Ester Bulaya; Sio ubunge tu, hata uwanjani yupo
Muktasari:
- Na licha ya kuwa shabiki wa mabingwa watetesi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, pia ni mtetezi wa kweli wa soka la wanawake na miongoni mwa wadau walioweza kupigia kelele thamani ya mwanamke katika michezo.
MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, ni miongoni mwa wanawake viongozi wachache waliokua katika familia ya wazazi wapenda michezo.
Na licha ya kuwa shabiki wa mabingwa watetesi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, pia ni mtetezi wa kweli wa soka la wanawake na miongoni mwa wadau walioweza kupigia kelele thamani ya mwanamke katika michezo.
Kutokana na hayo, mbunge huyo unaweza kumuita jasiri, kwani alivumilia changamoto nyingi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia hata katika nafasi za juu za kiuongozi, lakini alifanikiwa kupenya na sasa ni mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini katika Bunge.
Bulaya ni mmoja wa wanawake wachache waliopata fursa na kuitumia vizuri bila uoga wala kusema hapana mahali ambapo wengine waliogopa. Kupitia Mwanaspoti, anawashauri wanawake wakiwamo wanamichezo kuwa wanaweza kufanya lolote na wakafanikiwa.
Pia anaweka wazi kuwa unyanyasaji wa kijinsia haupo kwenye michezo tu, bali karibu kila mahali ambapo mwanamke anajaribu kufikia mafanikio, lakini haupaswi kupewa kipaumbele wala kumfanya mwanamke asipiganie ndoto zake.
SAFARI YA MAFANIKIO
Bulaya anasema siasa haikuwa kwenye ndoto zake, lakini kuna watu waliokuwa wanaziona kazi zake za uandishi wa habari na wakavutiwa na namna alivyokuwa akifanya kazi ya kuihabarisha jamii.
“Mimi ni mwandishi wa magazeti, lakini wengi walikuwa wanaona kama nafaa sana kwenye utangazaji wa televisheni. Ila sikuwa na ndoto za kisiasa. Lakini, kutokana na uchapakazi wangu, wengi waliona nafaa sana kwenye upande huo hadi viongozi wa vyama mbalimbali (vya siasa)," anasema mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza 2010 kama mbunge wa viti maalumu kupitia CCM nafasi aliyoitumikia hadi 2015.
“Ndipo taratibu nikaanza kujihusisha na uongozi wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tawi la Uhuru. Nikaanza kupata mafunzo na taratibu nikajikuta nimefika hapa.”
Mwaka 2015, kutokana na uthubutu na kutojiona mnyonge ari aliyokuwa nayo na ambayo anatembea nayo hadi sasa, aliamua kugombea ubunge wa Bunda Mjini kupitia Chadema na kufanikiwa kushinda hadi 2020 aliporejea katika viti maalumu kwa mara nyingine kupitia chama hicho.
Na katika uchaguzi mkuu wa 2025, alirudi tena Bunda akipeperusha bendera ya CCM na kushinda, ambapo ndiye mbunge wa jimbo hilo kwa sasa.
MICHEZO ILIANZA HIVI
Mbunge huyo anasimulia mapenzi yake katika michezo kwamba yalianza tangu utotoni kutokana na familia yao kuipenda fani hiyo. Hata alipokuwa mtu mzima aliendelea kucheza, hasa mchezo wa netiboli ambao amekuwa akiucheza hadi hasa.
“Mimi michezo ni tangu nipo utotoni. Hata nilipoanza kazi Uhuru na Mzalendo upande wa magazeti, nilikuwa nahodha wa timu ya netiboli," anasema mwanahabari huyo.
“Hata nilipokuwa mbunge niliendelea kucheza, na aliyenivutia zaidi alikuwa marehemu mama yangu, Bi Khadija, ambaye alikuwa mchezaji mzuri wa netiboli.”
Kutokana na mapenzi katika mchezo huo, Bulaya ameendelea kucheza netiboli ikiwamo katika timu ya Bunge ambako moto aliokuwa nao zamani huuonyesha mara moja moja anapopata nafasi inapokuwa na michezo mbalimbali.
MAPENZI NA YANGA
Bulaya anasema mapenzi yake na Yanga yalianzia kwenye familia, kwani wazazi wake wote walikuwa mashabiki wakubwa wa klabu hiyo na hata yeye alijikuta akiipenda na kuendelea kujivunia kuwa mwananchi hadi sasa.
“Familia yetu ilikuwa Yanga. Kwa hiyo nikajikuta nimekuwa shabiki. Nilifikia hatua hata (Yanga) wakifungwa nashindwa kufanya kazi za shule," anasema.
“Kwa mara ya kwanza baba yangu alinichapa kwa sababu ya Yanga baada ya kushindwa kufanya kazi ya shule. Mimi naipenda Yanga sana, na tukifungwa nakosa raha. Hata dabi ya juzi niliteseka sana. Mechi yoyote ya Yanga dhidi ya Simba au Azam napata wakati mgumu.”
Mnunge huyo anasema hata jimboni kwake wananchi wanajua kwamba yeye ni shabiki kindakindaki wa burudani inayotolewa na mastaa wa Yanga.
“Wananchi wangu na viongozi wanajua mimi ni Yanga. Kuna wakati mashabiki wa Simba wanakuja kutaka mchango na huwa natoa," anasema Bulaya akizungumzia namna ushabiki wake kwa Yanga usivyomtenganisha na jamii.
“Raha ya Yanga ni kuifunga Simba, lakini wanapokuja wananchi wangu wa timu tofauti huwa naungana nao ili kuondoa utofauti. Naona kabisa (msimu huu) klabu zimefanya usajili mzuri unaowapa furaha Watanzania.”
HADHI YA MWANAMKE
Kwa mbunge Bulaya ambaye amepitia changamoto mbalimbali hadi kufika alipo sasa hakosi kuwatia moyo wanawake wenzake kupambani ndoto na hadhi yao maishani.
Mbunge huyo anaeleza jinsi alivyopambana kuhakikisha soka la wanawake linapata heshima na pia umuhimu wa kinadada kujihusisha na michezo ikiwamo soka ambako kuna fursa nyingi zinazoweza kuwafungulia milango ya maisha.
“Wakati soka la wanawake linaanza hakukuwa na mwamko mkubwa kama sasa. Leo ni ajira. Tuna watu kama Aisha Masaka ambaye yuko Women's Super League. Zamani hata mimi bungeni nilikuwa nasema soka la wanawake halithaminiki, lakini sasa kuna mabadiliko. Tuna watu kama Clara Luvanga, bila mpira angekuwa wapi?
“Kikubwa (wanasoka wa kike) wapate watu wa kuwalea na wasione kama wao ni chaguo la pili baada ya wanaume kwa sababu wanaipa nchi heshima.”
Na ni kutokana na mafanikio ambayo soka la wanawake limefikia kiongozi huyo anasema hata mafanikio ya timu ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' yanaonyesha uwezo mkubwa wa wanawake katika michezo.
Hata hivyo, Bulaya anasema kwa sasa hana ndoto ya kugombea uongozi wa soka, kwani kiti alichonacho cha kuwatumikia wananchi wa Bunda Mjini kinamtosha.
Anasema: “(Viongozi) waliopo wanatosha na wanafanya vizuri. Nimesikia kiongozi wa sekta ya michezo Paul Makonda akisema anataka michezo mingine ikue kama mpira wa miguu.”
MAFANIKIO YAKO HAPA
Akizungumzia kwa ujumla mchezo wa soka na mingineyo, Bulaya anasema mafanikio yataonekana zaidi ikiwa kutakuwa na uwekezaji mkubwa kwenye kukuza vipaji kuanzia utotoni kupitia akademi na hivyo ni wajibu wa wadau kuwekeza katika eneo hilo.
“Kwenye jambo lolote lazima kuwe na mfumo mzuri wa kujenga msingi. Nchi kama Senegal zina vipaji vikubwa (vya soka) kwa sababu ya mifumo yao," anasema.
“Hata Tanzania kuna vipaji vingi, lakini misingi bado ni changamoto. Angalia Azam FC inavyovuna vipaji kupitia akademi yake, kama Aishi Manula na wengine.”
TUKIO ASILOSAHAU
Bulaya anakumbuka tukio moja kubwa wakati wa michuano ya mabunge ya Afrika Mashariki, ambapo alikuwa mmoja wa mastaa wa timu ya Bunge la Tanzania.
“Nakumbuka michuano ya mabunge ya Afrika Mashariki, nahodha (wa timu yao) alikuwa Halima Mdee. Tulipitia changamoto nyingi lakini (Tanzania) tulishinda mbele ya Yoweri Museveni (rais wa Uganda).
“Baada ya ushindi watu walilia kwa furaha. Hayo ni miongoni mwa mafanikio makubwa niliyoyapata kwenye michezo.”
SIO SOKA TU
Mbunge huyo anasema anapenda michezo mingi na hufurahi anapouona ushindani baina ya pande zinazoshindana.
“Napenda kucheza karata, volleyball (mpira wa mikono) na tenisi. Nilikuwa shabiki mkubwa wa Serena Williams (staa wa zamani wa tenisi duniani) na hata nimejaribu kucheza.
“Mieleka napenda kuifuatilia, lakini sichezi. Wakati naandika magazetini nilikuwa nafanya sana makala za michezo na burudani.”
Mbunge huyo anasema licha ya kuipenda michezo na burudani, lakini maendeleo ya teknolojia yanakuja kwa kasi na pia yana faida na hasara zake.
“Kila kitu kina faida na hasara. Teknolojia ni nzuri kama itatumika kwa manufaa chanya. Vijana wa sasa wana fursa kubwa kupitia teknolojia, hasa katika sanaa na michezo,” anasema Bulaya akiwasihi vijana kutojitenga na teknolojia, bali kuitumia kwa manufaa ya kuwaingizia vipato.
Akizungumzia uhusiano wa jamii na michezo, mwanahabari huyo anasema kwamba mara zote husaidia kujenga daraja bora kati ya mtu na mtu na jamii kwa ujumla.
Anasema, “michezo inaleta furaha na mshikamano katika jamii. Timu ya taifa ikifanya vizuri unaona nchi nzima inafurahi. Michezo pia inapunguza migogoro na ni chanzo cha ajira kwa vijana.”
SIRI YA UREMBO
Unapokutana na Bulaya huwezi kumtofautisha na binti mwenye umri mdogo licha ya kwamba kwa sasa umesogea.
Anasema mwonekano wake unatokana na kujipenda na kwamba hakukuibuka tu kama uyoga, bali ni jambo alilolipenda tangu zamani, na kuna wakati aliwahi kusimamia mashindano ya urembo mkoani Morogoro, ingawa hakufika mbali kutokana na majukumu yake mengine.
“Wanawake tumeumbwa hivyo. Lakini, kwa upande wangu pia (urembo) unachangiwa na majukumu yangu kama kiongozi, na lazima niwe mfano. Huko nyuma niliwahi kufanya mambo ya urembo Morogoro japokuwa sikugombea (fani ya urembo). Nilipata nafasi ya kuwasimamia warembo wakati huo," anasema na kuongeza:
“Unapokuwa nadhifu kila wakati inakusaidia kujiamini, hasa unapokuwa mbele za watu.”
USHAURI KWA WANAWAKE MICHEZONI
Bulaya anasema wanawake wanaofanya kazi katika soka na michezo mingine hawapaswi kujiona wa kawaida, bali wajipe thamani.
“Hapo zamani ilionekana mwanamke akicheza soka ni kama mwanaume au mhuni, lakini sasa mambo yamebadilika.
“Nina timu ya wanawake kule Bunda. Ni mabinti wazuri wanajipenda na wanacheza mpira wa miguu kwa sababu ni kazi kama zilivyo nyingine," anasema mbunge huyo.
“Ni muhimu kuwe na utaratibu wa kulinda mabinti ili wasinyanyasike wanapotafuta fursa.” Jimboni Bunda kuna timu ya wanawake ya Bunda Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
CHANGAMOTO KUBWA
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Bulaya pia anagusia suala la kunyanyapaliwa kiungozi katika medani za kisiasa, akisema lingalipo, lakini wanawake hawana budi kupambania ndoto zao.
“Kwenye siasa kuna mambo mengi, lakini kunyanyapaliwa katika uongozi ni changamoto kubwa. Watu wanaona mwanamke hafai kuwa kiongozi," anasema.
“Nilipoanza ubunge tulipelekwa Uingereza kujifunza namna wanawake wanavyoweza kushinda katika uongozi.”
Bulaya anawapa ujumbe wanawake wanaotamani kufika mbali katika uongozi akiwataka kujitambua na kufanya mambo kwa ukubwa wake.
“Mwanamke jitambue na uwe na malengo. Usisikilize wanaokukatisha tamaa, bali chukua maneno yao kama chachu ya kupambana. Mimi mtu akiniambia siwezi nachukua kama chachu ya kumuonyesha kwamba naweza," anasema.
“Sisi kufika hapa tumepitia mengi. Kuna mambo unaweza kusema na mengine huwezi, lakini hata ukilia peke yako unafuta machozi na kutoka na ujasiri mpya kuhakikisha malengo yanatimia.”