Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Filamu ya Makame usajili JKT tanzania, Yanga

Muktasari:

  • “Nakumbuka nilikuwa Dar es Salaam kwenye moja ya hoteli. Meneja wangu asubuhi alinipigia simu kuwa atanipitia twende kusaini mkataba Yanga.

“NILIKUBALIANA na Yanga kila kitu; gharama ya usajili, mshahara wangu kwa mwezi na kupata nakala ya mkataba kwa njia ya simu ili niusome kwa lengo la kuusaini mara baada ya kuonana kukamilisha dili hilo, lakini mambo hayakuenda sawa.

“Nakumbuka nilikuwa Dar es Salaam kwenye moja ya hoteli. Meneja wangu asubuhi alinipigia simu kuwa atanipitia twende kusaini mkataba Yanga.

Tumefika eneo la tukio tunasubiri kusaini mkataba, simu moja ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic, ilikatisha zoezi la kusainishwa kwangu mkataba,” ni sehemu ya mazungumzo ya beki wa JKT Tanzania, Laurian Makame alipozungumza na Mwanaspoti..

RAMOVIC ALIKWAMISHA USAJILI WAKE

Mwanaspoti lilikuwa sehemu ya kuripoti taarifa za aliyekuwa beki wa Fountain Gate, Makame, kuwa anaweza kutua Yanga msimu uliopita, lakini hadi dirisha linafungwa dili hilo halikufanyika. Makame amezungumzia sababu za kushindwa kuitumikia timu hiyo kuwa Ramovic ndiye aliyekwamisha.

“Simu ya kujiunga na Yanga nilipokea kutoka kwa Hersi (Said, rais wa Yanga). Nikamwambia siwezi kuzungumza chochote, nikamuunganisha na meneja ili waweze kuzungumza juu ya mahitaji yangu, kwa sababu meneja ndiye anafahamu kila kitu kunihusu mimi. Kazi yangu ni ku-cheza,” anasema na kuon-geza:

“Siku mbili mbele nilipokea simu kutoka kwa bosi wangu kipindi hicho, Mwigulu Nchemba, ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu wetu. Akanambia kuwa kuna ofa ya Yanga, je, wamenitafuta? Nikamjibu ndiyo wamenipigia. Akasema mmemalizana vipi? Nikamjibu nimewaunganisha na meneja. Mazungumzo yakaishia hapo.”

Anasema baada ya mazungumzo walipata nafasi ya kuzungumza meza moja, huku makubaliano yakiwa yamekamilika na ilifikia hatua hadi ya kutumiwa mkataba wa kusaini kwa njia ya simu ili aweze kuupitia kabla ya kuitwa kusaini.

“Huwezi kuamini hadi sasa nina mkataba wa Yanga kwenye simu yangu. Baada ya kuusoma niliitwa ofisi za Yanga, kipindi hicho nikiwa katika harakati za kuusaini, ilipigwa simu kutoka kwa kocha wa Yanga msimu huo, Ramovic, ambaye alisema nisisainishwe kwanza hadi anione nikicheza, kwani aliniona kwenye mchezo mmoja tu;

“Na huo ndio ulikuwa mwisho wangu wa makubaliano na Yanga kwani sikukubaliana na hilo nifanyiwe majaribio wakati tayari nina nafasi ya kucheza timu za ligi. Nalimwambia meneja wangu na Hersi kuwa siwezi kufanya hivyo, japo yeye kama kiongozi alijaribu kunishawishi niweze kusaini mkataba hata wa awali. Nilikataa.”


ALIFUNGUA POP KUWAHI USAJILI

Ukiondoa dili la Yanga kukwama, beki huyo alipata ofa nyingine kutoka Azam FC, lakini pia mambo hayakwenda kama yalivyopangwa kutokana na jeraha alilokuwa nalo kama anavyofunguka.

“Nakumbuka msimu uliopita, nikiwa Fountain Gate, sikumaliza mechi ya playoff baada ya kucheza ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons. Niliumia goti, lilipata shida kidogo, hivyo nilipewa mapumziko. Nikiwa nimefungwa POP nilipokea ofa Azam FC. Ili kutoshtukiwa, niliamua kutoa POP kabla ya muda husika ili niende kusajiliwa.

“Mambo hayakwenda sawa kwani kutokana na kutoa POP kabla ya muda mguu ulivimba sana na Azam FC waliniambia hawawezi kunisajili hadi wafanye vipimo. Na mimi nilikuwa nafahamu kuwa sipo sawa, hivyo nikaona nakwama kwani mambo hayapo sawa, na huo ndio ukawa mwisho wa ofa yangu,” anasema Makame.


FILAMU KUTUA JKT TANZANIA

Licha ya kwamba alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Fountain Gate, mambo yake ya kupata ofa ndani ya msimu huo kwake ilikuwa kama bahati, kwani licha ya kufeli Azam FC kutokana na majeraha, uongozi wa JKT Tanzania haukuzingatia hilo zaidi, kwani waliamini ni suala la muda na kuamua kunasa saini yake akiwa na jeraha hilo.

“Mambo yalikuwa mazuri upande wangu licha ya kukwama Azam FC kutokana na jeraha nililokuwa nalo. JKT Tanzania walinionea imani na kunisainisha mkataba kwa kuvunja mkataba wangu uliokuwa umebaki Fountain Gate. Sikutaka kuzungumzia hili la mkataba kwani lilizua utata, mambo mengi yalitokea siyo sawa kuweka wazi kwa sasa.

“Kikubwa ninachoweza kusema nawashukuru sana viongozi wa JKT Tanzania kwa kuniamini na kunipa mkataba ambao nautumikia hadi sasa. Nipo hapa kuipambania nembo ya hii timu. Malengo ni kuona inafanya vizuri msimu huu kwa kumaliza nafasi tano za juu.”


INONGA, BACCA MABEKI HASWA

Tanzania wamepita mabeki wengi bora wa kigeni waliocheza beki ya kati. Wamecheza kwa mafanikio na kuacha alama, lakini kwa upande wa Makame anamtaja Henock Inonga kuwa ndiye beki wake bora kwa miaka ya karibuni akimfananisha na Bacca.

“Kuna mabeki wengi bora na wanafanya vizuri, lakini nimekuwa nikimtazama Ibrahim Hamad ‘Bacca’. Ni beki mzuri, ana vitu vingi bora anavifanya uwanjani. Nimekuwa nikivichukua na kuvifanyia kazi ili niweze kuwa bora zaidi yake, na nimekuwa nikimfananisha na Inonga aliyewahi kucheza Simba; wana aina moja ya uchezaji,” anasema na kuongeza:

“Ili uwe bora lazima ukubali kujifunza na kuchukua mazuri kutoka kwa watangulizi wako. Nakubaliana na uwezo nilionao, lakini kuna sehemu najiona sitoshi. Hivyo namuangalia aliye bora kwangu ili nichukue ujuzi, nifanyie kazi niweze kuwa juu zaidi yake.”

Anasema Inonga na Bacca wanaendana kwenye aina ya uchezaji na ndio maana wote anawakubali; ni aina ya mabeki ambao anawataja kuwa wanacheza kwa kujiamini, hawatumii nguvu, wao akili nyingi.


BARES ALIMBADILI NAMBA

Si wachezaji wote namba wanazocheza sasa walianza nazo tangu wanajitafuta. Wengi wamebadilika ukubwani kutokana na aina ya makocha wanaokutana nao kama anavyothibitisha Makame ambaye ameweka wazi kuwa alianza kushambulia hadi sasa anakaba.

“Nikiwa najitafuta nilianza kucheza kama mshambuliaji, na baada ya kutua Mlandege kocha alikuwa Abdallah Mohamed ‘Bares’. Alianza kunitumia kama kiungo mkabaji na baadaye akanirudisha beki ya kati ambayo ndiyo nacheza hadi sasa na nafurahia kucheza eneo hili,” anasema na kuongeza:

“Ukiondoa beki mkabaji ambayo Bara ndio wananitambua zaidi kwa kucheza nafasi hii, nina uwezo wa kucheza beki ya pembeni na kiungo mkabaji. Ni nafasi ambazo nacheza kwa usahihi kwani tayari nimeshawahi kufanya hivyo huko nyuma.”


DAKIKA 90 ZILIVYOMPA MAISHA

Wachezaji wengi hasa wa Kizanzibari ukiondoa ligi wanayocheza mashindano ya Mapinduzi Cup ndiyo yamekuwa yakiwapa maisha kwa kuonwa na timu za Bara na kujikuta wanasajiliwa kama anavyodai Makame.

“Baada ya kumaliza dakika 90 mchezo wa fainali dhidi ya… nikiwa na Mlandege tulicheza dhidi ya Singida Big Stars. Simu ziliita sana kutoka timu za Bara, lakini Singida ndio walikuwa na kisu kikali,” anasema.

“Ukiondoa Singida, Dodoma Jiji pia walionyesha nia ya kunihitaji, lakini timu ambayo iliweka mkwanja mkubwa ndio niliyofanikiwa kusaini mkataba na kutua Ligi Kuu Bara.”

Makame anasema ubora aliouonyesha kwenye michuano hiyo ndio ulimpa nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara na kupata ofa nyingi ambazo fedha ndio ziliamua atue Singida.


URUBANI HADI SOKA

Si kila mchezaji anayecheza soka ndoto yake ilikuwa ni kuibukia huko. Licha ya wengi kuwa huko kutokana na mapenzi na mchezo huo, kwa upande wa Makame ameweka wazi kuwa alikuwa anatamani kuwa rubani wa ndege, matokeo yalimsaliti.

“Napenda sana mpira, lakini kabla ya kuwekeza juhudi zangu huku ndoto yangu ilikuwa ni kuwa rubani wa ndege, lakini matokeo ya kidato cha nne yalinisaliti na ndipo nilipoamua kuwekeza juhudi zangu huku,” anasema.

“Nisingeweza kutimiza ndoto ya kuwa rubani kwani matokeo hayakunipa nafasi ya kuendelea kusoma. Namshukuru Mungu soka limenikubali na sasa ndiyo linaniingizia kipato kwani ndiyo kazi ambayo imeniajiri. Bila mpira sina kitu kingine cha kufanya.”

Makame anasema soka kwa kiasi limemlipa; kuna matunda amevuna kupitia mpira japo bado anaamini ana safari ndefu ya kupambana zaidi ili kuweza kufikia malengo ambayo amejiwekea kimaisha.


KINA BANKA WAMVUTA

Achana na uwepo wa kina Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na mastaa wengine wengi ambao wanafanya vizuri Ligi Kuu Bara. Makame humwambii kitu kuhusu marehemu kiungo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam FC na Taifa Stars, Ibrahim Jeba; Abdi Kassim ‘Babi’ kiungo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa ‘Banka’.

“Nilipokea kwa furaha sana kujiunga na Singida Big Stars kwa sababu ndoto yangu ilikuwa ni kuona siku moja nacheza Ligi ya Bara, na kabla ya kutua nilikuwa nawafuatilia sana kina Babi, Banka na marehemu Jeba. Ni watu ambao walikuwa wananifanya niamini hata mimi siku moja nitacheza Bara,” anasema na kuongeza:

“Ukiondoa hao pia kwa sasa nawafuatilia kaka zangu walionitangulia, kina Bacca, Fei Toto, Mudathir. Wote nawatazama na najifunza mambo mengi kutoka kwao. Ukiondoa hayo pia ni washauri wakubwa kwangu hasa kwenye mambo yanayohusu soka kwani wao tayari wamekuwa wazoefu.”

SIRI YA BEKI, VIUNGO ZANZIBAR

Ukitaka beki bora wa kati na kiungo mzuri, vuka maji. Hiyo ndiyo kauli ya wadau wa soka kutokana na sehemu hiyo kutoa nyota wengi bora wa nafasi hizo kama anavyofunguka Makame.

“Ni kweli Zanzibar kuna viungo wengi na mabeki wengi bora hasa wa kati. Siri kubwa ni kutafuta nafasi ya kucheza Bara. Kwa miaka ya karibuni imebainika kuwa timu za Bara zinasaka wachezaji wengi kwenye nafasi hizo mbili kutokana na watangulizi kufanya vizuri.

“Kutokana na hiyo sasa wachezaji wengi wamekuwa wakikimbia nafasi wanazocheza na kujiweka kwenye mazingira mazuri kucheza nafasi ya kiungo na beki ya kati, wakiamini ndiyo njia sahihi ya wao kuvuka maji na kuja kujaribu bahati zao.”

Anasema wachezaji wengi wa Zanzibar wamefahamu kuwa Bara wanapenda viungo na mabeki, hivyo wamejikuta wengi wao wakibadili nafasi wanazocheza ili wawe bora kwenye maeneo hayo mawili. Lengo lao ni kutafuta nafasi ya kucheza Bara.