Eti Ntibazonkiza mzee…
BAADA ya kuondoka kiungo Gael Bigirima ambaye alikuwa amesajiliwa na Yanga akiwa na rekodi ya kuitumikia timu ya Newcastle United ya England, alibaki mchezaji mwingine mwenye wasifu mkubwa kwenye Ligi Kuu Bara.
Mchezaji aliyebaki anaitwa Saido Ntibazonkiza mfalme wa Burundi, huyu alikuja nchini na kuanza kuitumikia Yanga ambapo alifanya vizuri kwa kipindi kifupi ambacho alikaa hapo, kila mmoja anakumbuka.
Saido alipata heshima kubwa baada ya kutumika kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa akiichezea Caen ya huko na kuwa mchezaji pekee aliyecheza ligi kubwa zaidi kuwa hapa nchini kwa sasa.
Ukubwa wa ligi aliyoichezea unafanana na ukubwa wake akiwa uwanjani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, tayari kwa sasa ndiye mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi kwa msimu huu pamoja na kwamba amekuwa akipigiwa kelele nyingi na mashabiki wa timu hiyo kuwa hastahili kumaliza dakika tisini.
Juzi staa huyo alitoa pasi mbili za mabao kwa Pape Sakho katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting, pasi ambazo zinamfanya Saido kuhusika kwenye jumla ya mabao 22 ya Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa ndiye kinara kwa wachezaji wote 480 waliosajiliwa kwenye timu 16 msimu huu.
Saido alianza msimu akiwa na timu ya Geita ambayo aliitumika kwa miezi sita tu akiwa alitokea Yanga ambapo taarifa ambazo hazikudhibitishwa na uongozi ni kwamba mchezaji huyo alishindwa kuongezewa mkataba baada ya kutoroka kambini siku chache kabla ya mchezo wao dhidi ya Simba mkoani Mwanza.
Kabla ya kwenda Geita mashabiki waligawanyika mara tatu, wengine waliamini bado alikuwa anastahili kubaki Yanga na wengine waliamini kuwa Simba inaweza kuwa timu sahihi kwake lakini kundi la tatu liliamini hana uwezo kwa kuwa ni mzee.
Akiwa na Geita Saido alikuwa na kipindi kifupi kizuri ambapo alihusika kwenye mabao kumi, alifunga mabao manne na kutengeneza sita akiwa ndiye bora zaidi kwenye timu hiyo kwa miezi sita aliyokaa hapo.
Lakini baada ya kujiunga na Simba maneno mengi yalibebwa na neno kuwa sasa ni mzee na hawezi kuwa na makali tena kwenye Ligi Kuu Bara ambayo ina wachezaji wengi vijana.
Namba za Saido ambaye alifunga mabao 108 akiwa na Vital’ O hadi sasa ambapo tunafika mwishoni mwa msimu zinaonyesha kuwa hakuna mchezaji, awe kijana au mzee mwenzake aliyeweza kumfikia, ikiwa inaonyesha kuwa ni kiungo mshambuliaji wa kiwango cha juu zaidi kwenye ligi kwa sasa.
Baada ya kukaa Simba pia kwa miezi sita, ameonekana kukua zaidi kuliko alivyokuwa na Geita na Yanga baada ya kuhusika kwenye mabao 12, amefunga sita na kutoa pasi ya mabao sita, na jumla ya msimu ikiwa imebaki michezo miwili anakuwa na jumla ya mabao 10 na pasi 12 za mabao ukubwa wake unaonekana hapa.
Pamoja na kutajwa kuwa na umri mkubwa tofauti na jinsi inavyoonekana kwenye karatasi zake, staa huyo wa zamani wa NEC Nijmegen namba za msimu huu zinazifunika zile za msimu uliopita na kuonekana kuwa ndiye anayepanda vizuri zaidi.
Akiwa Yanga, Mrundi huyo ambaye amekuwa na umuhimu mkubwa kwenye timu ya Taifa ya Burundi alifanikiwa kufunga 10 katika michezo 18, ambayo ni nusu ya michezo ya msimu.
Wasifu wake unaonyesha kuwa ana miaka 36, lakini uwezo wake uwanjani kutokana na kile ambacho amekivuna kinaonyesha kuwa umri wake ni wa chini zaidi ya hapo.
Hat trick' yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu Bara akiwafunga Prisons ni moja ya jambo lingine ambalo linaonyesha kuwa bado anaweza kuitumikia timu nyingine ya Ligi Kuu Bara kama siyo Simba kwa msimu mwingine kutokana na wachezaji wachache kuweza kufanya hivyo.
Ntibazonkiza ambaye aliwahi kucheza soka Poland kwa miaka minne, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mpya msimu huu kufunga mabao matatu na kutoa asisti kwenye mchezo wake wa kwanza kwenye ligi na inaonekana ni rekodi ambayo inaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi kwenye ligi hii.
Kwa mashabiki ambao wamekuwa wakihudhuria mazoezi ya Simba hawawezi kukubaliana na yule atakayewaeleza kuwa mchezaji huyo ni mzee, nidhamu ya Saido, juhudi ambazo amekuwa akionyesha akiwa kwenye uwanjani wa mazoezi ni jambo pekee ambalo linaweza kumshawishi kocha yeyote kumpa jezi kwenye mchezo unaofuata.
“Ni kati ya wachezaji imara wenye nidhamu nzuri, kuishi na Saido siyo jambo gumu anafahamu zaidi kuhusu nini anatakiwa kufanya kwa wakati gani, lakini tazama hata uwanjani huwezi kumuona akiwa na nidhamu mbovu.
“Unaweza kuhesabu amepewa kadi mara ngapi? Ni kati ya wachezaji wetu wenye nidhamu nzuri uwanjani, hata mchezaji mwenzake akiingia kwenye mabishano na yule wa timu pinzani yeye huwa wa kwanza kwenda kumaliza ugomvi, kwani naona ni mtu sahihi,” aliwahi kusema meneja wa Simba Patrick Rweyemamu.
Pamoja na uwezo wake uwanjani, lakini kila mmoja anakumbuka kuwa ni mchezaji pekee ambaye baada ya kumalizana na Yanga bado alionyesha nidhamu ya juu na kwenda mazoezini kuwaaga wenzake ambapo waliweka duara moja akazungumza na kuondoka, Simba bado anaweza kwenda kuwika kwingine.