.
Hata hivyo, njia ya Foden kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza huenda ikapatikana katika nafasi nyingine.
Foden alianza mchezo dhidi ya Man United uliochezwa Old Trafford akiwa winga wa kulia. Ingawa City ina mawinga wanne, Allan Elias wa Brazil amekuwa akipata nafasi chache. Foden anaweza kuwa mshindani mkubwa zaidi wa Jeremy Doku, Antoine Semenyo na Iliman Ndiaye.
Kisha, licha ya City kuwa na kikosi kipana kiasi cha kuwa na wachezaji wawili kwa kila nafasi, kuna nafasi moja muhimu ambayo inaonekana kuwa tofauti; mshambuliaji wa kati. Maresca alikuwa amekiri kwamba atalazimika kumpumzisha Erling Haaland hivi karibuni, ambapo mshambuliaji huyo alionekana kujitoa mwenyewe uwanjani katika muda wa nyongeza dhidi ya Ipswich baada ya kupata maumivu, ingawa baadaye aliondoa hofu ya kukaa nje kwa muda mrefu kwa kumwambia kocha wake kuwa alikuwa sawa.
Hata hivyo, Semenyo alikuwa amepangwa kuwa mbadala wa Haaland. Jambo hilo huenda likaongeza uzito kwa wazo kwamba Foden anaweza kupata muda zaidi wa kucheza katika nafasi za pembeni.
Wakati wachezaji wengine kadhaa, akiwemo Semenyo, Fernandez na Anderson, walipopumzishwa na kutocheza kuanzia mwanzo dhidi ya Ipswich, hali hiyo ilizua uwezekano kwamba walikuwa wamehifadhi nguvu kwa ajili ya mechi zilizofuata. Pia ilionekana kuwa Haaland angeweza kukosa mchezo wa leo, Jumanne, dhidi ya AEK Athens katika Ligi ya Mabingwa.
Ikiwa ndivyo, Foden anaweza kupewa jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa. Ingekuwa vigumu kumchagua kuongoza safu ya ushambuliaji wakati alikuwa hajafunga kwa zaidi ya miezi 10. Sasa kipindi hicho kirefu cha kusubiri kimefikia mwisho.
“Nina furaha sana kwa bao lake, na natumaini litakuwa mwanzo tu wa mabao mengi na kiwango kizuri cha uchezaji,” anasema Maresca.
Foden alionyesha kuwa amepunguziwa mzigo mkubwa wa mawazo baada ya kufunga.
“Kwa kweli, nilikuwa nimechelewa kufunga bao. Nimepoteza nafasi kadhaa kubwa msimu huu. Jambo hilo limekuwa likinitesa sana, kwa hiyo ilikuwa vizuri kufunga,” anasema Foden. Kabla ya kutupia wavuni mpira wa krosi ya Doku, Foden alikuwa amepata nafasi za kufunga.
Katika Ligi Kuu England pekee, takwimu yake ya mabao yaliyotarajiwa kufungwa ilikuwa 1.56 msimu huu kabla ya mchezo dhidi ya Ipswich. Baada ya kufunga bao hilo, takwimu yake ikilinganishwa na nafasi alizopata baada ya bao lake la mwisho msimu uliopita ilikuwa 2.35.
Umaliziaji wake wa utulivu ulikuwa ukumbusho wa sifa alizoonyesha miaka iliyopita; uwezo wa kupima muda sahihi wa kukimbilia ndani ya eneo la hatari na kipaji cha kufunga mabao mengi.
Kurejea kwake katika kiwango kizuri pia kumekuja wakati unaofaa kwa sababu mashabiki wa City wamekuwa wakivuta hisia za watu zaidi, kufuatia mwitikio wao wenye rangi na kumbukumbu za zamani kuhusu hukumu 114 zilizotolewa dhidi ya klabu hiyo.
Foden alipoingia katika mahojiano baada ya mchezo, alikuwa amebeba ndizi kubwa ya kuchezea iliyojazwa upepo. Kitendo hicho kilikuwa ukumbusho kwamba yeye ni shabiki wa Man City, na kwamba kwa namna tofauti mwaka huu umekuwa wenye changamoto kwa mashabiki wengi wa klabu hiyo.